HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 14, 2018

Vijana, wanawake na walemavu wala neema Manispaa ya Sumbawanga

Halmashauri ya manispaa ya Sumbawanga imetoa shilingi milioni 70.5 kwa vikundi 21 vya vijana, wanawake na walemavu ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya Mwaka 2004 yenye adhima ya kuwainua wananchi kiuchumi ili kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Manispaa ya Sumbawanga imedhamiria kutekeleza maelekezo ya serikali kwa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani na kuwezesha vikundi hivyo ambapo tangu mwaka wa fedha 2018/2019 uanze mwezi Julai hadi mwezi Novemba Halmashauri tayari imeshakusanya Shilingi bilioni 1.1 ambayo ni nusu ya makusanyo ya malengo waliyojiwekea kwa mwaka huu.

Fedha hizo zilitolewa katika hafla fupi ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo aliyekabidhi hundi kwa vikundi hivyo na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule, Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Mh. Justin Malisawa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na vikundi husika.

Akisoma taarifa ya kukabidhi fedha hizo kwa vikundi Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya alisisitiza kuwa Ili dhamira ya Serikali ya kufikia uchumi wa kati na Tanzania yenye Viwanda itimie shughuli utoaji wa mikopo lazima iwe endelevu na kuwa halmashauri imejiimarisha katika kukusanya mapato yake ya ndani ili kuleta matunda kwa kutoa mikopo.

“Vikundi hivi  vinajishughulisha na Usindikaji mafuta, chakula,vinywaji, Useremala, Utengenezaji wa Chaki na ushonaji, ufumaji na utengenezaji wa Mabatiki na Ufugaji wa kuku na ngombe wa maziwa. Pia Halmashauri inatarajia kutoka kiasi cha mkopo kilichobakia kwa mwezi Januari, 2019 kitakachokuwa kimekusanywa kutokana na makusanyo ya ndani.” Alisema.

Aliongeza kuwa ili kuona vikundi hivyo vinakuwa kiuchumi maafisa maendeleo ya jamii  ngazi ya kata na halmashauri kuhakikisha wanakuwa na orodha ya vikundi vilivyokopeshwa, kwaajili kufuatilia shughuli za vikundi na kuwajengea uwezo pamoja na kubaini mwendo wa urejeshaji wa mikopo kwa vikundi  na kufanya ufuatiliaji wa marejesho ya mikopo.

KWa upande wake Mh. Wangabo aliipongeza Manispaa ya Sumbawanga na kwaagiza wakurugenzi wote wa halmashauri zizlizopo Mkoa wa Rukwa kuhakikisha wanatekeleza agizo hilo ili kuweza kukuza kipato cha mwananchi wa Mkoa kwa kuwawezesha kiuchumi na hatimae kuongeza ajira pamoja na kukuza uchumi wa viwanda.

Pi aliwapongeza wale waliofanikiwa kupata mikopo hiyo na kuwasihi waweze kurudisha kwa wakati ili na wengine wapate fursa ya kukopeshwa na kujikwamua na kuwaonya kutotumia fedha hizo kwa matumizi ambayo yako tofauti na walichoombea.

“Serikali haitafurahishwa kuona fedha zilizokopwa zinatumika kwa malengo ambayo hayakukusudiwa kama vile anasa, aidha, nitoe wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote ndani ya Mkoa wetu kupitia hafla hii, kuweka mipango na mikakati ya kuhakikisha wananchi wanawezeshwa kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha na wadau mbalimbali wa maendeleo  ndani na nje ya Mkoa kwa kadiri itakavyowezekana.”Alisisitiza.

Kuanzia mwaka 2013/2014 hadi 2017/2018 fedha zilizopaswa kuchangiwa na Halmashauri yetu kama asilimia 10 ya mapato ya ndani ni shilingi 684,055,823. Hata hivyo hadi kufikia Juni 2018 jumla ya shilingi 50,000,000 zilitolewa kwa vikundi 43 sawa na asilimia 7.3 ya lengo. kiasi cha shilingi 634,055,823 hakikutolewa kutokana na mwenendo wa makusanyo.
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kulia) akisalimiana na mmoja wa wanakikundi cha Wanawake cha Tupendane kinachojishughulisha na utengenezaji wa mabatiki kilichopokea hundi ya Shilingi Milioni 3.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule (aliyeshika kipaza sauti) akitoa maelezo mafupi kwa kikundi cha sanaa za maigizo cha Great Mind Association (GMA) (wawakilishi wawili wamesimama kushoto) muda mfupi baada ya kikundi hicho kupokea hundi ya shilingi Milioni 3 ili kukuza shughuli zao za sanaa na miradi mingine ya kikundi. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad