HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, December 6, 2018

DKT. MABODI AFANYA ZIARA MANISPAA YA MJINI ZANZIBAR

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi, amesema CCM imendelea kusimamia kwa ufanisi sera za maendeleo kwa jamii bila kujali itikadi za kisiasa. Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na Watendaji wa Baraza la Manispaa Mjini, huko Sebleni katika mwendelezo wa ziara yakeb ya kukagua miradi mbali mbali iliyotekelezwa na manispaa chini ya mfumo wa Ugatuzi.

Dk.Mabodi ameeleza kwamba mipango endelevu inayotekezwa na Serikali za mitaa kwa lengo la kuimarisha huduma muhimu za kijamii katika nyanja za afya,elimu,uvuvi,ufugaji,kilimo na ujasiriamali ni kwa ajili ya wananchi wa rika zote bila ya kubaguliwa. Ameeleza kuwa Serikali Kuu imeamua kupeleka madaraka katika Serikali za Mitaa kwa lengo kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za kijamii kwa wananchi.

Ameeleza kwamba utekelezaji mzuri wa mipango iliyomo katika ugatuzi ndio litakuwa ni chimbuko la utengenezwaji wa Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/2025, iliyokuwa bora na inayoendana mahitaji halisi ya wananchi. Pamoja na hayo amewasihi Watendaji wote waliotolewa Serikali Kuu na kupelekwa Serikali za mitaa kuendelea kuwa wazalendo wenye kujituma kwa moyo mmoja katika kuhudumia jamii.

Kupitia ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu huyo, aliitaka Manispaa hiyo kuhakikisha miradi mbali mbali inayotelezwa inakuwa ndio vipaumbele halisi vya wananchi husika katika maeneo yao na inakuwa na viwango vinavyokubalika kisheria.

Dk.Mabodi ameitaka Manispaa hiyo kuhakikisha inatekeleza ujenzi wa vyoo vya kisasa maskulini pamoja na maeneo ya kijamii kwa lengo la kuondosha changamoto za ukosefu wa huduma hizo kwa baadhi ya maeneo ya Mji wa Zanzibar. Sambamba na hayo ameipongeza Manispaa hiyo kwa juhudi zao za kubuni mikakati mbali mbali ya uimarishaji wa huduma za kijamii hasa suala zima la ukusanyaji mapato na utekelezaji mzuri wa miradi ya ugatuzi.

Nae Mkurugenzi wa Manispaa ya Mjini Ndugu Said Juma Ahmada Akisoma taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Manispaa hiyo, amesema katika kipindi cha mwaka 2018/2019 walikadiria kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 8,754,432,507 na wamekusanya shilingi bilioni 5,058,976,742 sawa na asilimia 30. Amesema katika kuimarisha usafi wa mazingira wamekusanya jumla ya tani 159,399.8 na zimepelekwa katika jaa kuu la Kibele.

Mkurugenzi Said ameeleza kuwa katika kuimarisha huduma za Afya ya Mama na Mtoto wamefanya matengenezo kwa Vituo Vinne vya Afya. Kwa upande wa Sekta ya elimu amesema kuwa jumla ya wanafunzi 3,356 kwa mwaka 2018 wa skuli 18 za maandalizi wameendelea kupatiwa huduma ya lishe sawa na ongezeko la asilimia 124.

Said ameeleza wataendelea kubuni vyanzo mbali mbali vya ukusanyaji wa mapato ili kuhakikisha Manispaa hiyo inakuwa imara zaidi katika vyanzo vyake vya upatikanaji wa fedha kwa lengo la kutoa huduma bora kwa jamii. Akizungumza Mstahiki Meya wa Baraza hilo, Hatib Abdulrahman Hatib amesema pakiwepo na Serikali za Mitaa zenye maamuzi na nguvu ya kiutendaji na kiutawala, maendeleo ya Zanzibar yataendeleo kuimarika kwa kiwango kikubwa.

Naye Daktari dhamana wa Manispaa ya Mjini, Ramadhan Mikidad amesema dhana ya ugatuzi imekuwa ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya wananchi hasa katika upatikanaji wa huduma bora za afya, kwani wananchi wenyewe ndio wanaojipangia mahitaji yao tofauti na utaratibu uliokuwepo wakati wa miaka iliyopita.

Akizungumza Mwenyekiti wa Kikundi cha utengenezaji wa mbolea ya kisasa kupitia taka taka kilichopo Shauri Moyo Bi. Mwanajuma Ngwali Ahmed, amesema licha ya kukabiliwa na changamoto ya soko bado wameendelea kupata mafanikio mbali mbali yakiwemo fursa za ajira kwa vijana na wanawake kupitia miradi yao.

Katika ziara hiyo Dk.Mabodi ametembelea Kituo cha Afya cha Mama wajawazito na Watoto kilichopo Sebleni kwa Wazee, kikundi cha ujasiriamali kilimo cha mboga mboga shehia ya Nyerere, Shule ya msingi Kidongo chekundu, ujenzi wa soko la kuku Darajani pamoja na Kikundi cha utengenezaji wa Mbolea kupitia Taka kilichopo Shauri Moyo Unguja.
 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi  akielekea  katika ukaguzi wa ujenzi wa jengo la kisasa la machinjio ya kuku katika Soko la Darajani.
 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi akipokea maelezo juu ya maendeo yaliyofikiwa katika ujenzi wa jengo la soko la kuku darajani.
 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi akikagua shamba la mboga mboga la kikundi cha shehia ya Nyerere iliyopo katika Wadi ya Amani ambao wanajishughulisha na kilimo na wanasaidiwa na Manispaa ya Majini katika kazi zao.
 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi (kushoto) akipokea maelezo kutoka kwa Afisa  Muunguzi  Ashura Amour Mwinyi (kulia)  wa Kituo cha Mamama  Wajawazito na Watoto cha Sebleni akielezea huduma za Afya zinazotolewa bure katika kituo hicho zikiwemo za kipimo cha Ultra Sound.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi akipewa maelezo ya mashine maalum ya kusaga taka taka za kutengenezea mbolea ya mimea huko katika kikundi cha ujasiriamali kilichopo Shauri Moyo Zanzibar , katika ziara yake ya kukagua miradi inayotekelezwa na Manispaa ya Mjini chini ya ugatuzi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad