HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 28, 2018

MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI KISUTU YAPOKEA MAJALADA NANE YA GUGAI YENYE MAJINA TOFAUTI

Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii
MAHAKAMA ya Hakimu mkazi Kisutu imeelezwa kuwa aliyekuwa mhasibu wa Takukuru Godfrey Gugai anayekabiliwa na mashtaka ya kumiliki Mali zisizolingana na kipato chake pamoja na wenzake watatu, anamiliki hati nane za umiliki wa ardhi zikiwa na majina mawili tofauti.

Hayo yameelezwa jana Novemba 27, 2018 na Afisa msajili msaidizi wa hati  wa Wizara ya Ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi Joanitha Kazinja ambaye ni shahidi wanne wa upande wa mashtaka wakati Akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

 Shahidi huyo ambaye kazi yake ni kusajili hati na miamala mingine  inayofanyika chini ya kifungu 334 cha Wizara ya ardhi amesema, miamala inayofanyika ni pamoja na rehani na kubadilisha hati ya umiliki wa ardhi pamoja na kutunza kumbukumbu na kutoa ushahidi mahakamani dhidi ya masuala ya ardhi.

Akiongozwa na wakili wa Serikali kutoka TAKUKURU Awam Mbangwa, shahidi Kazinja amesema Gugai ndiye mmiliki wa kwanza wa ardhi kutoka Oktoba, Mosi 2004 na hiyo ni pamoja na kiwanja namba 225 kitalu namba 6 kilichopo Jkt Mbweni Manispaa ya Kinondoni na alipata hati yake kwenye ofisi ya msajili 19 Mei, 2009.

Shahidi ameeleza kuwa amemtambua Gugai kuwa mmiliki wa ardhi hizo kutokana na Gugai kukiri na kuweka saini katika maelezo katika hati hiyo ya umiliki.

Majina ya umiliki katika hati hizo  yanaonesha kuwa takribani hati 6 zinaonesha umiliki wa Godfrey John Gugai na hati mbili za umiliki wa ardhi zikionesha jina la John Baptist Gugai.

Kufuatia maelezo hayo, Shahidi Kazinja aliomba mahakama kutoa  majalada 8 ya umiliki wa ardhi ya mshtakiwa  Gugai kama sehemu ya kielelezo katika kesi hiyo, ambapo mahakama ilipokea majalada hayo nane.

Akijibu maswali yalioulizwa na wakili Seni Malimi kuhusiana na majina tofauti yaliyopo kwenye hati ambayo ni Godfrey John Gugai na John Bapstist Gugai shahidi Joanitha Kazinja amesema kuwa hawafahamu tofauti iliyopo ila amesoma majina hayo kutokana na kumbukumbu zilizopo.

Hakimu Simba amehairisha kesi hiyo hadi kesho saa tano asubuhi.

Mbali na Gugai, washtakiwa wengine ni, George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera ambao wanakabiliwa na makosa 43, kati ya hayo 19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali, ambalo linamkabili Gugai.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka 43 yakiwemo 20 ya utakatishaji fedha haramu, kumiliki mali zisizoendana na kipato na kughushi mikataba ya mauziano ya viwanja katika maeneo mbalimbali.
Mhasibu wa Takukuru Godfrey Gugai anayekabiliwa na mashtaka ya kumiliki Mali zisizolingana na kipato chake pamoja na wenzake watatu, anamiliki hati nane za umiliki wa ardhi zikiwa na majina mawili tofauti kiwa anatoka mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad