HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, January 18, 2019

Shirika la posta lahamasisha ufundishwaji wa uandishi wa barua kwa wanafunzi ngazi zote

 Meneja Masoko Msaidizi wa Shirika la Posta mkoa wa Dar es Salaam, Evord Mwauzi amesema tatizo la uandishi wa barua kwa wanafunzi ikiwamo wa elimu ya juu bado ni tatizo kubwa. Meneja huyo,ameyasema hayo leo Januari 18.2019 wakati wa maadhimisho ya siku ya Umoja wa Posta Afrika yaliyofanyika katika ofisi za Posta zilizopo Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na walimu pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Ilala.
Amesema, katika utekelezaji wao wa majukumu, wamebaini kuwa uandishi wa barua hasa kwa wanafunzi wakiwamo wa vyuo vikuu bado ni tatizo kubwa hapa nchini. Akiwaelezea wanafunzi hao jinsi shirika hilo la posta linavyotoa huduma,Mwauzi ametoa wito kuwa  siku  zijazo baadhi ya huduma za Shirika la Posta ziingizwe katika mitaala ya elimu.

Amebainisha kuwa, Shirika la Posta limetenga siku ya Jumatano kwa ajili ya kutoa elimu hasa ya uandishi wa barua kwa wanafunzi na  huduma wanazozitoa na kuzitaka shule kuwatumia maombi  iwapo wanahitaji elimu hiyo. Ameongeza,  hali hiyo inatokana na kuwa namabadiliko ya teknolojia, kitu ambacho kimepelekea pia hata hali ya watu kumiliki masanduku ya posta kupungua, lakini utaratibu uliopo  mtu yoyote anayekuja nchini kuwekeza  lazima awe na sanduku la Posta.

Hata hivyo alibainisha kwa kwa sasa Shirika la Posta linatoa kila huduma kwa kutumia njia ya mtandao  ikiwamo huduma ya Post Code ambayo humfanya mtu, kufahamu nyumba ya mtu  anayoitafuta iko mahali gani ikiwa tu atakuwa akifahamu jina la mtaa na barabara husika.

Kwa upande wake, Afisa Masoko Mwandamizi wa shirika hilo, James Musyangi amesema maadhimisho hayo ya Siku ya Umoja wa Posta Afrika yalianzishwa Januari 17, mwaka 1980 yakiwa na lengo la kuhakikisha uelewa wa wafanyakazi wa Posta Afrika kuwa mmoja katika mambo mbalimbali katika kutekeleza majukumu yao na kutetea maslahi na hata katika nyanja ya elimu pia.

Aidha,Afisa Masoko huyo Mwandamizi aliwatembeza wanafunzi wa Shule ya Msingi Ilala katika vitengo mbalimbali vya shirika hilo ikiwamo maeneo ya kutuma barua za ndani na nje ya nchi na  ukaguzi wa mizigo inayotumwa kutoka ndani kwenda nje ya nchi na inayotoka nje ya nchi kuingia nchini kama ni halali na inastahili kulipiwa kodi ama la.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad