HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 17 January 2019

TAASISI YA SLYNN YA NCHINI UINGEREZA YAAHIDI KUSHIRIKIANA NA MAHAKAMA YA TANZANIA


Na Mary Gwera, Mahakama
Taasisi ya Slynn ya nchini Uingereza imeahidi kushirikiana na Mahakama ya Tanzania katika masuala mbalimbali ikiwemo kutoa Mafunzo kwa Waheshimiwa Majaji ili kuboresha huduma ya utoaji haki nchini.
Akimzungumza na Jaji Mkuu wa Tanzania mapema Januari 15, Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo inayojishughulisha na masuala ya Haki, Bi. Alison Fenney alisema kuwa lengo la ziara yao ni pamoja na kutaka kubaini maeneo ya ushirikiano. 
“Lengo la kutembelea Mahakama ya Tanzania ni pamoja na kujua taratibu mbalimbali za uendeshaji mashauri, kubadilishana uzoefu katika utendaji kazi na vilevile kuona jinsi gani Taasisi inasaidia katika maeneo yatakayobainishwa,” alisema Bi. Fenney.
Katika msafara huo Bi. Fenney aliambatana na Majaji Wastaafu,  Lord Bonomy na Nic Madge pamoja na Balozi wa Uingereza nchini, Bi. Sarah Catherine Cooke ambao kwa  pamoja walifanya mazungumzo na Jaji Mkuu ofisini kwake Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na ugeni huo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma aliainisha baadhi ya changamoto ikiwa ni pamoja na baadhi ya wananchi kukosa huduma za Mahakama katika maeneo waliopo au kusafiri umbali mrefu kupata huduma hiyo kutokana na kukosa majengo.
“Tanzania ni nchi kubwa, hivyo kuna baadhi ya maeneo ambayo wananchi hawapati huduma ya Mahakama au hutakiwa kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hiyo,” alieleza Jaji Mkuu.
Aidha, Jaji Mkuu aliongeza kuwa, idadi ya Majaji ni ndogo ukilinganisha na wingi wa mashauri yaliyopo ambapo alisema kuwa kila Jaji anasikiliza wastani wa kesi 400 kwa mwaka kiwango ambacho ni kikubwa.
Kufuatia changamoto hizi, Jaji Mkuu alieleza kuwa Mahakama iliona ni vyema kuandaa Mpango Mkakati ambao unatumika kama dira katika kutatua changamoto mbalimbali. 
Aliongeza kuwa Mpango Mkakati huo umejielekeza katika maeneo/nguzo kuu tatu (3) ambazo ni Utawala bora, Uwajibikaji na Usimamizi wa Rasilimali,  Upatikanaji na utoaji haki kwa wakati na Kurejesha imani ya jamii na ushirikishwaji wa wadau.
Taasisi ya Slynn iliyopo nchini Uingereza ina takribani umri wa miaka 30 inajihusisha na masuala ya haki na sheria na inafanya kazi  kwa karibu na Majaji na Taasisi za haki duniani ili kuboresha mifumo ya utoaji haki na uongozi wenye kufuata misingi ya sheria.
Ujumbe huo ambao utafanya ziara ndani ya Mahakama kwa siku tatu umejielekeza kujua zaidi jinsi gani Mahakama ya Tanzania inafanya katika suala zima la Usuluhishi ‘Mediation’ na masuala mengineyo. 
  Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyeketi mbele) akizungumza na Ujumbe kutoka Taasisi ya Slynn iliyopo nchini Uingereza, katika mazunguzo hayo walikuwepo pia Viongozi Wakuu wa Mahakama;  Jaji Kiongozi, Msajili Mkuu pamoja Naibu Msajili Mwandamizi –Mahakama ya Rufaa.

Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania, Mhe. Sarah Catherine Cooke akizungumza jambo.

Jaji Mstaafu wa Mahakama  nchini Uingereza, Lord Bonomy (kushoto) akiongea jambo. Katikati ni Balozi wa Uingereza nchini, Bi. Sarah Catherine Cooke, kulia ni Jaji Mstaafu wa Mahakama-Uingereza, Jaji Nic Madge. 
 Jaji Mkuu wa Tanzania,  Prof. Ibrahim Juma (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Wageni na baadhi ya Maafisa wa Mahakama  waliomtembele,  katikati ni Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Dkt. Eliezer Feleshi, wa nne kushoto ni Balozi wa Uingereza nchini, Bi. Sarah Catherine Cooke, wa pili kushoto ni Jaji Mstaafu wa Mahakama nchini Uingereza, Jaji Lord Bonomy, wa nne kulia ni Jaji Mstaafu wa Mahakama nchini Uingereza,  Jaji Nic Madge wa tatu kulia ni Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Slynn, Bi. Alison Fenney, wa kwanza kushoto ni Msajili Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Katarina Revocati na wa kwanza kulia ni Naibu Msajili Mwandamizi, Mahakama ya Rufani (T), Elizabeth Mkwizu.
Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Katarina Revocati (wa nne kulia akiwaonesha Wageni kutoka Taasisi ya Slynn, Ukumbi wa Kituo cha Mafunzo cha Mahakama kilichopo katika eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam. Wageni hao walipata nafasi ya kutembelea kituo hicho na kujionea ‘Video Conference’ iliyofungwa katika kituo hicho, vilevile wageni hao walifanya mazungumzo na Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Dkt. Eliezer Feleshi.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad