HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 23 January 2019

WATENDAJI WATAKIWA KUYAFANYIAKAZI MAAGIZO WANAYOPEWA

Na Sekela Mwasubila, Afisa Habari Kondoa Mji
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa Msoleni Dakawa amewataka watendaji wa kata na mitaa kuyafanyia kazi maagizo yanayotolewa kutoka halmashauri kwani wananchi wana imani nao katika kuwaletea maendeleo.

Aliyasema hayo wakati akifungua kikao kazi kati ya watendaji hao na wakuu wa Idara kilichofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Uwekezaji Kondoa Mjini. Alisema kuwa watendaji hao ndio wasimamizi na wakurugenzi katika maeneo yao ya kazi hivyo wanapaswa kuwajibika ili kuhakikisha kata na mitaa yao inakuwa na maendeleo na huduma za msingi zinapatikana.

“Mkifanya vibaya nyie halmashauri yote itaonekana imefanya vibaya sababu tunafanya kazi kama timu ila nasikitika watumishi ngazi ya wilaya wanafanya sana kazi lakini ikifika kwenu hamfanyi kazi na kutimiza majukumu yenu mjitathmini.”Alisema Dakawa

Aidha aliongeza kwa kuwataka kusimamia miradi ya maendeleo na ukusanyaji wa mapato na kuwachukulia hatua wale wote ambao miradi itatekelezwa chini ya kiwango  na wao kutochukua hatua zozote kwa kisingizio cha kutokushirikishwa kwani miradi yote ipo chini yao.

“Pia kuna watendaji hapa nimepata habari ni wababe kwa wenyeviti wao wa mitaa hadi wanaogopwa hii haipendezi mkafanye kazi kwa kushirikiana lengo liwe moja tu kuwaletea maendeleo wananchi.” Alisisitiza Dakawa

Kwa upande wake Afisa Sheria wa Halmashauri Wakili Edward Mhina aliwataka watendaji kuepuka tabia ya kuingia mikataba na watu mbalimbali bila kushirikisha ofisi ya Mkurugenzi kwani mikataba yote ambayo haijapitiwa na Mwanasheria ni batili.

“Nawakumbusha watendaji ambao walipewa mashine za kukusanyia mapato na hawakupeleka fedha benki kufanya hivyo ndani ya wiki moja hadi jumatano ijayo wote wapeleke fedha benki ambao hawatapeleka tutawafikisha mahakamani.”Alisema Mhina

Akiongea kwa niaba ya watendaji Mtendaji wa Kata ya Kingale Samson Mtui aliushukuru uongozi wa halmashauri kwa kikao kazi hicho kwakuwa kimewakumbusha majukumu yao ambayo mengi walikuwa wakiyafanya kinyume na kuahidi kwenda kufanya kazi kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni.

Kikao kazi cha uongozi wa halmashauri na watendaji wa kata na mitaa kimefanyika kwa lengo la kuwakumbusha majukumu yao na kupatiwa mada mbalimbali kutoka idara na vitengo vya sheria, Manunuzi, Fedha,Mipango, Elimu Sekondari na Utumishi.
 Mkurungezi wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa Msoleni Dakawa akisisitiza jambo wakati wa kikao kazi cha wakuu wa Idara na Watendaji wa kata na mitaa
  Watendaji wa kata na mitaa wakisikiliza kwa makini mada zilizowasilishwa katika kikao kazi kati yao na wakuu wa Idara.
 Afisa Mipango wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa Kaunga Amani akiwasilisha mada ya usimamizi wa miradi kwa watendaji wa kata na mitaa

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad