HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 31 January 2019

MAJAJI, MAHAKIMU NA MAKADHI ZANZIBAR WAPEWA MAFUNZO YA NAMNA YA KUSHUGHULIKIA MASUALA YA FEDHA HARAMU

Na Ramadhani Ali - Maelezo  
Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu amesema tatizo la Utakatishaji  Fedha haramu linahitaji mashirikiano ya pamoja katika kukabiliana nalo kwani linahatarisha Maendeleo ya Mataifa mengi duniani. Amesema tatizo hilo linapelekea taifa kupoteza heshma yake na kutoaminika mbele ya mashirika na jamii ya kimataifa na kuzorotesha maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Jaji Makungu alieleza hayo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo Majaji, Mahakimu na Makadhi wa Zanzibar namna ya kushughulikia masuala ya fedha haramu yanayofanyika Chuo cha Maendeleo ya Utalii Maruhubi. Amesema utakatishaji fedha haramu ni vitendo vya aibu na vinahatarisha mfumo mzima wa fedha katika nchi, sheria na usalama hatimae nchi kupoteza washirika wake wa maendeleo.

Alisema kwa kutambua ukubwa wa tatizo hilo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikifanya juhudi mbali mbali ikiwemo kutunga sheria ya kukabiliana na vitendo hivyo viovu. Aliwaeleza washiriki wa mafunzo hayo kuwa jitihada za pamoja zinazochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupambana na tatizo hilo zimeleta mafanikio makubwa.

Alisema vitendo vya uhalifu na dawa za kulevya, ambavyo ni miongoni mwa mambo yanayopelekea utakatishaji wa fedha haramu vimekua vikidhibitiwa na kupungua kwa kiasi kikubwa. Amekipongeza Kitengo cha kudhibiti fedha haramu Tanzania kwa juhudi kubwa wanazochukua kutoa elimu kwa wadau wa kada mbali mbali nchini ili kufahamu athari zinazotokana na vitendo hivyo na njia za kupambana navyo.

Akimkaribisha Jaji Mkuu kufungua mafunzo hayo, Kamishna wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu Tanzania Onesmo Makombe amesema vitendo vya utakatishaji wa fedha haramu vinadhoofisha ukuaji wa uchumi wa nchi. Aliishauri jamii ya Watanzania kuungana kupiga vita vitendo vya utakatishaji fedha haramu ili nchi iendelee kuaminika na kujenga imani mbele ya jamii ya kimataifa.

Alimuhakikishia Jaji Mkuu wa Zanzibar kwamba Kitengo cha kudhibiti Fedha Haramu Tanzania kitaendelea kutoa taaluma  ndani ya pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuhakikisha tatizo hilo linapungua na hatimae kuondoka moja kwa moja.
 Kamishna wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu Tanzania Onesmo Makombe akitoa maelezo kwa Majaji, Mahakimu na Makadhi wa Zanzibar wanaoshiriki mafunzo ya kuwajengea uwezo kuhusu masuala ya fedha haramu yanayofanyika Chuo cha Maendeleo ya Utalii Maruhubi.
 Baadhi ya Mjaji, Mahakimu na Makadhi wa Zanzibar wanaoshiriki mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo kuhusu kushughulikia masuala ya fedha haramu wakifuatilia ufunguzi wa mafunzo hayo yanayofanyika Chuo cha Maendeleo ya Utalii Maruhubi.
 Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu akifungua Mkutano wa siku mbili wa kuwajengea uwezo Majaji, Mahakimu na Makadhi wa Zanzibar juu ya kushughulikia masuala ya fedha haramu yanayofanyika Chuo cha Maendeleo ya Utalii Maruhubi.
Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Mkungu (kati kati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji, Mahakimu na Makadhi baada ya kufungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo kuhusu utakatishaji fedha haramu katika Chuo cha Utalii Maruhubi

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad