HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 29 October 2018

Wasichana 600 kunufaika na kampeni ya kujiweka salama wakati wa hedhi ya taasisi ya Her Africa

Katika dhamira yake ya kuhakikisha Watoto wa kike wanapata elimu kuhusu umuhimu wa usafi katika kipindi vya hedhi, taasisi ya Her Africa imezindua kampeni ya kitaifa inayojulikana kama “Hedhi yangu, Furaha yangu” katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike ambayo huadhimishwa tarehe 11, Oktoba kila mwaka kama ilivyopangwa na Umoja wa Mataifa (UN).

Kupitia kampeni hii mifuko maalum itatolewa kwa wasichana ambao ndani yake kukiwa na mahitaji muhimu katika kipindi cha hedhi kama vile, paketi za pedi za kutumia mara moja na za kutumia zaidi ya mara moja, vitambaa laini vya kujisafishia, chupi na khanga mpya, sabuni ya kuogea pamoja na ya kufulia na dawa ya Dettol. Vifaa vinavyopatikana katika kifurushi hiki vimetolewa na wadau mbalimbali katika jamii kama msaada kutokana na jitihada kubwa zilizofanywa kupitia mitandao ya kijamii na taasisi ya Her Africa kufanya  uhamasishaji wa kulielezea tatizo na kutafuta kuungwa mkono kulipatia ufumbuzi.

Meneja Miradi wa Her Africa, Salha Kibwana amesema “Wanawake wengi na wasichana katika jamii zetu hupata changamoto kubwa katika kipindi cha mzunguko wao wa mwezi wa siku za hedhi, kutokana na kutoweza kumudu kununua pedi za kutumia, ukosefu wa elimu kuhusiana na hali hiyo, imani za mila ambazo zinawafanya wengi kuamini kuwa suala la hedhi halipaswi kuongelewa, ukosefu wa mazingira rafiki ya kujihifadhi mtu anapokuwa kwenye hali hiyo kama vile vyoo na maji safi ya kutumia. Changamoto hizo zote zinasababisha watumie vifaa vya kuwasitiri visivyofaa ambavyo vinaweza kuwasababishia kupata maradhi.”

Naye Zena Tenga, kutoka taasisi hiyo ya Her Africa, aliongeza kusema “Kampeni yetu hii imelenga kutoa elimu ya ufahamu kuhusiana na umuhimu wa usafi katika kipindi cha hedhi, kuwezesha kufahamu mzunguko wa siku za hedhi kwa mwezi kwa ajili ya kujiandaa, kujua dalili za kuingia kwenye siku za hedhi na mengineyo mengi.”

Kampeni hii imeungwa mkono kwa kiasi kikubwa na jamii, kampuni ya AIM Group Tanzania ilikuwa mstari wa mbele kuhakikisha inashiriki kukabili changamoto za hedhi kwa kutoa msaada wa pedi 144 na kugharamia mifuko maalum 14 yenye vifaa vya hedhi ambayo ilitolewa kama msaada kwenye kituo cha Watoto yatima cha Hiari.

“Tumejitoa kusaidia kukabili changamoto hii kwa kuwa wanawake wengi na wasichana katika jamii wanapata shida wakati wa kipindi cha mzunguko wa siku zao za hedhi kwa mwezi, kutokana na kutoweza kumudu gharama za vifaa vya kuwasitiri, ukosefu wa elimu hiyo na imani potofu kuwa suala la hedhi ni mwiko kuongelewa hadharani. Wakati umefika sasa wa kuunganisha nguvu na kuunga mkono watu binafsi na taasisi ambazo zimejitoa kupambana kuondoa changamoto hizo.”alisema Ritha Tarimo kutoka kampuni ya AIM Group.

AIM Group imetoa wito kwa watu binafsi na makampuni kusaidia kutoa pedi na vifaa vingine vya kufanikisha huduma za elimu ya uzazi ili kuhakikisha changamoto za hedhi kwa wasichana na wanawake zinapungua nchini. Wakati wa kukabidhi msaada katika kituo cha watoto yatima na katika Shule ya Msingi ya St. Joseph, Kituo cha masuala ya Jamii cha SISA, kilitoa elimu kwa wasichana kuhusiana na hedhi, uzazi, umuhimu wa kuzingatia usafi wakati wa hedhi na jinsi ya kujiweka vizuri katika kipindi hicho.

Mwasisi wa Kituo cha masuala ya Kijamii cha SISA, Saidy Kabanda alisema “Wasichana wanayo nafasi kubwa ya kutoa mchango wa ujenzi wa taifa, hivyo wanapaswa kujengewa mazingira ya kujiamini na kutobaguliwa, kwa kupatiwa elimu ya mabadiliko ya miili yao katika makuzi yao ikiwemo elimu ya kujistiri wanapokuwa kwenye kipindi cha hedhi. Wasichana wanapaswa kusaidiwa ili waone hali hiyo ni ya kawaida kutokana na maumbile yao na kujua jinsi ya kukabiliana nayo”.

Taasisi ya Her Africa imepokea msaada wa fedha kutoka kwa watu binafsi na makampuni ambao umewezesha kununua pedi 294 na pedi za kutumia zaidi ya mara moja 18. Her Africa imelenga kuhakikisha inawafikia wasichana 50 wenye changamoto ya kupata vifaa vya kuwastiri wakati wa kipindi cha hedhi kila mwezi, kupitia kampeni hii itakayofanyika kwa kipindi cha miezi 12, lengo likiwa ni kuwafikia wasichana 600 kwa mwaka.

Her Africa, itakuwa inatafuta msaada wa michango kwa ajili ya kufanikisha kutoa mifuko maalumu yenye vifaa vya hedhi kwa wasichana 600, sambamba na kuendesha semina kuhusiana na elimu ya umuhimu wa usafi wakati wa hedhi, jinsi ya kujihifadhi katika kipindi hicho, matumizi ya fedha, umuhimu wa kuwa na ujuzi mbalimbali, kuwapatia mwongozo wa fani za kusomea na maendeleo yao kibinafsi kwa ujumla.

Kampeni ya "Hedhi Yangu, Furaha Yangu" ya taasisi ya Her Africa itaendelea kufanyika kwa kuhamasisha wachangiaji wengi kujitoa kusaidia na kuandaa warsha za mashuleni na vituo vya wanawake katika mikoa mbalimbali nchini ili kufanikisha kupunguza tatizo la ‘changamoto za hedhi zinazotokana na umaskini’ na itashirikisha watu binafsi zaidi ili wawe sehemu ya kulipatia ufumbuzi tatizo hili.
 Moja ya mwanzilishi wa mradi wa " Her Africa" akizungumza na wanafunzi wa kike kutoka shule ya primary St Joseph kuhusu elimu hedhi kabla ya kutoka msaada wa mifuko maalum kwa wasichana hao yenye vitu muhimu vya kutumia wakatika wa kipindi cha hedhi.
Wanafunzi  kutoka shule ya msingi ya St Joseph wakionesha mifuko maalum waliyopokea kutoka kwa "Her Africa" yenye vitu muhimu vya kutumia wakatika wa kipindi cha hedhi. Her Africa imeanzisha kampeni ya "Hedhi yangu, Furaha Yangu" ambayo inatarajia kuwafikishia wasichana 600 mifuko hiyo maalum yenye vifaa vya hedhi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad