HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 9, 2018

WAZIRI MKUU AKUTANA NA BALOZI WA PALESTINA NCHINI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefanya mazungumzo na Balozi wa Palestina nchini Tanzania, Mheshimiwa Hamdi Abuali na kusema Serikali itahakikisha inaimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Palestina.

Akizungumza na Balozi huyo ofisini kwake Bungeni, jijini Dodoma leo (Ijumaa, Novemba 9, 2018), Waziri Mkuu amesema Serikali itaendeleza ushirikiano huo ulioasisiwa na hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa kiongozi wa Palestina,Yasser Arafat.

“Tanzania na Palestina zina historia ya kutosha. Tunatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati nchi zote mbili, ambayo yalikuwepo kuanzia Serikali ya awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimul Julius Nyerere.”

Waziri Mkuu amesema Tanzania na Palestina zimekuwa zikishirikiana kuboresha na kuimarisha sekta mbalimbali ikiwemo ya afya, ambapo madaktari bingwa kutoka Palestina wamekuwa wakija nchini na kuhudumia wananchi kwenye hospitali mbalimbali.

Amesema Serikali imedhamiria kuendeleza sekta ya viwanda nchini kama mkakati wa kukuza uchumi na kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025, hivyo ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wafanyabiashara kutoka nchini Palestina waje kuwekeza kwenye viwanda.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Tanzania ina vivutio vingi vya utalii ikiwa ni pamoja na uwepo wa mlima Kilimanjaro, mbunga zenye wanyama wa aina mbalimbali na fukwe nzuri za bahari, hivyo amewakaribisha watalii kutoka Palestina waje kuangalia vivutio hivyo.

Kwa upande wake, Balozi Abuali ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mzuri na wa muda mrefu uliopo baina yake na Serikali ya Palestina, ambapo amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba nchi yao itashirikiana kuboresha maendeleo.

Amesema Palestina ipo tayari kushirikiana na Tanzania kuhakikisha mkakati wa Serikali ya kukuza uchumi kutoka wa chini kwenda wa kati kupitia sekta ya viwanda unafanikiwa. Pia watashirikiana na Serikali kuboresha teknolojia katika maeneo yote ambayo wao wamepiga hatua, ikiwemo sekta ya kilimo.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Serikali ya Japan kuboresha maendeleo ya Taifa kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA).

Waziri Mkuu ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Japan nchini Mheshimiwa Shinichi Goto, ofisini kwake Bungeni jijini Dodoma, ambapoBalozi hiyo alikwenda kujitambulisha.

Amesema Watanzania wanafurahishwa na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Japan kutokana na utekelezwaji wa miradi mbalimbali ukiwemo wa daraja la juu katika eneo la Tazara (Mfugale flyover) pamoja na miradi ya maji, kilimo kupitia ufadhili wa JICA.

Pia Waziri Mkuu amemueleza Balozi Goto kuwa Serikali itahakikisha inampa ushirikiano katika kipindi chote cha uwakilishi wake nchini.

NayeBalozi Goto ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa mapokezi mazuri na amesema atahakikisha anaendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo iliyoanzishwa na mtangulizi wake ikiwemo ya miundombinu ya maji, elimu na kilimo.

 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana na Balozi wa Palestina nchini Hamdi Abuali, ofisini kwake Bungeni jijini Dodoma Novemba 9, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na Balozi wa Palestina nchini Hamdi Abuali, alipomtembelea ofisini kwake Bungeni jijini Dodoma Novemba 9, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad