HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, December 1, 2018

BABA ADAIWA KUWAUA WATOTO WAKE WATATU AKIWEMO WA MIEZI 10


Na Mwamvua Mwinyi
JESHI la polisi mkoani Pwani ,limethibitisha kutokea kwa vifo vya watoto watatu akiwemo wa miezi kumi ,waliouawa kwa kunyweshwa sumu na baba yao mzazi. Chanzo cha kutenda kitendo hicho cha kikatili kinadaiwa ni kutokana na ugomvi mkubwa kati ya wazazi wa watoto hao. Kamanda wa polisi mkoani humo ,Wankyo Nyigesa alieleza tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana huko maeneo ya Kibindu ,Chalinze .

Aliwataja watoto hao kuwa ni pamoja na Shaila Salehe miaka sita ,Nurdin Salehe (4)na Sabrat Salehe mwenye miezi kumi waliouawa kwa kunyweshwa sumu ambayo ni dawa ya kuulia magugu iitwayo Twiga Amine na baba yao mzazi Salehe Masokola (22),mkazi wa kijiji cha Kunwe ,Mvomero mkoa wa Morogoro . Wankyo alibainisha,baba wa watoto hao alikuwa na mgogoro na mkewe ambae ndiye mama wa watoto .

"Mtuhumiwa alipowafuata watoto kutoka kwa mama mkwe wake kwa madai kwamba anakwenda kucheza nao na angewarudisha baadae " alifafanua Wankyo. Alielezea,mtuhumiwa aliwapakia marehemu kwenye baiskeli kutoka Kunke hadi kitongoji cha Ditele ,Kibindu ambapo aliwanywesha dawa hiyo kwa kuwachanganyia na juisi hivyo kupelekea vifo vya watoto hao. Kamanda huyo alisema ,katika eneo la tukio kumeokotwa chupa mbili za juisi zilizotumika ,chupa ya dawa na matapishi ambavyo vilichukuliwa kwa uchunguzi zaidi.

"Mara baada ya tukio mtuhumiwa alikunywa sumu kwa lengo la kutaka kujiua lakini aliokolewa na watu kisha kukimbizwa katika hospital ya mission Bwagala wilaya ya Mvomero kwa matibabu" Wankyo aliweka bayana. Mpaka sasa hali yake sio nzuri kwani yupo katika chumba cha wagonjwa mahututi akiwa chini ya uangalizi wa polisi .Katika hatua nyingine ,Wankyo alisema jeshi hilo limekamata viroba saba vya bangi vilivyokuwa vikisafirishwa kwenye gari yenye chesesi namba V75w - aina ya mitsubishi station wagon huko Mwatemo Kiwangwa ,Bagamoyo
Kamanda wa polisi wa mkoani Pwani,Wankyo Nyigesa akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani)kuhusiana na matukio mbalimbali yaliyotokea mkoani hapo .(picha na Mwamvua Mwinyi)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad