HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 3 January 2019

BALOZI SEIF AZINDUA BARABARA YA WAWI-MABAONI-MGOGONI

  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiizindua Bara bara ya Kilomita Tatu ya Wawi – Mabaoni – Mgogoni ikiwa ni shamra shamra za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia Miaka 55.
 Muonekano wa Bara bara ya Wawi Mabaoni – Mgogoni iliyozinduliwa na Balozi Seif imeigharimu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zaidi ya Shilingi Bilioni 1.9.
 Balozi Seif akiikagua Bara bara Mpya ya Wawi hadi Mgogoni iliyojengwa na Kampuni ya Mecco akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Nd. Mustaha Aboud Jumbe.
 Balozi Seif akimpongeza Mwakilishi wa Kampuni ya Ujenzi ya Mecco Bwana Bujet kutokana na Wahandisi wake kukamilisha ujenzi wa Bara bara ya Wawi – Magogoni kabla ya wakati uliokubalika ndani ya Mkataba.
 Baadhi ya Wanafunzi wa Skuli za Sekondari na Msingi wakishuhudia hafla ya uzinduzi wa Bara bara iliyozunguuka Vijiji wanavyoishi ndani ya Wilaya ya Chake Chake Pemba.
 Baadhi ya Viongozi wa Serikali na kisiasa wakifuatilia matukio mbali mbali yaliyokuwa yakitendeka kwenye hafla ya uzinduzi wa Bara bara Wawi – Magogoni.
 Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Dr. Sira Ubwa Mwamboya akitoa maelezo kabla ya kumkaribisha Balozi Seif kuzungumza na Wananchi wa Wilaya ya Chake Chake kwenye Uzinmduzi wa Bara bara ya Wawi – Mgogoni.

 Balozi Seif akizungumza na Wananchi wa Wilayua ya Chake chake katika hafla ya uzinduzi wa Bara bara ya Wawi – Mabaoni – Mgogoni ndani ya shamra shamra za maadhimisho ya Sherehza kutimia Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mwakilishi wa Jimbo la Wawi Mheshimiwa Hamadi Ali Rashid { Gerei } akitoa shukrani kwa Serikali kwa niaba ya Wananchi wa Jimbo lake kutokana na Utekelezaji sahihi wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi YA Mwaka 2015 -2020 katika Sekta ya Mawasiliano. Picha na – OMPR – ZNZ.

     Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewakumbusha Wananchi wanaoishi pembezoni mwa Miundombinu ya Bara bara Nchini kuwa walinzi kwa kutoa Taarifa kwa vyombo husika dhidi ya wale wanaoharibu kwa makusudi miundombinu hiyo iliyojengwa kwa gharama kubwa.

Alisema wapo baadhi ya Watu waliojitoa mshipa wa fahamu kwa kuiba alama zilizowekwa Bara barani, kuchimba Mchanga au udongo pembezoni mwake jambo ambalo kama Wananchi hawatakuwa tayari kutoa ushirikiano wao kwa vyombo vya Dola  ile azma ya Serikali ya kuimarisha Sekta ya Mawasiliano inaweza kufifia.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kumbusho hilo wakati wa hafla ya kuizindua rasmi Bara bara ya Kilomita Tatu iliyojengwa kwa Kiwango cha Laki kuanzia Wawi -Mabaoni  hadi Mgogoni Chake Chake Pemba ikiwa ni mwanzoni mwa Shamra shamra za Maadhimisho ya kusherehekea Miaka 55 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Alisema uzoefu unaonyesha wazi kwamba mahala popote palipojengwa Miundombinu ya Bara bara katika kipindi kifupi hutoa fursa kwa Wananchi wake kunawirika Kiuchumi kutokana na harakati za Kibiashara zinazoambatana na ujenzi wa Makaazi bora yanayolingana na uwepo wa Bara bara husika.

Balozi Seif  alieleza kwamba shabaha ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964 yalilenga kumjengea mazingira bora ya Uhuru pamoja na kumuondolea umaskini Mwananchi wake baada ya kubaini kwamba Utawala wa Kikoloni haukuwa na dhamira njema ya kujenga uchumi na ustawi wa maisha ya Mwafrika.

Balozi Seif aliwaeleza Wananchi wa Chake Chake na Vitongoji vyake kwamba ndoto na dhamira ya kuleta Maendeleo ndani ya visiwa vya Zanzibar ilitaka kukatishwa na wapinga maendeleo kufuatia kitendo chao cha  kumuuwa Jemedari wa Mapinduzi ya Zanzibar Mzee Abeid Amani Karume, lakini umadhubuti wa Baraza la Mapinduzi unaendelea kulinda fikra, busara na maazimio yake yatakayodumishwa Milele.

“ Mzee Karume ameuawa na kuzikwa, lakini kilichokufa na kuzikwa ni kiwiliwili chake tu, Chama na Baraza la Mapinduzi vipo pale pale, mawazo, fikra, busara na maazimio yake yapo na yataendelea kudumishwa Milele”. Balozi Seif  alikariri maneno hayo muhimu ya Baraza la Mapinduzi.

Alisema ahadi na Sera za Chama cha Afro Shirazy Party bado zinaendelea kutekelezwa na Serikali za Awamu zote Saba tokea Mwaka 1964 hadi hivi sasa kipindi cha Utawala wa Awamu ya Saba inayoongozwa na Dr. Ali Mohamed Shein.

Balozi Seif alisema mbali ya maendeleo mbali mbali katika Sekta tofauti ikiwemo Kilimo, Afya na Elimu lakini miundombinu ya Bara bara kupitia Wizara inayosimamia Ujenzi imefanikiwa kujenga Bara bara za kiwango cha Lami zenye urefu wa Kilomita 1,261 Unguja na Pemba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaasa Madeveva watakaoitumia Bara bara hiyo ya Wawi Mabaoni hadi Mgogoni kuzingatia taratibu wa Usafiri ikiwemo kuendesha vyombo vyao wakijali watumiaji wengine wanaoitumia kwa Miguu na vyombo vidogo.

Aliishukuru na kuipongeza Kampuni ya Ujenzi wa Mecco kwa jitihada iliyochukuwa ya Wahandisi wake kukamilisha uwekaji wa Lami kabla ya muda waliopangiwa katika Mkataba wa Ujenzi wa Bara bara hiyo yenye uwezo wa kudumu zaidi ya Miaka 30 iwapo itatumiwa kwa uangalifu.

Akitoa Maelezo ya Kitaalamu ya Ujenzi wa Bara bara ya Wawi, Mabaoni hadi Mgogoni,  Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Nd. Mustafa Aboud Jumbe alisema Wizara hiyo tayari imeshatekeleza Ilani ya Chama Tawala cha CCM kwa ujenzi wa Bara Bara mbali mbali hapa Nchini.

Nd. Mustafa alisema zaidi ya Kilomita 1,261 zimeshajengwa kwa Kiwango cha Lami tokea Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 ambapo Kilomita 723 zimejengwa Katika Kisiwa cha Unguja na Kilomita 538 zimejengwa katika Kisiwa cha Pemba.

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar alifahamisha kwamba kazi iliyombele kwa Wizara ya Ujenzi katika ujenzi wa Miundombinu mbali mbali ni muendelezo wa ujenzi wa Bara bara Muyuni – Kombeni, Mwanakwerekwe – Fuoni, Jendele – Cheju na Mahonda – Mkokotoni kwa Unguja.

Alisema kwa upande wa Kisiwa cha Pemba Bara bara zilizomo kwenye mpango huo kwa sasa ni pamoja na zile za Mgagadu, Kiwani, Mkanyageni Kangani pamoja na Ole zikiwa na dhamira ya kuja kusaidia Maendeleo ya Wananchi.

Nd. Mustafa alisisitiza kwamba katika kuimarisha mpango huo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji imeshaagiza vifaa vya kisasa vitakavyotumika katika miradi hiyo vinavyotarajiwa kuwasili Nchini Mwishoni mwa Mwezi huu.

Mapema Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Dr. Sira Ubwa Mwamboya aliyewa Wizara hiyo itaendelea kuzingatia umuhimu na dhamira ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha Miundombinu kwa azma ya kuwarahisishia Mawasiliano Wananchi wa Visiwa vya Zanzibar.

Dr. Sira alisema hii inatokana na kuifanya Sekta ya mawasiliano  iweze kuwa rafiki kwa Mwananchi katika kujiletea Maendeleo ya haraka yanayobadilika kila mara kutokana na kukua kwa Teknolojia ya Mawasiliano Duniani.

Alizipongeza Taasisi mbali mbali Nchini pamoja na wasimamizi wake wanaoendelea kuiunga Mkono Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar katika utekelezaji wa malengo yake iliyopangiwa na Taifa.

Bara bara ya Wawi – Mabaoni hadi Mgogoni Chake Chake itakayoondoa tatizo la msongamano katika Bara bara Kuu ya Wete hadi Mkoani kwa kutumika kama Njia Mbadala kwa Gari zinazotoka Kaskazini kuelekea Uwanja wa Ndege imejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1,959,000,000/-.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad