HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 3 January 2019

MAHAKAMA YA WATOTO KISUTU YAPOKEA MASHAURI 118 YA JINAI KWA MWAKA 2018

 Katibu Mkuu Wizara yaAfya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii) (kushoto) Dkt. John Jingu akisisitiza jambo wakati wa ziara yake ya kufuatilia utekelezaji wa kazi za Maendeleo na Ustawi wa Jamii na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Mkoa Dar es salaam (katikati) ni Afisa Ustawi wa Jamii Mwandamizi Bi. Rehema Kombe na kulia ni Afisa Ustawi wa Jamii wa mkoa wa Dar es Salaam Bi. Sufiani Mdolwa.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Given Sure (kulia) akitoa maelezo kuhusu utekelezaji wa kazi za Idara ya Maendeleo ya Jamii ya Mkoa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii) Dkt. John Jingu (hayupo pichani) na kulia ni Afisa Ustawi wa Jamii wa mkoa wa Dar es Salaam Bi. Sufiani Mdolwa. Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW

Kwa mwaka 2018 Mahakama ya watoto ya Kisutu ilipokea jumla ya mashauri 118 ya jinai na makosa 295 ya madai yalipokelewa na kufanyiwa kazi na matukio ya kesi za watoto yakiwa wengi wa watoto hao ni wale ambao wamekinzana na Sheria na pili ni wale ambao Sheria inawakuta na makosa. Hayo yamebainishwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu Bi. Agness Mchome wa jijini Dar es Salaam wakati akitoa maelezo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu Maendeleo ya Jamii) Dkt. John Jingu alipotembelea katika Mahakama ya Watoto Kisutu jijini Dar es Salaam.

Hakimu Agness Mchome amewataka wazazi kutimiza wajibu wao wa malezi kwa watoto ili kuwaepusha na mashitaka yanayozuilika kwani watoto wanaofikishwa mahakamani ni wale ambao wazazi au walezi wao hawakutimiza wajibu wao wa kutoa malezi stahiki.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. John Jingu ameridhishwa na utendaji kazi wa Mahakama ya Watoto ya Kisutu jijini Dar Es Salaam kwani imekuwa ikifanya kazi nzuri ya kusaidia kurekebisha maadili ya watoto nchini.

Dkt. Jingu amesisitiza wazazi kuzingatia malezi bora na kutoacha watoto kuangalia televisheni na mitandao ya kijamii wakati wote ambapo kwa kiasi kikubwa mitandao ya kijamii na video zisizo na maadili zinachangia kuharibu maadili ya watoto nchini.

Naye Afisa Ustawi Mwandamizi kutoka Mahakama ya Watoto ya Kisutu Bi. Asha Mbaruku ameiasa jamii kutosambaza picha za watoto waliofanyiwa vitendo vya ukatili ikiwa ni kwa mujibu wa Kifungu 158 cha Sheria ya Mtoto kinazuia utoaji wa taarifa na kusambaza picha za mtoto aliyeumizwa au kufa.

Wakati huo huo Katibu Mkuu Dkt. Jingu alitembelea Kituo cha Kutoa Huduma cha Mkono kwa Mkono ( One Stop Centre) kilichopo katika Hospitali ya Aman jijini Dare es Salaam na kuridhishwa na huduma inayotolewa kituoni hapo.

Dkt Jingu aliongeza kuwa vitendo vya ukatili vimekuwa vikishamiri sana nchini kwa kipindi cha hivi karibuni hivyo uwepo wa vituo vya kutoa Huduma ya Mkono kwa mkono (One Stop Centre) nchini utasaidia kuwapatia huduma waathirika wa vitendo vya ukatili.

Ameongeza kuwa ukatili unaofanyika kwenye familia ni unasikitisha hivyo kituo cha huduma ya mkono kwa mkono kitasaidia kutoa mchango katika kunusuru waathirika wa ukatili na amewasisitiza wazazi kutimiza wajibu wao wa malezi kwa watoto na na kuhamasisha jamii kuachana na tabia potofu ya mmomonyoko wa maadili.

“Nimeridhishwa na kazi inayofanywa na kituo katika kuwapokea na kuwafanyia uchunguzi watoto na wanawake waliofanyiwa ukatili wa kijinsia, kuwa kubaini kiini cha ukatili na kutoa huduma stahiki kwa wahanga” alisema Dkt. Jingu

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Suphian Mndolwa ameeleza kuwa kituo hicho ni miongoni mwa vituo vinavyotoa huduma bora katika utetezi wa ulinzi na usalama wa watoto na wanawake nchini.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad