HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 19 December 2018

LUKUVI ALIA HALMASHAURI KUSHINDWA KUSIMAMIA MABARAZA YA ARDHI YA KATA

Na Munir Shemweta, WANMM
Waziri wa ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema halmashauri zina wajibu wa kuayasimamia mabaraza ya ardhi ya Kata katika maeneo mablimbali nchini.

Kauli ya Lukuvi inafuatia Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kumeleza kuwa ofisi yake hairidhishwi na namna  Mabaraza ya Ardhi ya Kata yanayofanya kazi  na kubainisha kuwa baadhi yake yanaendeshwa na watu wasiokuwa na taluma ya sheria huku wakitoa hukumu za kisheria ambazo  baadhi yake hazieleweki.

Akizungumza na wananchi wa wilaya ya Kinondoni  wakati wa  mkutano wa kusikiliza migogoro ya ardhi kupitia Program ya Funguka kwa Waziri uliofanyika  uwanja wa shule ya msingi Bunju B jijini Dar es Salaam jana, Waziri Lukuvi alisema halmashauri kupitia kwa mwanasheria wake zinapaswa kujua maamuzi yote yanayotolewa katika Mabaraza ya Ardhi ya  Kata.

Alisema, pamoja na kilio cha wananchi wengi dhidi ya Mabaraza ya Ardhi ya Kata katika maeneo mbalimbali lakini upo utaratibu mzuri uliopangwa kuhusiana na Mabaraza hayo ingawa  yameachwa yajiendeshe yenyewe huku Halmashauri chini ya Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ikiyaangalia bila kufuatiliwa.

Kwa mujibu wa Lukuvi, udhaifu wa Mabaraza ya Ardhi ya Kata na vijiji katika maeneo mengi unachangiwa na mabaraza hayo kutojengewa uwezo ambapo alibainisha kuwa mwanasheria wa halmashauri analo jukumu la kujua yote yanayoendelea katika mabaraza ikiwemo hukumu zinazotolewa.

‘’Uonevu wowote unaofanyika katika mabaraza ya ardhi ya kata basi mwanasheria wa halmashauri anapaswa kulaumiwa kwa kuwa ana uwezo wa kuwaita waliotoa maamuzi na kuwahoji dhidi ya uonevu uliofanyika sambamba na kuhakikisha maamuzi yanayofanyika katika mabaraza hayo yanazingatia haki.’’ alisema Lukuvi

Aidha, Waziri wa Ardhi Nyuumba na Maendeleo ya Makazi alielezea pia utaratibu wa kupiga mnada nyumba za watu walioshindwa kulipa madeni mara baada ya kukopa fedha na hati ya nyumba kuwekwa dhamana bila kufuata utaratibu lengo likiwa ni kutwaa nyumba za wahusika,

Lukuvi alizungumzia suala hilo kufuatia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kueleza uonevu wanaofanyiwa baadhi ya wananchi wake pale wanapokopa fedha kwa makubaliano hati ya nyumba kuwekwa dhamana ambapo alisema muda wa kurudisha fedha unapofika mhusika huzima simu kwa siku kadhaa na baadaye kwenda Baraza la Ardhi la Kata kudai kupewa  nyumba kwa maelezo kuwa mkopaji alishindwa kulipa.

‘’ Kuanzia sasa uhamishaji hati za nyumba kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine ni lazima Msajili na mimi tuelewe lengo likiwa kujiridhisha kama hakuna ujanja uliofanyika kwa lengo la kumdhulumu mkopaji’’ alisema Lukuvi.

Akigeukia suala la migogoro ya ardhi katika wilaya ya Kinondoni, Lukuvi alisema wilaya hiyo ndiyo kinara wa migogoro ya ardhi ukilinganisha na wilaya nyingine za mkoa wa Dar es Salaam.

Hata hivyo, alisema Serikali ya awamu ya tano imeshaanza kutafuta tiba ya migogoro hiyo na mingi ya migogoro iliyopo sasa ni ya miaka mingi na hakuna migogoro mipya na moja ya hatua ya kudhibiti migogoro ni kuziweka hati katika mfumo wa digitali kutoka analogia  na kazi hiyo ilishaanza katika wilaya za kinondoni na Ubungo na sasa inaendelea wialaya nyingine za jiji la Dar es Salaam.

Lukuvi alihitimisha ziara yake ya kinondoni kwa kusikiliza migogoro ya ardhi na kuitafutia ufumbuzi zaidi ya mia nne ambapo ilimlazimu kusikiliza migogoro hiyo hadi saa nne usiku ikiwa ni tofauti ya masaa mawili na muda aliotumia katika wilaya ya Ilala.
 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na wananchi wa wilaya ya Kiondoni mkoa wa Dar es Salaam waliojitokeza kuwasilisha migogoro yao ya ardhi  katika program maalum ya Funguka kwa waziri katika uwanja wa shule ya Msingi Bunju B.
 Mmoja wa wananchi wa Mabwepande akiwasilisha lalamiko lake la mgogoro wa ardhi kawa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi katika program maalum ya Funguka kwa waziri katika uwanja wa Shule ya Msingi Bunju B.

  Baadhi ya wananchi waliojitokeza kuwasilisha malalamiko yao ya migogoro ya ardhi kwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi katika program maalum ya Funguka kwa Waziri katika uwanja wa Shule ya Msingi Bunju B.
  Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Daniel Chongolo mara baada ya kumaliza kusikiliza migogoro ya ardhi katika wilaya ya Kinondoni eneo la Shule ya Msingi Bunju B jana usiku. Kulia ni Katibu Tawala mkoa wa Dar es Salaam Abuubaka Kunenge.
 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi (kushoto) akisalimiana na Meya wa Kinondoni Benjamin Sitta mara baada ya kuwasili kusikiliza migogoro ya ardhi katika wilaya ya Kinondoni eneo la Shule ya Msingi Bunju B jana usiku.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi (kushoto) akiwasili uwanja wa Shule ya Msingi Bunju B mara baada ya kuwasili kusikiliza migogoro ya ardhi katika wilaya ya Kinondoni eneo la Shule ya Msingi Bunju B jana usiku. (Munir Shemweta-WANMM)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad