HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 28 January 2019

Balozi Seif azindua mradi wa maji safi na Salama Shule ya msingi Mangapwani

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameonya kwamba Serikali haitosita kumuwajibisha na hata kumpelekea Mahakamani Mtendaji ye yote wa Halmashauri ya Wilaya atakayebainika kuhusika na ubabaishaji wa matumizi ya Fedha za Mfuko wa Jimbo zinazotengwa kwa ajili ya kuendeleza Miradi ya Wananchi.

Alisema zipo hitilafu zinazojitokeza kuzorotesha uendelezaji wa Miradi ya Wananchi Majimboni ambazo husababishwa na baadhi ya Watendaji wa Halmashauri za Wilaya zikionyesha kuzunguukwa na mazingira ya utapeli hasa katika matumizi ya Fedha.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo wakati alipozindua Rasmi Mradi wa Maji safi na salama katika Skuli ya Msingi Mangapwani ambao pia utasaidia kusambaza huduma hiyo katika vijiji jirani vinavyoizunguuka Skuli hiyo.

Alisema wapo baadhi ya Watendaji ndani ya Halmashauri za Wilaya wakionyesha udhaifu wa kuzorotesha Miradi ya Wananchi waliyoianzisha ilhali fedha zinazotengwa kuitekeleza Miradi hiyo huwa tayari zimeshaidhinishwa na kutiwa saini na Viongozi wanaouhusika.

Balozi Seif alisema kuanzia sasa atalazimika kufuatilia changamoto zote anazowasilishiwa zinazohusiana na kadhia hiyo na hatosita kumchukulia hatua za kinidhamu mtendaji atakayebainika kuhusika na hadaa yoyote hasa ile inayohusiana na masuala ya Fedha.

Aliwataka Wananchi wa Mangapwani kutoa taarifa mapema pale yanapojitokeza matatizo ya kiufundi katika uendeshaji wa Mradi huo wa Maji safi na salama na kuacha tabia ya kuwatumia Mafundi wa vichochoroni wanaoweza kuleta athari zaidi ya kiufundi kwenye mradi huo muhimu kwa ustawi wa Jamii.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza na kuwashukuru Wananchi wa Vijiji vya Mangapwani, Kiomba Mvua, Vuga Mkadini na Matetema kwa jitihada zao za kujisogezea huduma mbali mbali za Kijamii na Maendeleo kwenye maeneo yao.

Katika ziara hiyo Balozi Seif akiwa pia Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda alipata wasaa wa kukagua Mradi wa Kisima cha Maji safi kilichochimbwa kupitia Fedha za Mfuko wa Mbunge hapo Mangapwani, Jengo linalotarajiwa kuwa Skuli ya Msingi la Kiomba Mvua, Jengo la Skuli ya Msingi Vuga Mkadini pamoja na Mradi wa Umeme uliopo katika Kijiji cha Matetema.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizindua Rasmi Mradi wa Huduma ya Maji safi na salama uliopo Skuli ya Msingi Mangapwani utaosambaza pia katika Vijiji Jirani vinavyoizunguuka Skuli hiyo.
 Balozi Seif akitoa onyo kwa Mtendaji ye yote wa Halmashauri ya Wilaya atakayebainika kuzorotesha uendelezaji wa Miradi ya Wananchi ndani ya Majimbo.
 Balozi Seif  akikemea ucheleweshwaji wa Mradi wa Maji safi katika Kijiji cha Mangapwani uliofanywa na Mhandisi wa Mradi huo unaotekelezwa kupitia Fedha za Mfuko wa Mbunge wa Jimbo la Mahonda.
Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balaozi Seif akikagua maendeleo ya Ujenzi wa Jengo la Skuli ya Msingi ya Kiomba Mvua unafanywa na Wananchi wenyewe. Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad