HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 7 December 2018

WAZEE WAMPA USHAURI MZITO SHEIKH WA MKOA

NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
WAZEE wa dini ya Kiislamu jijini Mwanza wameushauri uongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kumtanguliza Mungu, ukubali kukosolewa na kuacha kuwapokea mafisadi baada ya kupenyezewa bahasha.

Walitoa rai hiyo ilitolewa jana walipokutana na kuzungumza na Kaimu Sheikh wa Mkoa, Alhaji Sheikh Hassan Musa Kabeke ili  kutoa ushauri wao kwa viongozi wa BAKWATA Mkoa wa Mwanza.
Wazee hao walisema ili uongozi wa baraza hilo uende vizuri ukubali kukosolewa na zaidi wamtangulize Mwenyezi Mungu katika kutenda na kuwatumikia waislamu na kuwa wakweli.

“ Aliyewazidi  wenzake ni mcha Mungu na hivyo timu hii izidishe ucha Mungu.Msiwapokee mafisadi kwa kupenyezewa bahasha baada ya kuwa wamefanya ufisadi misikitini.Bahasha hizo zinaidhoofisha BAKWATA na kuonekana ni jalala,” alisema Sheikh Rajab Charahani.

Alisema yapo malalamiko katika misikiti mingi yakiwatuhumuwa viongozi wa wilaya kupokea bahasha ili kufumbia macho mambo ya ovyo na kuutaka uongozi wa BAKWATA Mkoa ujiepushe na bahasha hizo na wakubali kukoselewa ikizingatiwa kila binadamu anakosea na hata yeye (Charahani) alikosea, wakifanya hivyo wazee watawapa ushauri.

Pia aliwashauri waislamu wenye uwezo watoe misaada yao ya kusaidia jambo zuri la ucha Mungu hata asiye mwislamu, hata kama linasimamiwa na BAKWATA. Hamis Hassan yeye alisema ubovu wa viongozi wa BAKWATA walipoacha misingi kulisababisha kulindana katika vyeo na kustahiana hata pale kiongozi anapofanya makosa na kushauri viongozi wa sasa kuepuka hayo.

Aidha, Jumanne Daud wa msikiti wa Nyakato alisema kushindwa kuheshimiana  kulilifanya baraza hilo lifike lilipo hivyo kuna kazi ya kufundisha kweli ili kurudisha imani baina ya waislamu wenyewe, pia viongozi wachaguliwe kwa sifa na uwezo bila hivyo ni kujenga uzio usiovunjika.

Kwa upande wake Mohamed Zuberi wa Msikiti wa Shamsia alisema; “Tunafanya kazi ya kutafuta pepo hivyo tuwasaidie viongozi wetu kuwashauri namna ya kutenda kazi ya Mungu.Mtu amuogope Mungu  asirejee yaliyopita.”  Naye Sheikh Shariff  Idrisa BAKWATA mpya itende na kuepuka ya zamani.Hakika wakiyatenda inayokusudia basi itakuwa nzuri lakini pia viongozi wasikae ofisini wapiti misikitini kubaini kero za waislamu.

Akizungumza baada ya wazee hao kutoa ushauri wao Sheikh Kabeke alisema yote waliyohusiwa ameyapokea na kuahidi kuwaheshimu kwa michango yao lakini baraza hilo katika kukusanya mali za waislamu halitamuonea mtu. Alieleza kuwa migogoro yote iliyopo kwenye misikiti mbalimbali wataishughulikia ili kwenda kwenye BAKWATA ya maendeleo na kuhoji watafikaje kwenye maendeleo ilhali hawaelewani wa kuzungumza?

“Wazee naomba mtusaidie kuisafisha BAKWATA na kurejesha imani kwa waislamu,kwenye uongozi wangu sitakubali kuona wazee wanadhalilishwa na watakaotuhubutu watatumbuliwa.Rai yangu wazee waingie kwenye vyombo vya maamuzi watusaidie kutafuta suluhu ya migogoro,”alisema sheikh Kabeke. Kaimu sheikh huyo wa mkoa alionyesha masikitiko yake kutokana na msikiti wa Nyegezi kuchomwa moto bila kuwepo kwa vita na kuhoji waislamu wanakuwa na raha gani mbele ya Mwenyezi Mungu.

Kuhusu utoaji wa zaka alisema wapo viongozi walitumia vibaya na kujinufaisha wao binafsi na kuwakatisha tamaa waislamu hivyo wamefungua akaunti itakayotumika kuweka fedha za zaka. “Tuwe wakweli nani alikuwa anaweza kupeleka zaka BAKWATA sababu wapo viongozi walitumia kuolea ama kufanya biashara.Sitaki kuzua migogoro Mwanza ila waliojimilikisha mali za waislamu waje mezani kwa mazungumzo,”alisema Sheikh Kabeke.
Sheikh Rajab Charahani mmoja wa wazee maarufu wa Dini ya Kiislamu jijini Mwanza akitoa nasaha kwa uongozi wa BAKWATA mkoani humu (hawapo pichani) baada ya kukutana kwenye kikao cha ushauri kilichofanyika jana katika Ukumbi wa Salum Ferej wilayani Nyamagana. Picha na Baltazar Mashaka
Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Alhaji Sheikh Hassan Musa Kabeke akizungumza na wazee maarufu wa dini ya Kiislamu jijini Mwanza (hawapo pichani) jana. Picha na Baltazar Mashaka

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad