HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 21 January 2019

Wahamiaji haramu 35 wakamatwa jijini Dar

WAHAMIAJI haramu 35 kati ya 81 wamekamatwa wakiuza pipi, karanga na kahawa na kujifanya machinga. Akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake, Kaimu Afisa Uhamiaji mkoa wa Dar es Salaam, Mrakibu Novaita Mrosso alisema kati ya watu hao 35 ni raia wa Burundi ambao walikuwa wanafanya biashara hiyo kama machinga kwa kutembeza sehemu mbalimbali.

Wahamiaji hao, wamekamatwa mwishoni mwa wiki na Idara ya Uhamiaji wakifanya biashara hiyo jijini Dar es Salaam. Operesheni kali imekuwa inafanyika jijini zima ili kuhakikisha wahamiaji wote wanatiwa mbaroni ambapo wahamiaji hao baadhi wamejifanya machinga kukwepa kukamatwa. Hatua hiyo, imekuja baada ya mwishoni mwa mwaka jana, Rais Dkt. Magufuli kutoa vitambulisho maalum kwa ajili ya kuwatambua wafanyabiashara wadogo wadogo nchini ambapo kila Mkuu wa Mkoa alikabidhiwa.

Vitambulisho hivyo jumla 25,000 na kila kitambulisho kitagharimu shilingi 20,000 kwa machinga. Uhamiaji imeingia kazini baada ya kugundua kuwa wapo baadhi ya wahamiaji haramu wamekuwa wanafanya biashara kama wamachinga na kazi hiyo ilifanyika Januari 17, mwaka huu hadi Januari 20 ambapo jumla ya watu 81 walikamatwa.

Mrakbu Mrosso alisema wahamiaji hao wamekuwa wanauza kahawa, karanga, pipi na vitu vidogo sehemu mbalimbali za jiji huku wakijifanya kama sehemu ya machinga kujificha.

"Tumewanasa na wanafikishwa mahakamani haraka kisha watarudishwa kwao,"alisema. Aliongeza kuwa bado wanaendelea kuwahoji wahamiaji wengine 46 kujua wanatoka nchi gani na kujua uhalali wao wa kuwepo hapa nchini. "Hapa tumebaini wapo wasomali,wanigeria, Mcameroon na wengine,"alisema. Mrakibu Mrosso alisema kazi ya kuwasaka wahamiaji haramu ni endelevu na wamekuwa wanashirikiana na viongozi wa serikali za mitaa ili kuwabaini wote.

"Nawaomba watu wenye taarifa watupe habari, sisi tutaendelea kuwaficha wale wote wanaopa ushirikiano ili kuwakamata wahamiaji,kamwe hawaponi tutawakamata wote na wale wanaowaleta,"alisema. Pia, amewaomba viongozi walioajiri wageni kutoa taarifa kwa vile hivi sasa wanaendelea na kazi ya kupitia kila sehemu ikiwemo viwanda,ofisi, baadhi ya makazi ili kuwanasa wageni wote wanaoishi kinyemela.

Alisema wamefanya kazi hiyo toka Novemba na Disemba,mwaka jana na kuhakiki jumla ya wageni 16,102 ambapo 7,000 walihakikiwa katika ofisi ya mkoa.Wengine 3,613 walihakikiwa katika ofisi ya Ilala, 3,668 Kinondoni,1,267 Temeke,356 Ubungo na 198 Kigamboni. Mrakibu Mrosso alisema kwenye zoezi hilo,wamefanya utambuzi na uandikishaji wa raia wa Malawi na wahamiaji walowezi ambapo jumla waliandikishwa ni 1,770.

Kwenye mabao Kinondoni(756),Ilala (548)Temeke(162),Ubungo (144) na Kigamboni ni 150. Ametoa onyo kali kwa wananchi wanaohifadhi wahamiaji haramu kuacha mara moja kwa vile mali zao na kifungo huenda kikawakumba. "Unajua sheria imebadilika hivi sasa kifungu cha 46 cha sheria uhamiaji sura ya 54 rejeo la 2016,mtu akikamatwa amehifadhianaweza kufungwa miaka 20,gari au nyumba inataifishwa pia na adhabu zote zinaweza kuwa za pamoja,"alionya.
 Wahamiaji haramu waliokamatwa mkoa wa Dar es Salaam wakiwa wamechuchumaa  baada ya kufikishwa makao makuu ya uhamiaji.(Picha na Emmanuel Massaka,MMG)
Kaimu Afisa Uhamiaji  jijini Dar es Salaam, Novaita Edmund Mrosso akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wahamiaji haramu  waliokamatwa  maeneo mbalimbali ya jijini Dar es Salaam .
Kaimu kamishina wa Uhamiaji jijini Dar es Salaam,Novaita Edmund Mrosso akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.


No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad