HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 7 January 2019

LUGOLA: SERIKALI ITAWASHUGHULIKIA VIONGOZI WA DINI WALIOJIPENYEZA KUANZISHA MAKANISA NA MISIKITI KWA LENGO LA KUFANYA UCHOCHEZI, KUVURUGA AMANI NCHINI

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akizungumza na wananchi wa Mji wa Ngara, Mkoani Kagera (hawapo pichani), katika Mkutano wa hadhara uliofanyika mjini humo, leo. Katika mkutano huo, Lugola amesema baadhi ya viongozi wa dini nchini wamejipenyeza na kuanzisha makanisa na misikiti kwa lengo la kuanzisha vichaka vya kujificha ili tujue ni watu wa Mungu kumbe wanataka kufanya uchochezi na kuvuruga amani nchini.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akizungumza na Askari na Watumishi wa Wizara yake wa Wilaya ya Ngara, Mkoani Kagera (hawapo pichani), katika kikao hicho, Lugola aliwataka watumishi hao wafanye kazi kwa kujituma bila kuchukua rushwa. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Luten Kanali Michael Mtenjele. Kulia ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi.
Baadhi ya Askari na Watumishi wa Mjini Ngara, Mkoani Kagera wakimsikiliza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (hayupo pichani) wakati alipokua anajibu maswali ya watumishi hao kuhusu masuala mbalimbali ya Wizara yake, katika kikao kilichofanyika mjini humo, leo. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Na Felix Mwagara, MOHA-Ngara.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema baadhi ya viongozi wa dini nchini wamejipenyeza na kuanzisha makanisa na misikiti kwa lengo la kuanzisha vichaka vya kujificha ili tujue ni watu wa Mungu kumbe wanataka kufanya uchochezi na kuvuruga amani nchini. 
Lugola amesema Serikali ya Rais Dkt. John Magufuli haitawavumilia wale wote walioanzisha taasisi hizo kwa lengo lao binafsi na itahakikisha inawashughulikia ipasavyo bila kuwaonea huruma.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na mamia ya wananchi wa Mji wa Ngara, leo, Lugola amesema makanisa na misikiti ambayo imesajiliwa na Wizara yake hatakubali kuona viongozi hao ambao wanajifanya kuwa na watu wa Mungu kumbe wanamalengo hayo binafsi.
“Makanisa na miskiti itakayobainika ina malengo hayo, sitaona haya kuifutia usajili, na pia nawataka viongozi wa dini endapo migogoro inaibuka hakikisheni  mnaitatua wenyewe kwa amani,” alisema Lugola.
Lugola ameongeza kuwa, Serikali inaheshimu imani ya dini na pia viongozi wao wanamchango mkubwa katika maendeleo ya nchi kutokakana na maombi pamoja na kuwaongoza waumini wao vizuri, lakini pia wapo baadhi ya viongozi hao wa dini, wanaingiza masuala ya siasa makanisani na misikitini.
“Niwaombe na niwatake viongozi wote wa dini, wakati tunapoenda katika uchaguzi, viongozi wa makanisa na misikiti iliyosajiliwa, niwaombe pale migogoro inapoibuka hakikisheni mnaitatua wenyewe kwa amani na msiruhusu mtu ambaye ana nia mbaya na maendeleo ya nchi hii, aje kuwaingilia,” alisema Lugola. 
Aidha, Waziri Lugola katika mkutano huo aliitaka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) apitie upya usajili na utoaji wa vitambulisho vya taifa katika mikoa ya Kagera na Kigoma ili waweze kuwabaini  na kuwaondoa raia wa nchi jirani zinazoizunguka mikoa hiyo.
Pia Lugola, alimpa wiki mbili  Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini, awe amefika katika mikoa hiyo kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kufanya operesheni kubwa ya kuwaondoa Wahamiaji haramu katika Mikoa hiyo kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu.
Lugola aliongeza kuwa, licha ya kutangaza operesheni hiyo, lakini viongozi wa uhamiaji katika mikoa hiyo wawe makini mara kwa mara kuhakikisha wanawafuatilia wahamiaji hao kwa kuwashirikisha wananchi waaminifu ili waweze kutoa taarfia sahihi za wahamiaji hao.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad