HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 28 January 2019

WAZIRI KAMWELWE AIPA MIEZI SITA SHIRIKA LA POSTA KURUDISHA MALI ZOTE

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe ameuagiza uongozi wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) kurudisha mali zote za Shirika hilo ikiwemo viwanja, majengo ndani ya miezi sita zilizopo kwenye maeneo mbali mbali nchini nzima
Kamwelwe ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha 26 cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania kilichofanyika Dar es Salaam ambacho kimejumuisha viongozi na wawakilishi wa Baraza hilo kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar ambapo Shirika hilo lina mtandao wa miundombinu yake na inatoa huduma za mawasiliano ya posta, vifurushi na vipeto kwa wananchi
“Ifikapo tarehe 30 Juni mwaka huu wa 2019 mali zote za Shirika ziwe zimerudi kuwa mali ya Shirika la Posta Tanzania, hata kama mliuziana zirudi, hizi ni mali za Serikali na ninyi hamtakuwa wa kwanza kurudisha majengo, viwanja kwa kuwa wenzenu wa Shirika la Reli Tanzania wamerudisha,” amesisitiza Kamwelwe
Pia, ameuagiza uongozi wa Shirika hilo ndani ya kipindi hicho cha miezi sita, kuhakikisha kuwa Wilaya zote 186 nchi nzima ziwe na huduma za posta. Aidha, amewataka kupitia kikao cha Baraza hilo, wajadiliane kuhusu utekelezaji wa jambo hilo na bajeti watakayoijadili iwe na mwelekeo huo. Amesisitiza kuwa TPC ina watumishi wengi wapatao 821 nchi nzima hivyo wafanyakazi kazi kwa bidii, wawe wabunifu na wachape kazi kwa kuzingatia taaluma zao ili kuongeza ufanisi, tija, ukuaji na maendeleo ya Shirika ili waweze kuwahudumia wananchi. Amewaagiza kuhakikisha kuwa wanatumia mifumo ya kielektroniki kusafirisha fedha badala ya kutumia mfumo wa zamani wa wafanyakazi kushika pesa za mauzo, makusanyo na mapato mkononi
Amesema kuwa anaushukuru uongozi wa Shirika hilo kwa kuendelea kulipa deni la wastaafu ambalo limefikia kiasi cha shilingi bilioni 6.5 na amewaahidi kushirikiana nao ili Serikali iweze kurudisha fedha zao na amekiri kuwa Shirika limeiokoa Serikali na kuficha aibu hiyo. Pia, amewaahidi kulifanyia kazi deni la shilingi bilioni 12 ambapo amesema kuwa anahitaji kuelimishwa ili alielewe aweze kwenda kuwafahamisha wabunge ili waridhie na watoe kibali cha kulipa deni hilo
Katika hatua nyingine, ameuelekeza uongozi wa Shirika hilo kutumia miundombinu ya postikodi iliyopo sehemu mbali mbali nchini ili kufanikisha na kuharakisha utoaji wa huduma za mawasiliano ya posta kwa wateja wake kwa kuwa watanzania wana imani na Shirika lao na lina mtandao mpana nchi nzima
“Huduma ziwafikie watu wa vijijini haraka ili kuwapunguzia gharama na kero za kwenda mjini kufuata huduma ili kurahisisha uendeshaji wa kila siku wa maisha ya wananchi na mafanikio ya Shirika hili yaguse watanzania wote, ikitokea umepoteza nyaraka, mteja lazima ajibiwe haraka, kama umepoteza, lipa,” amesisitiza Kamwelwe.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo, Kanali mstaafu Dkt. Haruni Kondo amemweleza Kamwelwe kuwa Shirika halijapewa mtaji na Serikali ila anawapongeza wafanyakazi kwa ushirikiano wao na kwa kulifikisha Shirika hapo lilipo kwa kuwa wanadai deni la shilingi bilioni 6.5 Serikalini kwa kulipa wastaafu
“Deni tunaloidai Serikali la kulipa wastaafu linatutesa sana, tunajua nguvu zako, tunakuomba utusaidie”, amesisitiza Kondo. Pia, ameongeza kuwa anamuomba Kamwelwe alisaidie Shirika kuondolewa kwenye orodha ya mashirika ya umma yaliyowekwa chini ya uangalizi ili Shirika liweze kutekeleza majukumu yake kwa kuwa ni Shirika kubwa ambalo limelala
Akitoa taarifa ya Shirika hilo kwa Kamwelwe, Posta Masta Mkuu wa Shirika hilo, Hassan Mwang’ombe amesema kuwa tayari Shirika limejiunga na mfumo wa malipo wa Serikali kwa njia ya kielektroniki (eGPG) ili mteja anapolipia alipie kwa urahisi na kuliwezesha Shirika kuona mapato yake yote kwa njia ya mtandao kwa kuwa malipo yatakuwa yanafanyika kwa njia ya kielektroniki na huduma zitaanza ndani ya wiki moja
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe akisisitiza jambo kwa wajumbe wa kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania wakati akifungua rasmi kikao hicho, Dar es Salaam. Wakisikiliza kwa makini viongozi wa Shirika hilo, wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi, Kanali mstaafu Dkt. Haruni Kondo na wa kwanza kulia ni Posta Masta Mkuu, Hassan Mwang’ombe.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Posta Tanzania Kanali mstaafu Dkt. Haruni Kondo akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe (wa kwanza kulia) wakati wa kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo. Anayesikiliza kwa makini ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Wizarani, Kitolina Kippa.
 Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Hassan Mwang’ombe akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe ( wa pili kushoto) baada ya ufunguzi wa kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo, Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi, Kanali mstaafu Dkt. Haruni Kondo na wa tatu kulia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Wizarani, Kitolina Kippa (wa tatu kulia)
 Baadhi ya wajumbe wa kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania wakiimba wimbo maalumu wa wafanyakazi kabla ya ufunguzi wa kikao hicho uliofanywa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe (hayupo pichani)
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe (katikati mstari wa mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania baada ya kufungua kikao hicho, Dar es Salaam. Viongozi wa Shirika hilo wakiwa kwenye picha hiyo, wanne kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi, Kanali mstaafu Dkt. Haruni Kondo na wa nne kulia ni Posta Masta Mkuu, Hassan Mwang’ombe 

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad