HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 4 January 2019

KESI YA VIGOGO SIMBA KUENDELEA KUUNGURUMA JANUARI, 15

Na Leandra Gabriel, Blogu ya Jamii

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wa Simba hadi January 15, 2019 kutokana na hakimu anayesikiliza kesi hiyo kutokuwepo.

Vigogo  wanaokabiliwa na kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni pamoja na Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva (ambaye hakufika Mahakamani),  Makamu  wake,  Geofrey Nyange maarufu kama 'Kaburu' na Mwenyekiti wa  Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba Zacharia Hans Poppe.

Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Leonard Swai amemueleza Hakimu Mkazi, Janeth Mtega kuwa shauri hilo liliititwa kwa ajili ya kusikilizwa na Hakimu anayesikiliza kesi hiyo Thomas Simba hayupo.

Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Mtega ameahirisha kesi hiyo hadi January 15,2019.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 10 yakiwemo ya kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi,  kutoa maelezo ya uongo na utakatishaji fedha haramu.

Katika shitaka la utakatishaji fedha linalomkabili Aveva, anadaiwa Machi 15, 2016 katika benki ya Baclays Mikocheni, jijini Dar es Salaam alijipatia Dola za Kimarekani 187,817, takriban Sh. Milioni 400 kutoka katika Timu ya Simba wakati akijua zimetokana na zao la kosa la kughushi.

Katika shitaka la kughushi linawakabili washtakiwa wote, ambapo wanadaiwa katika tarehe hizo hizo kwa pamoja walighushi hati ya malipo ya kibiashara ya Mei 28, 2016 wakionyesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zinathamani ya dola 40,577 sawa na zaidi ya Sh. Milioni 90 huku wakijua kwamba sio kweli.

Pia katika shtaka jingine inadaiwa Aveva, Nyange na Hans Poppe kati ya March10 na September 30, 2016 waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad