HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, 27 November 2018

MHANDISI NYAMHANGA: HAKUNA SABABU ZA KUCHELEWESHA MRADI

Serikali imewataka Makandarasi wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Tabora-Koga-Mpanda yenye urefu wa KM 359 inayounganisha Mkoa wa Tabora na Katavi kupitia daraja la Koga, kufanya kazi kwa bidii ili kukamilisha mradi huo kabla ya muda uliopangwa.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph nyamhanga, wakati wa ziara yake katika mikoa hiyo ambapo amesema fedha za mradi huo zipo hivyo hakuna sababu ya kuuchelewesha. "Fedha za ujenzi wa mradi huu zipo hivyo fanyeni kazi usiku na mchana ili kukamilisha mapema barabara hii kwani hakuna vikwazo vyovyote na mvua isiwe sababu ya kusimamisha kazi za ujenzi", amesema Mhandisi Nyamhanga.

Mhandisi Nyamhanga, amewataka wasimamizi wa mradi wakishirikiana na Mameneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), wa mikoa hiyo kusimamia mradi huo kwa ukamilifu na kwa ubora uliopangwa bila kuongeza gharama. "Hakikisheni mradi huu unasimamiwa kwa ubora uliopangwa na mdhibiti gharama za mradi hata ikiwezekana ipatikane akiba ya fedha ambayo itatumika kwa miradi mingine ya barabara hapa nchini", amesisitiza Katibu Mkuu huyo.

Ameeleza umuhimu wa kukamilika kwa barabara hiyo kuwa utakuza uchumi wa wananchi na kuongezeka kwa shughuli za kibiashara kwakuwa ni miongoni mwa mikoa yenye uzalishaji mwingi wa bidhaa mbalimbali za kilimo, ufugaji wa nyuki, madini na utalii. Kuhusu uharibifu wa miundombinu ya barabara hapa nchini, Mhandisi Nyamhanga, ametoa wito kwa wananchi wa mikoa hiyo kuilinda miundombinu hiyo kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekamatwa.

Aidha, amewataka wananchi ambao wanaguswa na miradi inayoendelea kuhakikisha kwamba hakuna wizi wa vifaa vya ujenzi, nondo, uharibifu wa mitambo ya makandarasi, mafuta na saruji  kwani kunarudisha nyuma utekelezaji wa miradi hiyo na  kuongeza gharama. Kwa upande wake mkazi wa kijiji cha Nzaga, Bw. Karoli Kilanga, ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwani kutapunguza gharama za usafiri na kupunguza muda waliokuwa wakipoteza hasa vipindi vya mvua magari mengi yalikuwa yanakwama kutokana na ubovu wa barabara.

Mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Tabora-Koga-Mpanda unajengwa kwa sehemu tatu ambazo ni kutoka Usesula - Komanga, sehemu ya Komanga-Kasinde  na sehemu ya Kasinde-Mpanda ambapo utagharimu jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 481 na unatarajiwa kukamilika kabla ya mwaka 2021.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, akikagua kingo za daraja la kasisi katika barabara ya Tabora-Sikonge yenye urefu wa KM 30 iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Tabora.
 Mkandarasi wa kampuni ya  M/S Jiangxi Geo-Engineering, Li Jinaru, akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, wakati alipokagua mitambo ya kuchanganya lami katika kambi ya mkandarasi huyo anayejenga barabara ya Usesula-Komanga yenye urefu wa KM 108 kwa kiwango cha lami, Mkoani Tabora.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, akitoa maelekezo kwa Mhandisi Mshauri kutoka Kampuni ya LEA International Bw. Sanjeev Gupta (wa tatu kushoto) anayesimamia ujenzi wa barabara ya Usesula-Komanga yenye urefu wa KM 108, kwa kiwango cha lami, wakati akikagua hatua za ujenzi wa barabara hiyo, mkoani Tabora.
 Muonekano wa sehemu ya barabara ya Tabora-Sikonge yenye urefu wa KM 30, iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami.
 Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Katavi Mhandisi Martin Makabende, akitoa taarifa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga (katikati), kuhusu hatua zilizofikiwa katika ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Kasinde-Mpanda yenye urefu wa KM 105.389, Mkoani humo.
 Muonekano wa sehemu ya barabara ya Kasinde-Mpanda yenye urefu wa KM 105.389 inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Katavi.
Muonekano wa mtambo wa kuchanganyia lami katika mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya  Komanga-Kasinde yenye urefu wa KM 108, mkoani Katavi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad