HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 23 October 2018

UKOSEFU WA UWAJIBIKAJI NA UWAZI CHANZO CHA MIGOGORO AZAKI

Ukosefu wa uwazi na uwajibikaji katika  shughuli za Asasi za Kiraia Tanzania  unaathiri uwezo wa nchi kutambua kiwango cha michango na misaada inayotolewa na wadau wa maendeleo na matokeo yake katika maendeleo ya  nchi.

Hayo yamesema jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. John Jingu wakati akizungumza na wajumbe wa Mkutano Mkuu Wa Asasi za KIrai Tanzania katika hotuba aliyoitoa kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kasimu Majaliwa wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Asasi za Kirai Tanzania.  

Dkt. Jingu aliongeza kuwa ukosefu wa uwazi na uwajibikaji wa baadhi ya AZAKI unatoa fursa ya rasilimali za umma ambazo hutolewa kwao kutumika vibaya na hivyo kuathiri kufikiwa kwa matokeo yanayotarajiwa.

Katibu Mkuu huyo aliendelea kusema kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha malalamiko na manung’uniko kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo wafadhili wao na walengwa wa miradi yao.

“Ukosefu wa uwazi umekuwa chanzo cha migogoro miongoni mwa wanachama wa AZAKI husika.  Pia, kukosekana kwa uwazi na uwajibikaji kumesababisha baadhi ya AZAKI kutumika vibaya kinyume na sheria za nchi na kinyume malengo ya kuanzishwa kwao’’. Aliongeza Dkt Jingu.

Pamoja na mapungufu hayo Dkt. Jingu amezisifu Asasi hizo za Kiraia kuwa zinatoa mchango mkubwa katika kupambana na rushwa na ubadhirifu wa mali za umma na kuleta uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa mali za umma.

Dkt. Jingu amesema serikali Itahakikisha masuala ya uwazi na uwajibikaji yanazingatiwa na Asasi za kirai imeweka utaratibu unaozitaka AZAKI kuweka wazi vyanzo vya rasilimali zinazoendesha miradi yao na kutaja utaratibu huo kuwa ni AZAKI kutangaza mikataba ya ufadhili unaozidi milioni ishirini katika vyombo vya habari ambavyo vinasikika au kusomwa na watu wengi zaidi kwa urahisi katika jamii.

Aidha Dkt. Jingu aliendelea kusema kuwa AZAKI pia zinatakiwa kuzingatia misingi ya uwazi na uwajibikaji wa kifedha ikiwa ni pamoja na kuepuka matumizi mabaya ya fedha za ufadhili zinazotolewa.

Aliongeza kuwa Asasi za Kiraia zihakikishe zinaweka utaratibu wa AZAKI kuwajibika kwa wananchi inaowahudumia kupitia mifumo ya Serikali za Mitaa iliyopo akiongeza kuwa  takwa hili litaiwezesha jamii husika kufahamu miradi inayotekelezwa na AZAKI katika maeneo yao.

Aidha Dkt. Jingu aliongeza kuwa Serikali inazitaka Asasi za Kiraia zinataka kuwa na kanuni maridhawa za matumizi ya fedha na manunuzi kwa namna ambayo hakuna mtu mmoja ndiye mwenye sauti ya mwisho.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa AZAKI Dkt. Sitigmata Tenga amesema Taasisi yake ya Tanzania Foundation for Civil Society awali ilikuwa inatoa ruzuku kwa Asasi mbalimbali imekuwa ili ziweze kukua na pia kuweza kufanya usajili wa kudumu lakini kwa kuwa Taasisi hizo zimeisha imarika kwa sasa malengo ya Taasisi yamebadilika na sasa wanajikita zaidi kwenye uwazi katika matumizi ya rasilimali fedha.

Tunataka kujua kama kila senti inayotumka imetumika kwa thamani ya fedha na kujihakikishia kuwa kila fedha iliyotumika ilifika kwa mlengwa na Taasisi zinawekeza kwa faida kwa kila senti wanayiopata’’.Alisisitiza Dkt. Tenga.

 Asasi za kiraia zinakutana mjini Dodoma kwa Siku tano katika Mkutano wao kwa lengo la kupata jukwaa na Serikali pamoja na wabunge, Sekta binafsi na wabia wengine ili kubadilisha taarifa na uzoefu kuhusu fursa mbalimbali za ubia na ushirikiano.
  Katibu Mkuu Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ,Dkt John Jingu akikata utepe kufungua maonesho ya Wiki ya Asasi za Kiraia Tanzania AZAKI yanayofanyika  jijini Dodoma kwa siku tano kuanzia Oktoba 22-26, 2018.
 Katibu Mkuu Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ,Dkt John Jingu akitoa hotuba yake wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Asasi za Kiraia Tanzania AZAKI inayoendelea leo jijini Dodoma Kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Uratibu Profesa Faustine Kamuzora na kulia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Usajili na Uratibu Wa NGOs Bw. Leornard Baraka .
 Kaimu Msajili wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali wa  Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ,Bw. Leornad Baraka akijibu hoja za wadau Wiki ya Asasi za Kiraia Tanzania AZAKI yanayofanyika  jijini Dodoma kwa siku tano kuanzia Oktoba 22-26, 2018 kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ,Dkt John Jingu.
 Baadhi ya wadau wa Mkutano wa Asasi za kiraia wakifuatilia kwa makini yanayojili katika Mkutano Mkuu wa Asasi za Kiraia Tanzania AZAKI unaofanyika  jijini Dodoma kwa siku tano kuanzia Oktoba 22-26, 2018. Picha na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad