HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 4 January 2019

BARABARA YA MBINGA-MBAMBA BEY KUKAMILIKA 2021

*Waziri Mkuu akagua ujenzi, aridhishwa na kasi ya mkandarasi
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekagua mradi wa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mbinga kwenda Mbamba bey yenye urefu wa kilomita 69 itakayogharimu sh. bilioni 129.3.

Amekagua barabara hiyo leo (Ijumaa, Januari 4, 2019) wakati akielekea wilayani Mbinga akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani Ruvuma.

Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo wa barabara inayojengwa na kampuni ya Chico ya nchini China, ambapo ameuagiza uongozi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kusimamia vizuri mradi huo.

“Kazi hii inafanywa kwa uhogari mkubwa, naipongeza kampuni ya Chico kwa hatua waliyoifikia na ninaamini kwamba barabara hii inayotarajiwa kukamilika Januari 2021 itakamilika mapema zaidi.”

Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutachochea ukuaji wa uchumi kwa wananchi na mkoa kwa ujumla kwani itarahisisha usafiri kwa watu pamoja na usafirishaji wa mizigo.

Amesema pia barabara hiyo itakuza sekta ya utalii na uvuvi katika mkoa wa Ruvuma kwa sababu itawezesha watalii na wafanyabiashara kufika kwa urahisi katika wilaya ya Nyasa ambako ni kuingo cha biashara kati ya nchi jirani na mikoa inayopitiwa na ziwa Nyasa.

Mkuu huyo wa mkoa ametumia fursa hiyo kuushukuru uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuwapelekea fedha za ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo ya hospitali, vituo vya afya, shule, nishati na maji.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimina na Mbunge wa Nyasa na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya wakati alipokagua ujenzi wa barabara ya Mbinga- Mbamba bay kwa kiwango cha lami yenye urefu wa Kilomita 66, Januari 4, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wafanyakazi wa Kampuni ya Ujenzi ya CHICCO kutoka China inayojenga barabara ya Mbinga – Mbamba bay  kwa kiwango cha lami, yenye urefu wa Kilomita 66 wakati alipokagua ujenzi wa barabara hiyo, Januari  4, 2019. Kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Ruvuma,  Christina Mndeme. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Ruvuma na wafanyakazi wa Kampuni ya Ujenzi ya CHICCO kutoka China inayojenga barabara ya Mbinga – Mbamba bay yenye urefu wa Kilomita 66 wakati alipokagua ujenzi wa barabara hiyo, Januari 4, 2019.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi  wakati alipokagua ujenzi wa barabara ya Mbinga – Mbamba bay kwa kiwango cha lami yenye urefu wa Kilomita 66 unaofanywa na Kampuni  kutoka China ya CHICCO, Januari 5, 2019.  
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Askofu wa Jimbo la Mbinga, John Ndimbo wakati alipowasili kwenye kijiji cha Nyoni wilayani Mbinga kuhutubia mkutano wa hadhara Januari 4, 2019. Kulia ni Sheikh wa wilaya ya Mbinga, Said Majid.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad