HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 7, 2018

MAHAKAMA KUU TANGA YAJIPANGA KUSIKILIZA NA KUMALIZA MASHAURI KWA WAKATI

Na Amina Ahmad, Mahakama Kuu-Tanga
Mahakama Kuu Kanda ya Tanga imefanya kikao cha kusukuma mashauri (Case flow Management Meeting) na kujadili mikakati mbalimbali ikiwemo namna bora ya kuzuia mashauri kuwa mrundikano na kuondoa vikwazo visivyo vya lazima ili kurahisisha uendeshwaji wa mashauri.
Akiongoza Kikao hicho Novemba 05, Mwenyekiti wa kikao ambaye pia ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Tanga, Mhe. Amiri Mruma aliwataka Wadau kutoa ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha lengo lililopo mbele yao.
“Wito wangu kwa Wahe. Majaji na Mahakimu wa Kanda hii ni kufanya vikao vya awali na Wadau (Pre – session meeting) ili kuweza kujadili masuala mbalimbali hususani changamoto za Mashahidi ili kurahisisha uendeshwaji wa mashauri pindi vikao vya Mahakama (Session) vitakapokuwa vinaendelea,” alieleza Mhe. Mruma.
Akisoma taarifa katika kikao hicho, Katibu wa kikao ambaye pia ni Naibu Msajili Mahakama Kuu, Kanda ya Tanga, Mhe. Francis Kabwe alisema, tangu kuanza mwaka 2018 Mahakama Kuu Kanda hiyo imefanikiwa kufanya vikao vitatu (3) vya kesi za mauaji (criminal sessions) ambapo jumla ya mashauri 20 ya usikilizwaji wa awali (PH) yalipangwa kusikilizwa. 
Mhe. Kabwe alisema kati ya mashauri hayo, jumla ya mashauri 12 yaliisha na mashauri 8 yalitolewa maelekezo ya kupangwa katika vikao vijavyo ambapo kati ya mashauri 8, mashauri 6 pia yalimalizika. 
Kwa upande wa mashauri ya mrundikano, Mhe. Kabwe alisema, Mahakama Kuu Tanga ina mashauri 21 yenye umri kati ya miezi 13 – 24 yakiwemo mashauri ya Mahakama ya kazi. 
“Mashauri hayo 21yamewekewa mkakati madhubuti wa kuyaondoa ili kuzuia mrundikano (Back stopping) ambapo tayari kikao kimoja kimeshaanza kusikiliza mashauri hayo mbele ya Mhe. Jaji Mruma na kutarajiwa kumaliza Novemba, 15, 2018,” alisema Mhe. Kabwe.
Aidha; Mhe. Kabwe aliwaeleza wajumbe kuwa kikao kingine kitafanyika kuanzia Novemba 12 hadi Novemba 15, 2018 mbele ya Mhe. Jaji Edson Mkasimongwa. 
Wajumbe waliohudhuria ni kutoka Ofisi ya mwanasheria wa Serikali, Mawakili wa kujitegemea, Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), CMA na Taasisi ya kutoa msaada wa kisheria (TAWLA).
 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tanga, Mhe. Amiri Mruma (aliyesimama) akizungumza na Wadau waliohudhuria katika kikao cha kusukuma mashauri.
 Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Francis Kabwe akiwasilisha taarifa  katika kikao hicho. Katikati ni Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Amir Msumi, wa pili kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Tanga, Bw. Ahmed Ng’eni, wa kwanza kulia ni Kaimu Mwenyekiti chama cha Mawakili wa kujitegemea (TLS – TANGA CHAPTER), Bi. Linda Lugano na Kushoto niKaimu Mwanasheria wa Serikali Mfawidhi Mkoa wa Tanga, Mhe. Shose Naimani. 
Pichani ni baadhi ya Wadau waliohudhuria kwenye kikao.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad