HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 4 January 2019

NAIBU WAZIRI MABULA AWATUMBUA WAKUU WA IDARA YA ARDHI KIGOMA

Na Munir Shemweta, WANMM Kigoma
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula amewavua nyadhifa zao Wakuu wa Idara za Ardhi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji na Halmashauri ya wilaya ya Kigoma pamoja na Afisa Ardhi Mteule kutokana na watendaji hao kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Waliovuliwa nyadhifa zao ni Mkuu wa Idara ya Ardhi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji Brown Nziku, Emanuel Magembe Mkuu wa Idara ya Ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma na Afisa Ardhi Mteule wa Manispaa ya Kigoma ambaye pia Afisa Mipango Miji Paul Misuzi.

Mabula alifanya maamuzi hayo jana tarehe 3 Januari 2019 alipofanya ziara ya kushtukiza katika manispaa na halmashauri ya Kigoma wakati akiwa mkoani humo kuhudhuria kikao cha utatuzi wa mgogoro wa matumizi ya ardhi katika hifadhi ya Moyowosi mkoani Kigoma.

Uamuzi wa kuwavua nyadhifa watendaji hao wa sekta ya ardhi unafuatia kushindwa kusimamia maagizo na maelekezo yaliyotolewa tangu mwaka 2017 kuhusu ukusanyaji kodi ya ardhi, uingizaji wamiliki wa viwanja na mashamba kwenye mfumo wa malipo kwa njia ya kielektronik, utoaji hati kwa wamiliki wa ardhi pamoja na utoaji hati za madai kwa wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi jambo lillosababisha manispaa na halmashauri husika kukosa mapato yanayotokana na kodi ya ardhi.

"Kigoma mmezidi kunitibua hakuna unafuu wowote na uamuzi huu wa kuwavua nyadhifa ni sehemu tu na uamuzi huu ni salamu kwa nchi nzima, popote nilipotoa maelekezo tukikuta hayajatekelezwa basi wakuu wa idara wataondolewa"alisema Mabula.

Katika maelezo yake kwa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mkuu wa idara ya Ardhi halmashauri ya wilaya ya Kigoma Emanuel Magembe alisema kuwa halmashauri yake katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2018 imekusanya shilingi milioni 9, 291, 400 kati ya shilingi milioni 75 ilizopanga kukusanya, jambo lilomuudhi Naibu waziri wa Ardhi na Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Kwa mujibu wa Mabula,  pamoja na barua iliyoandikwa na Kanishna wa Ardhi Msaidizi Kanda ya Magharibi Idrisa Kayera tarehe 25 April 2017 kwenda kwa watendaji hao na maelekezo aliyoyatoa yeye mwenye wakati wa ziara yake mkoani humo mwaka jana  lakini watendaji hao hawakuonesha umakini katika kutekeleza ama kuijibu barua waliyoandikiwa.

Kufuatia hali hiyo Mabula ameagiza maelekezo yote yaliyotolewa katika Manispaa na Halmashauri yajibiwe kwa maandishi ifikapo tarehe 15 Januari 2019 pamoja na kuhakikisha viwanja na mashamba yanaingizwa kwenye mfumo wa kielektronik huku maeneo yaliyopimwa yakipewa kipaumbele.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mathias Kabundugulu alisema katika kuhakikisha serikali inakusanya mapato kwenye sekta ya ardhi jukumu la kwanza kwa watendaji wa sekta ya ardhi  ni kuhakikisha mfumo uliopo unatumika ipasavyo pamoja na watendaji kupanua wigo wa kukusanya mapato.

Alisema halmashauri ndizo zenye jukumu la kupanga na kusimamia ukusanyaji mapato ya ardhi huku wakurugenzi wake wakipaswa kusimamia ukusanyaji mapato na amewataka watendaji wa sekta ya ardhi kuwa wabunifu.
 Waziri wa Ardhi Nyumba na maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akipata maelezo mara baada ya kuwasili ofisi za halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji alipofanya ziara ya kushtukiza katika manispaa hiyo jana ambapo aliwavua nyadhifa wakuu wa Idara ya Ardhi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji na Halmashauri ya wilaya ya Kigoma pamoja na Afisa Ardhi Mteule kutokana na kushindwa kusimamia majukumu yao ipasavyo, wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa manispaa ya Kigoma Mwailwa Pangani.
 Mkuu wa Idara ya Ardhi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji Brown Nziku (kulia) na Afisa Ardhi Mteule Paul Misuzi (wa pili kulia) ambao wamevuliwa nyadhifa zao, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula (hayupo pichani) alipofanya ziara ya kustukiza katika Manispaa ya Kigoma wakati akihudhuria kikao cha utatuzi wa mgogoro wa matumizi ya ardhi katika hifadhi ya Moyowosi Kigoma.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angeline Mabula akimsikiliza mkazi wa Kigoma Iddy Salum alipowasilisha malalamiko yake kuhusiana na fidia kwenye Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZ) alipofanya ziara ya kushtukiza katika Manispaa ya Kigoma jana wakati akihudhuria kikao cha utatuzi wa mgogoro wa matumizi ya ardhi katika hifadhi ya Moyowosi Kigoma, Katikati ni Kamishna Msaidizi Kanda ya Magharibi Idrisa Kayera (Picha zote na Hassan Mabuye Wizara ya Ardhi).

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad