HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 9, 2018

Watendaji Mamlaka za Maji Watakiwa Kuimarisha Huduma Wanazotoa kwa Wananchi


   Frank Mvungi- MAELEZO
Naibu Waziri wa  Maji Mhe. Jumaa Aweso amezitaka Mamlaka za Maji nchini kuhakikisha kuwa zinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha kuwa wananchi wote wanafikiwa na huduma ya majisafi na salama katika maeneo yote.
Akizungumza wakati akifunga Kikao kazi cha siku mbili kwa watendaji wakuu wa Mamlaka za Maji na wahandisi amesema kuwa  wanalo jukumu kubwa la kutekeleza majukumu yote kwa weledi na kuimarisha huduma za maji kwa wananchi.
“ Kwa yoyote atakayejaribu kuturudisha nyuma katika kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano hatutaweza kumvumilia kwa namna yoyote zaidi yakumuweka pembeni “; Alisisitiza Aweso
Akifafanua Aweso amesema kuwa watendaji hao wanatakiwa kuhakikisha kuwa sekta  ya maji inachochea maendeleo na ustawi wa wananchi.
Pia alizitaka Mamlaka za maji kutangaza miradi ya maji inayotekelezwa katika maeneo yao ili kuonesha juhudi zilizochukuliwa na Serikali katika kuimarisha huduma ya maji kwa wananchi kote nchini.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa sekta ya maji ina mchango mkubwa katika kutekeleza dhana ya ujenzi wa uchumi wa viwanda inayosisitizwa na Serikali  ya Awamu ya Tano.
Aliongeza kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa Mamlaka za maji kutekeleza miradi ya maji kwa kutumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini ili kuchochea  ukuaji wa uchumi wa viwanda  na kusaidia katika kukuza ajira.
Kikao Kazi cha Watendaji wakuu wa Mamlaka za maji na wahandisi wa mikoa kimefanyika Jijini Dodoma kwa siku mbili kikilenga kuimarisha huduma hiyo katika maeneo yote hapa nchini.
 Naibu Waziri wa Maji Mhe.  Jumaa   Aweso akisisitiza Watendaji wa Mamlaka za Maji kuwajibika  kuimarisha huduma zinazotolewa kwa wananchi ili kuendana na azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayosisitiza huduma Bora kwa wananchi wote.hiyo ilikuwa tarehe 8 Novemba, 2018 wakati  wa kufunga kikao kazi hicho Jijini Dodoma.
 Katibu Mkuu Wizara ya Maji Prof. Kitila Mkumbo akizungumzia hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha kuwa huduma ya maji inaimarishwa katika maeneo yote hapa nchini. hiyo ilikuwa tarehe 8 Novemba, 2018 wakati  wa kufunga kikao kazi hicho Jijini Dodoma.

Sehemu ya washiriki wa kikao kazi cha siku mbili kilichowashirikisha  Watendaji Wakuu wa Mamlaka za Maji, Wahandisi wa Maji wa mikoa yaliyofanyika kwa siku mbili Jijini Dodoma. (Picha zote na Frank Mvungi- MAELEZO)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad