HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 7 January 2019

BENKI YA NMB YATUNUKIWA TUZO YA KUWA MSHIRIKA BORA KATIKA MASUALA YA KIFEDHA AFRIKA KWA MWAKA 2018

NMB Bank PLC imeshinda tuzo na kutajwa kuwa Mshirika Bora katika Masuala ya Kifedha Afrika kwa benki zinazofanya kazi na Shirika la Kimataifa la Fedha (IFC) la Benki ya Dunia. Hafla ya kukabidhiwa Tuzo hiyo ilifanyika Jijini Dar es Salaam. 

Akipokea tuzo hiyo kutoka kwa Mwakilishi Mkazi wa IFC Afrika Mashariki (IFC Resident for East Africa) Bw. Dan Kasirye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB Bi. Ruth Zaipuna alisema "Tumefurahishwa kwa namna ya pekee kupokea tuzo hii ya Kimataifa kutokana na mafanikio yetu; ni ushuhuda wa uwekezaji wetu katika teknolojia huku tukipanua mtandao wa matawi yetu na kuimarisha uwezo wetu wa kutoa huduma nzuri na za kisasa kwa wateja wetu." 

Aidha, Bi. Zaipuna aliongeza kuwa “katika miaka minne iliyopita, tumetoa huduma na bidhaa za kisasa na kuendelea kukidhi mahitaji ya wateja wetu nchini kote na kuziba pengo lililoachwa na benki nyingine katika soko. Kwa sasa tuna mtandao mpana zaidi nchini wenye matawi 228, ATM zaidi ya 800 na NMB Wakala zaidi ya 6,000 na hivyo kufanya upatikanaji wa huduma zetu nchini kuwa kwa asilimia 100%”. 

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa IFC kwa Afrika Mashariki Bw. Dan Kasirye alisema “NMB Bank imeshinda tuzo hii kutokana na uwezo wake wa kutoa huduma mseto za kifedha zinazomfikia mtumiaji wa chini kabisa. NMB Bank ni mshindi wa ushirikishwaji wa kifedha barani Afrika iking’ara zaidi kuliko benki nyingine zote ambazo zimeshafanya kazi na IFC. NMB imeonyesha uwezo wake katika kuwashirikisha wanawake, biashara ndogo, kubwa na za kati, pamoja na biashara ya kilimo Tanzania.” 

TUZO NYINGINE AMBAZO BENKI YA NMB IMESHINDA 
Katika kipindi cha miezi 12, Benki ya NMB imeshinda tuzo nyingine mbili za kimataifa ambazo ni; Benki Bora Tanzania kutoka Euromoney Awards for Excellence; Benki Bora ya Wateja Wadogo na Benki Bora ya Biashara Tanzania kutoka Banker East Africa Magazine. Pia benki ya NMB imeshinda tuzo mbalimbali za ndani kama vile; tuzo ya Afya na Usalama Kazini (OSHA) 2018 na tuzo ya utoaji wa taarifa bora za kifedha 2018 kutoka Bodi ya wahasibu na wakaguzi wa mahesabu (NBAA). 


Kaimu Mkurugenzi wa NMB Bank – Ruth Zaipuna akiwa na tuzo kutoka Shirika la Kimataifa la Fedha ambalo ni tawi la Benki ya Dunia ((IFC) iliyoitaja benki hiyo kuwa Mshirika Bora katika Masuala ya Kifedha kwa nchi za Afrika miongoni mwa benki zinazofanya kazi na shirika hilo.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad