HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 7 December 2018

SERIKALI YATOA MAFUNZO RASMI KWA MAFUNDI SIMU ZA MKONONI NCHINI

Naibu Katibu Mkuu wa Sekta ya Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi (wa kwanza kulia) akikabidhi cheti kwa Mwanahamis Abdul Salim aliyehitimu mafunzo ya kutengeneza simu za mkononi kwenye Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT). Anayeshuhudia wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara hiyo, Mulembwa Munaku
Naibu Katibu Mkuu wa Sekta ya Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi (aliyeketi katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na mafundi simu za mkononi wa kike watatu (waliosimama) kati ya 68 waliohitimu mafunzo DIT, Dar es Salaam. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa TEHAMA, Wizara hiyo Mulembwa Munaku na wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkuu wa Taasisi ya DIT, Prof. Patrick Nsimama 
Naibu Katibu Mkuu Sekta ya Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Dkt. Jim Yonazi (wa pili kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na meza kuu na wadau waliohudhuria hafla ya utoaji vyeti na leseni kwa mafundi simu za mkononi wa kwanza waliohitimu mafunzo yao, Taasisi ya DIT, Dar es Salaam. Wa tatu kulia ni Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara hiyo Mulembwa Munaku na wa pili kushoto ni Kaimu Mkuu wa Taasisi ya DIT, Prof. Patrick Nsimama
Naibu Katibu Mkuu wa Sekta ya Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Dkt. Jim Yonazi (aliyeketi katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na mafundi simu za mkononi waliohitimu mafunzo hayo kwenye Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam na baadhi ya wadau wa Sekta hiyo

Naibu Katibu Mkuu wa Sekta ya Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi ametoa vyeti vya mafunzo ya muda mfupi kwa mafundi simu za mkononi waliohitimu mafunzo hayo kwenye Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe
“Nawapongeza mafundi simu wa kike watatu kwa kuwa suala la ufundi linachukuliwa kuwa ni la wanaume, naamini ninyi watatu mtakuwa chachu kwa wanawake wengine kujiunga na mafunzo haya,” amesema Dkt. Yonazi wakati akitoa vyeti kwa mafundi simu za mkononi 68 waliohitimu mafunzo hayo ambapo kati yao watatu ni wanawake waliohudhuria mafunzo hayo ambayo yamefanyika kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi Julai mwaka huu. Ameongeza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa mafundi simu za mkononi kwa kuwa yatawawezesha kulinda usalama wa taarifa, yataleta tija na kuweza kuingiza fedha za kigeni kupitia Sekta ya Mawasiliano. 
Amefafanua kuwa mafunzo hayo yako sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambapo Serikali imejipanga kutekeleza Ilani hiyo kupitia kauli mbiu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ya ujenzi wa viwanda ambapo tayari Kampuni ya IPP Touchmate Tanzania Ltd itajenga kiwanda cha simu za mkononi nchini na wako tayari kuwapa ajira wahitimu hao kwa kuwa ni mafundi simu wa kwanza nchini kupata mafunzo hayo rasmi
“Naamini mtakuwa tayari kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini kufichua wahalifu wa makosa ya mtandao wanaotumia simu za mkononi ili kulinda usalama  wa nchi yetu,” amesisitiza Dkt. Yonazi. Pia, ameilekeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhakikisha kuwa mafundi simu za mkononi hao wanasajiliwa na kutambulika rasmi, kuweka majina yao kwenye tovuti ili wananchi waweze kuwatambua na kufahamu mahali walipo. Vile vile, ameitaka  TCRA kushirikiana na DIT kuendelea kufanya utafiti ili kuboresha mafunzo na utengenezaji wa vifaa vya kielektroniki
Naye Kaimu Mkuu wa Taasisi ya DIT Prof. Patrick Nsimama amesema kuwa DIT imetoa mafunzo hayo kwa mafundi simu za mkononi baada ya kufanya utafiti kwa kushirikiana na TCRA na yamezingatia na kulenga mahitaji ya jamii kuendana na utafiti uliofanyika. Pia, ameongeza kuwa mafunzo hayo wamepatiwa ya nadharia na kwa vitendo kwa kuwa DIT ina wataalam na wahadhiri waliobobea kutoa mafunzo ya aina mbali mbali kwa vitendo hivyo ameomba wananchi wawaamini mafundi hao 
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA John Walace Dafa amesema kuwa TCRA imehakikisha mafunzo hayo yametolewa kwa mujibu wa Sheria ya Kielektroniki ya Mawasiliano na Posta ya Mwaka 2010 na kanuni zake za mwaka 2018 ambapo mafundi simu hao waliohitimu watalazimika kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu husika na watahusika kuhakikisha kuwa hawapokei vifaa vilivyoibiwa na kuvifanyia matengenezo au kubadilisha matumizi ya vifaa hivyo
“Ulimwengu tunaoishi hivi sasa ni ulimwengu wa teknolojia, hatuwezi kuukwepa, kikubwa ni kuzingatia taratibu na sheria zilizowekwa ili tuepuke makosa ya mtandao,” amesema Naibu Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi anayeshughulikia uhalifu mtandaoni Mhandisi Shabani Hiki. Hiki amewaeleza mafundi simu hao kuwa huko wanakokwenda wakawe chachu na mabalozi wa wengine ili waepuke makosa na kuwa watumiaji wazuri wa simu za mkononi na huduma za mtandaoni ikiwa ni pamoja na kulisaidia Jeshi la Polisi kubaini wahalifu wa makosa ya mtandao. Amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi nchini haliko tayari kuona mtu yeyote anavunja Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 na tayari wameanzisha Kitengo cha Uhalifu wa Mtandao ili kudhibiti makosa hayo
Akisoma risala kwa niaba ya mafundi simu za mkononi wenzake waliohitimu mafunzo hayo, Clement Nkonyoka ameishukuru TCRA na DIT kwa kuwapa mafunzo hayo wakiwa wahitimu wa kwanza nchini ambapo yamewawezesha kufahamu sheria na kanuni husika, kupata uelewa wa utengenezaji simu kwa kutumia vifaa vya TEHAMA vya kisasa na yataiwezesha Serikali kuongeza mapato. Nkonyoka ameiomba Serikali iwatambue na kuwatangaza ikiwa ni pamoja na TCRA kuhakikisha kuwa hakuna fundi simu za mkononi atakayetengeneza simu za wateja bila kupata mafunzo hayo ili kuweza kuweka tofauti baina ya mafundi waliohitimu mafunzo hayo na wengine
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya IPP Touchmate Tanzania, Victor Tesha inayojenga kiwanda nchini ambacho kitaanza kutengeneza simu za mkononi mwakani amesema kuwa Kampuni yake itatoa ajira kwa mafundi simu za mkononi wa kwanza nchini wapatao 68 waliohitimu mafunzo hayo. “Mafundi simu msijione wanyonge, nyie mnafanya kazi kwa vitendo na mnatengeneza simu, nyie sio mafundi simu ila ni waanzisha simu, tutajiunga nanyi ili kuhakikisha ndoto zenu zinatimia na mnaotegemea kuajiriwa, muende kufanya kazi kwa bidii na kwa uaminifu mkubwa ili muendelee kuaminika,” amesema Tesha. Pia, ameongeza kuwa wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kubadilisha fikra na mitazamo ya watanzania na watumishi wa umma kwa kuwa viongozi na watumishi wa umma sasa wanafanya kazi kama sekta binafsi.   
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad