HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, 20 January 2019

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAANZA KUUGEUKIA UTALII WA FUKWE

NA. LUSUNGU HELELA- KIBAHA
Wizara  ya Maliasili na Utalii, imeanza kuyatambua na kuainisha maeneo kwa ajili ya utalii wa Fukwe katika Kisiwa cha Mafia mkoani Kibaha kwa ajili ya kuhamasisha Wawekezaji kuchangamkia fursa ya ujenzi wa Hoteli za kitalii ili kuwavutia watalii kutembelea katika kisiwa hicho.

Hatua hiyo inakuja ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliyoyatoa mwaka jana kwa Wizara hiyo  kuwa ianzishe Kurugenzi ya Fukwe itakayokuwa na jukumu la kusimamia na kuendeleza  Fukwe zote nchini.

Lengo likiwa ni kuhakikisha mapato yatokanayo na sekta ya Utalii kupitia Utalii wa Fukwe yanaongezeka kwa mfano Kisiwa cha Mafia ni cha tano duniani kwa uzuri wa vivutio vya utalii na rasilimali bahari na  cha pili barani Afrika, Hivyo kina sifa kemkem za kuongeza pato la Taifa zaidi.

Akizungumza mara baada ya kufanya ziara ya siku mbili kisiwani humo ya kutembelea Fukwe pamoja na magofu ya kale,  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu  amesema Wizara imejipanga kikamilifu kwa ajili kuwasaidia  Wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kwenye Fukwe kwa ajili ya utalii.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Kanyasu alitembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii vilivyopo kisiwani humo ukiwemo Msitu wa Mlola, Magofu na fukwe katika kijiji cha Kanga  pamoja na maeneo ya uwekezaji ya Ras Mlundo Jojo, Banja, Rasini Kanga na Tembo Unyama.

Hata hivyo, Baada ya ziara hiyo Naibu Waziri huyo alisema kuwa baadhi ya wamiliki wa maeneo hayo ya fukwe yamefanya kuwa mashamba ilhali ni kivutio kikubwa cha utalii ambapo baadhi ya nchi zimekuwa ziikingiza fedha nyingi za kigeni kupitia utalii wa fukwe.

Aidha, Kanyasu amewataka wananchi wanaomiliki maeneo karibu na Fukwe kuyatumia kwa ajili ya utalii wa fukwe  badala ya kuyageuza kuwa  mashamba.

Amesema kuwa watalii walio wengi kutoka nje za nchi mara baada ya kutembelea Hifadhi za Taifa kama vile Serengeti Mikumi, husafiri kwenda Msumbiji au Zanziba' kwa ajili ya kutembelea Fukwe ilhali kuna fukwe nzuri mbali na Kisiwa cha Mafia ambazo hazijaweza kuendelezwa

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Shaib Nnunduma alieleza kuwa wilaya yake inawakaribisha Wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika wilaya hiyo na kuahidi kuwa atatoa ushirikiano wa kutosha.

Aliongeza kuwa Wilaya hiyo tayari imeshatenga maeneo kwa ajili ya Wawekezaji kwa ajili ya ujenzi wa Hoteli za kiutalii katika maeneo ya ufukweni.
  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ( watatu kulia)  akiwa pamoja na kamati ya ulinzi na usalama akipewa maelezo na Kaimu Mkurugenzi wa Ardhi, Maliasili na Utalii, Juma Hassan kuhusu eneo la fukwe lililotengwa kwa ajili ya  uwekezaji  wa  ujenzi wa Hoteli za kitaliii wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea kwa ajili ya kuhamasisha utalii wa Fukwe katika wilaya ya Mafia mkoani Kibaha. 
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu akizungumza na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mafia, Mohammed Kongo wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea maeneo ya fukwe ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliyoyatoa mwaka jana kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa 
ianzishe Kurugenzi ya Fukwe 
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,  Constantine Kanyasu akishuka kwenye ndege  ndogo wakati alipowasili  wilayani Mafia mkoani Kibaha  kwa ajili ya kutembelea maeneo ya fukwe kwa ajili ya uwekezaji wa Utalii
 Baadhi ya rasilimali bahari maarufu kwa jina la  Matumbawe ambayo ni miongoni mwa vivutio vya utalii katika kisiwa cha Mafia mkoani Kibaha
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu (  kulia)  akiwa ameongozana na Mkuu wa wilaya ya Mafia pamoja na kamati ya ulinzi na usalama  wakati wa ziara ya kutembelea maeneo ya fukwe yanayofaa kwa ajili ya uwekezaji lengo likiwa ni kuhasisha utalii wa fukwe 
 Moja ya magogfu ya kale lililojengwa karne ya 18 ambalo linapatikana pembezoni mwa fukwe katika kisiwa cha Mafia mkoani Kibaha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mafia. Erick Mapunda akisoma taarifa ya wilaya hiyo kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu kabla hya kufanya ziara ya kutembelea maeneo ya fukwe kwa ajili ya uwekezaji wa utalii.  

  (PICHA ZOTE NA LUSUNGU HELELA-MNRT)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad