HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, January 6, 2019

UVCCM YASEMA WANASIASA UCHWARA HAWAJIAMINI

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) umesema ukuaji wa Demokrasia umetoa fursa pana kwa kila mwananchi kufanya mambo yake kwa uhuru bila usumbufu wa aina yoyote katika jamii. 

Umebainisha kuwa wapo baadhi ya wanasiasa uchwara wanaokesha wakiwaaminisha na kuwapotosha Wafuasi wao kuwa Demokrasia imebinywa jambo ambalo sio la kweli kwani Demokrasia isingekuwepo hata hizo Kauli wanazotoa zisingeweza kusikika nchini. Hayo ameyasema Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar  Mussa Haji Mussa katika hafla ya uzinduzi wa Matembezi ya kuyaenzi Mapinduzi ya mwaka 1964,ambapo hafla hiyo imefanyika katika Kijiji cha Chokocho Wilaya ya Mkoani Pemba. 

Alisema wanasiasa wanaoilalamikia serikali kuwa imebana Demokrasia ni wale waliozoea siasa za vurugu, vitisho na migogoro ya kisiasa hivyo kwa sasa wanaona hawana tena nafasi ya kufanya matukio ya aina hiyo ndio maana wanalalamika na kueleza bila aibu kuwa Tanzania na Zanzibar kwa ujumla hakuna demokrasia na uhuru wa kutoa na kupkea habari. 

Naibu Katibu Mkuu huyo wa UVCCM Mussa alisema Utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 umeenda sambamba na matakwa ya ASP katika upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi nchini.  Amesema mbali na kuimarika kwa huduma za kijamii na kiuchumi kwa asilimia 100 pia CCM na Jumuiya zake wameendelea kuwa vinara wa Demokrasia na Utawala bora hali inayotoa fursa pana kwa wananchi wa Zanzibar kushiriki kwa uhuru katika shughuli za kimaendeleo. 

Aliweka wazi kuwa hatua hiyo ya kimaendeleo imefikiwa kutokana na kufanyika Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, mwaka 1964 yaliyowakomboa wananchi na kuasisi maendeleo endelevu kwa wote.  Kupitia taarifa hiyo alieleza kuwa faida ya Mapinduzi haiwanufaishi watu Wana-CCM tu bali hata wale wanaopinga Mapinduzi pia nao wananufaika bila ya kubaguliwa.

Ndugu Mussa alishangazwa na Kauli za baadhi ya wanasiasa wanaodai kuwa hakuna kilichofanyika ndani ya mwaka 55 ya Mapinduzi ilhali wao wamesomeshwa na kuajiriwa mpaka wamestaafu bado wanahudumiwa  na Serikali ya CCM pamoja na watoto wao bado wamesomeshwa na serikali hizo wanazozibeza.  Katika maelezo yake Ndugu Mussa alisema wanasiasa wa vyama vya upinzani Tanzania wameendelea kupagawa na kuchanganyikiwa kila kukicha kutokana na kasi ya CCM katika usimamizi na utekelezaji wa Sera za Chama hicho kwa vitendo. 

Alisema Vijana wa UVCCM wataendelea kuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha amani na utulivu kwa wananchi pamoja na kundi la vijana wa rika mbali mbali. Matembezi hayo yalifunguliwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi ambapo zaidi ya vijana 400 wameshiriki matembezi hayo kutoka Chokocho hadi Mkanyageni Wilaya ya Mkoani Pemba.
 NAIBU Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Mussa Haji Mussa akisoma taarifa ya Matembezi ya kuenzi miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika Pemba.
BAADHI ya Vijana wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Zanzibar wakisikiliza nasaha mbali mbali zinazotolewa na viongozi katika hafla ya Matembezi hayo.
VIJANA wa UVCCM Zanzibar waliobeba Picha za viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na jamhzauri ya muungano wa Tanzania ambao ni aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Mzee Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania hayati Mwl.Julius Kambarage Nyerere ,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein.
BAADHI ya viongozi na vijana wa UVCCM wakiwa katika matembezi ya kuenzi miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar wakitokea Mkanyageni kuelekea Kangani Pemba.
BAADHI ya vijana wa UVCCM wakishiriki ujenzi wa Tawi la CCM Kangani.
NAIBU Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar ndugu Mussa Haji Mussa(kushoto), Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Mhe.Hemed Suleiman(anayeonekana katikati), Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa ndugu Tabia Maulid Mwita wakijenga Tawi la CCM Kangani Jimbo la Mtambile Pemba.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad