HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 12 October 2018

WATU 300 DAR WAFANYIWA UCHUNGUZI WA MACHO

*Ni baada ya Hospitali ya macho ya Dk Agarwal kuamua kufanya uchunguzi bila malipo
Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
WATU zaidi ya 300 wamefanyiwa uchunguzi wa macho yao na matatizo mbalimbali yamegunduliwa ambayo husababisha uoni hafifu au upofu huku pia ukitolewa ushauri wa namna ya kutunza macho.

Hivyo kati ya hayo yaliyogundulika, yamejumuisha magonjwa ya mtoto wa jicho, mzio wa macho, matatizo ya kisukari yalioathiri macho, presha ya macho na mengine. Uchunguzi huo umefanywa na Hospitali ya macho ya Dk Agarwal ambayo imeamua kutoa huduma ya upasuaji kwa wagonjwa waliobainika kuwa na matatizo ya macho, hasa kwa wale wagonjwa wenye mtoto wa jicho bila tozo yoyote.
Uamuzi huo ni kama mchango wake katika jamii katika harakati za kupunguza na kuondoa mzigo wa upofu hapa nchini Tanzania na Duniani kwa ujumla. 


Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Daktari Bingwa na Mshauri wa magonjwa ya macho na upasuaji wa Retina katika hospitali hiyo Dk. Emeritus Chibuga. Amefafanua kuwa Hospitali ya macho ya Dakta Agarwal, kama mdau wa kutoa huduma ya macho hapa Tanzania, imetoa huduma za uchunguzi wa macho kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam katika Hospitali ya Mwananyamala

Amesema kuwa mbali ya kutoa huduma za tiba kwa wagonjwa wote wenye mahitaji makubwa na wasio na uwezo pia Hospitali ya Macho ya Dk Agarwal imetoa ushauri unaohusu afya ya macho kwa watu waliojitokeza kupimwa macho yao na kuwafahamisha 
dalili za hatari zinazoweza kuashiria shida za macho.

Ameongeza wameelezwa namna ya kujikinga na matatizo yanayoweza kuleta uoni hafifu au upofu na hatua za kuchukua iwapo kutakuwa na dharura ya tatizo la jicho, umuhimu wa kukaguliwa macho mara kwa mara hasa kwa wagonjwa wenye matatizo ya muda mrefu kama magonjwa ya shinikizo la damu na kisukari. "Hospitali ya Dk.Agarwal pia inapenda kuutarifu umma ya kuwa imekuwa ikishirikiana bega kwa bega katika kutoa huduma za afya ya macho na Serikali kupitia ofisi ya Mganga Mkuu wa wilaya ya Kinondoni na Meneja Mpango wa Taifa wa macho Tanzania wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

"Na inaahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika mpango wa kuhakikisha huduma bora za matibabu ya macho zinatolewa kwa wananchi wote wanaoishi Tanzania kwa kiwango cha hali ya juu kama kilivyoelekezwa na Serikali," amesema Dk. Chibuga. Pia amesema kuhakikisha hakuna tena mgonjwa atakayepelekwa nje ya nchi kwa matibabu ya shida za macho, kwani huduma hizo zimekwishaletwa hapa Tanzania katika hospitali mbalimbali za macho zilizopo hapa nchini, ikiwamo hospitali ya macho ya Dk.Agarwal.

"Ni vizuri umma ukifahamu ya kuwa, vipimo vinavyoweza kubaini matatizo mbalimbali ya macho kwa sasa vinapatikana hapa hapa nchini," amesema. Ametoa rai kwa wananchi wote kwenda kufanya uchunguzi wa macho yao mara kwa mara kwenye vituo vinavyotoa huduma za macho hapa nchini ili kubaini matatizo ya macho. 

"Kwa kufanya hivyo, itasaidia kutoa tiba sahihi na kwa wakati kwenye matatizo ya macho ambayo yapo bado kwenye ngazi ya awali ambayo inaweza kutibika, na hivyo kuepuka upofu ambao unaweza kuzuilika," amesisitiza Dk.Chibuga. Pia amewakaribisha wananchi wote kukaguliwa afya za macho yao angalau mara moja kwa mwaka na kwamba Hospitali yao inawakaribisha watu wote kwenye vipimo na matibabu stahiki kwa matatizo mbalimbali ya macho.

Kuhusu sababu za kufanya uchunguzi huo Dk.Chibuga amefafanua kuwa kila mwaka Dunia huadhimisha Siku ya Macho Duniani  ambayo huwa ni Alhamisi ya pili ya Oktoba. Hivyo katika siku hiyo  wadau wote wa macho duniani hujitolea kutoa huduma mbalimbali za uchunguzi na matibabu kwa watu wenye uhitaji wa tiba ya magonjwa ya macho au ushauri wa kuyatunza macho yao kuepuka na matatizo ya macho yanayoweza kuleta upofu unaoweza kuzuilika.

Kwa mwaka huu wa 2018, siku ya macho duniani imefikia kilele chake Oktoba 11. Na kauli mbiu kwa maadhimisho ya mwaka huu ni : Afya ya Macho kwa Wote: Huduma za Macho Popote Ulipo Imeelezwa kwa hapa Tanzania, maadhimisho yamefanyika Kitaifa mkoani Dodoma, lakini shughuli za siku hiyo ya macho duniani, zimeendelea sehemu zote nchini.

Hivyo kwa wadau wa kutoa huduma za macho kutoa huduma za uchunguzi wa macho kwa jamii zinazowazunguka bila kuwatoza gharama yoyote. Hivyo kwa Dar es Salaam taasisi zinazojihusisha na huduma ya macho,  zimetoa huduma mbali mbali za uchunguzi wa macho katika wilaya zote, na kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu. Ambapo wameanza kutoa huduma  toka Oktoba 9 mpaka Oktoba 11 Oktoba, ambayo ndio kilele cha maadhimisho ya siku ya macho Duniani. 
 Dk. Emeritus Chibuga na Dr. Huzeifa kutoka hospital ya macho ya Dkt. Agarwal wakizungumza na mmoja wa watu walioenda kupata huduma ya kupima macho katika hospital ya Mwananyamala jana katika kuadhimisha siku ya macho duniani.
 Daktari mtaalam wa masuala ya macho kutoka hospital ya Dr. Agarwal iliyopo jijini Dar es Salaam akimpatia maelekezo kijana aliyefika kupatiwa huduma ya kupima macho.
Daktari akimpima mmoja wa wagonjwa wa macho aliyefika katika hospital ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam. Hospital ya Dr. Agarwal imetoa huduma ya upimaji na ushauri bure kwa watu mbalimbali wanaosumbuliwa na matatizo ya macho.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad