HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, 13 October 2018

WAZIRI MKUU AFUNGA TAMASHA LA URITHI FESTIVAL

*Atoa miezi miwili Wizara ya Habari ikamilishe mchakato wa vazi la Taifa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa muda wa miezi miwili na nusu kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezoiwe imekamilisha mchakato wa Tanzania kuwa na vazi la Taifa.

Amesema Watanzania bado hawajaunganishwa kwa kuwa na vazi la Taifa, ambalo mchakato wake  umeendeshwa kwa miaka mingi na wizara hiyo bila ya kujulikana wamefikia wapi.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Oktoba 13, 2018) wakati akifunga tamasha za Urithi Festival, lililofanyika kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini  Arusha.

“Ifikapo Desemba 30,2018 tuwe tumeanza kupata sura ya vazi la Taifa ili wadau walijadili na waamue ni vazi gani la Mtanzania ambalo litawakilisha Taifa kama nchi nyingine walivyomudu kuwa na vazi la Taifa.”

Aliongeza kuwa ili kufikia azma  Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezoiandae tamasha maalumu kwa ajili ya kuonesha aina tofauti za nguo ili kupata vazi la Taifa.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwaagiza waandaaji wa tamasha la Uridhi Festival wahakikishe kuanzia  mwakani kuwe na uratibu wa pamoja baina ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara ili tamasha lifunguliwe upande mmoja na kufungwa upande mwingine wa Muungano.

Amesema kwa kufanya hivyo watakuwa wametoa  fursa kwa walio Zanzibar kujifunza na kuona utamaduni wa bara na wa bara kujifunza ya Zanzibar, hivyo itasaidia kudumisha  umoja wa kitaifa. “Hakikisheni ikiwa tamasha litafunguliwa Tanzania Bara basi lifungwe Zanzibar ili liweze kuwa na tija’’.

Katika hatua nyingine,Waziri Mkuu amesema Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, inaitaka Serikali kuongeza msukumo katika kukuza utalii na kutangaza vivutio vyetu vya utalii vikiwemo utamaduni na malikale.

“Mtakubaliana nami kwamba tunapaswa kuendeleza mila, tamaduni na desturi zetu kwani ndizo kichocheo muhimu cha uzalendo tulionao hususan katika suala zima la maadili. Vilevile, utamaduni ni zao la uhakika kwenye sekta ya utalii na ukarimu.”

Amesema thamani ya utamaduni mara nyingi imekuwa ikionekana kwenye sekta nyingine kama elimu, afya, michezo, kilimo, viwanda na maendeleo ya jamii, ambapo alitoa rai kwaWizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, wadau wote wa utalii hususani Sekta binafsi na wananchi kwa ujumla washirikiane katika kulinda, kutunza, kutangaza na kuendeleza vivutio vya utalii nchini.

“Lengo la Serikali ni kuongeza idadi ya watalii kutoka 1,102,026 mwaka 2015 hadi 2,000,000 ifikapo mwaka 2020. Lengo hili linatekelezwa kwa kuwezesha sekta binafsi kuwekeza kwenye huduma ya miundombinu ya utalii na kuendelea kutangaza utalii ili kuwafikia watalii wengi zaidi.” 

Amesema Urithi Festival ni chachu ya kukuza, kulinda, kuimarisha nakutangaza utamaduni na malikale zetu na kuvigeuza kuwa zao la utalii. Tamasha hili litatuweka pamoja zaidi na kudumisha umoja, utaifa na uzalendo kwa nchi yetu.

Aidha, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuikumbusha Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mkoa wa Dodoma kuanza maandalizi mara moja ya kutekeleza agizo la Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan la kutenga eneo mahususi ambalo litatumika kwa ajili ya Tamasha la Urithi kila mwaka kitaifa Mkoani Dodoma.

“Napenda kutumia fursa hii na hasa nikizingatia maagizo ya Makamu wa Rais kuwapa changamoto Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wa utalii kuhakikisha kuwa kuanzia mwaka kesho (2019) tamasha hili linatambulika Kimataifa na kuwa moja ya kichocheo kikuu cha kukuza pato la Taifa litokanalo na utalii“

Amesema wakati wa uzinduzi wa tamasha hilo Septemba 15, 2018 jijini Dodoma, Makamu wa Rais, Mama Samia aliagiza kila Mkoa kutenga bajeti kwa ajili ya Tamasha la Urithi. “Napenda kutumia fursa hii kuwakumbusha tena Wakuu wa Mikoa kuanza maandalizi mapema.“

“Tamasha la Urithi sio tu linaenzi utamaduni na mila zetu, lakini ndio njia bora zaidi ya kurithisha vizazi vijavyo mila, desturi, tamaduni na historia yetu. Kwani yeyote yule ambaye haenzi utamaduni wake basi huyo ni mtumwa.“

 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwahutubia wananchi waliyohudhuria wakati wa kufunga Tamasha la Urithi, lililofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Oktoba 13, 2018
 Naibu Waziri Maliasili na Utalii Josephat Hasunga, akizungumza na wananchi waliyohudhuria kwenye Tamasha la Urithi, lililofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Oktoba 13, 2018
 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harisson Mwakyembe, akipiga makofi, wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwahutubia wananchi kwenye Tamasha la Urithi, lililofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Oktoba 13, 2018, kulia ni Naibu Waziri Maliasili na Utalii Josephat Hasunga.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akitembelea banda la Maliasili na Utalii katika Tamasha la Urithi, lililofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Oktoba 13, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa na mkewe Marry, akiangalia bidhaa ya asili katika banda la wajasiriamali katika Tamasha la Urithi, lililofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Oktoba 13, 2018, kutoka kushoto ni Bibi Eliamulika Ayo, Naibu Waziri Maliasili na Utalii Josephat Hasunga.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akipokea zawadi ya ngoma na kikombe kutoka kwa Mwenyekiti wa Kikundi cha Wasanii Arusha Fred Thomas, wakati akikagua mabanda kwenye Tamasha la Urithi, lililofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Oktoba 13, 2018.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa na mkewe Marry, wakiangalia bidhaa ya bidhaa iliyobuniwa na mwanadada Glory Silayo (kushoto), katika Tamasha la Urithi, lililofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Oktoba 13, 2018
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipokea maandamano, katika Tamasha la Urithi, lililofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Oktoba 13, 2018
  Kikundi cha Sanaa cha Ngoma ya Waadzabe kikitoa burudani katika Tamasha la Urithi, lililofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Oktoba 13, 2018
 Mwanamuziki Faustina Charles (Nandi) akikitoa burudani katika Tamasha la Urithi, lililofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Oktoba 13, 2018.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipeana mkono na Msanii Ali Kiba, kwenye Tamasha la Urithi, lililofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Oktoba 13, 2018, (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad