HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, October 8, 2018

UBALOZI WA SWEDEN WATOA ZAIDI YA BILION 14 ZA KITANZANIA KWA FCS

Kwa kipindi hiki ambacho tunahitaji kuelekea katika sera ya uchumi wa viwanda Tanzania inahitaji jamii iliyo huru, yenye demokrasia na inayofuata haki katika juhudi zake za kuwaleletea maendeleo wananchi wake.

Hayo yameelezwa jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society Bw. Francis Kiwanga wakati akipokea Ruzuku ya shilingi billion 14.3 za kitanzania ambayo ni sawa dola za kimarekani milioni 6.25 kutoka katika Ubalozi wa Sweden wa hapa Tanzania kwa ajili ya kuwezesha kazi za Asasi za Kiraia (AZAKI).

Ruzuku hiyo itatumika katika kujenga demokrasia na utawala bora kwa kuboresha AZAKI, kuongeza ushawishi na ushiriki wa wananchi katika maswala ya sera za maendeleo pamoja na mafunzo kwa kipindi 2018 – 2020.
Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society Bw. Francis Kiwanga akisaini hati ya kupokea msaada wa zaidi ya bilion 14 za kitanzania kutoka Ubalozi wa Sweden hapa nchini kwa ajili za kuwezesha Asasi za Kiraia.

Makubaliano hayo yamefanyika jana oktoba 5, 2018 katika ubalozi wa Sweden hapa nchini Tanzania uliopo posta jijini Dar es salaam na kutiwa saini na Balozi wa Sweden nchini Bw. Anders Sjoberg pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society  Bw. Francis Kiwanga.

Akiongea baada ya zoezi la kusaini Ruzuku hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa  Foundation For Civil Society Bw. Francis Kiwanga amesema kuwa Taasisi hiyo imejikita katika kuwasaidia watanzania na imeweka nguvu kubwa katika kuimiza uwajibikaji na utawala bora pamoja na kuwajengea uwezo vijana, wanawake na makundi mengine ili kusaidia maendeleo yao na ya  nchi kwa ujumla.

“Sekta ya Asasi za Kiraia (AZAKI) nchini sasa ni jukwaa madhubuti la kuhabarisha, kuwezesha na kuhamasisha wananchi kufuatilia,kuhoji na kushiriki katika jitihada za serikali katika ngazi zote. Ruzuku hii kwa kiwango kikubwa sana itatuongezea nguvu katika kufanikisha hilo”. amesema Bw. Kiwanga
Balozi wa Sweden nchini Bw. Anders Sjoberg akisaini mkataba na Taasisi ya FCS wa kusaidia AZAKI za hapa nchini, mkataba huo uliosainiwa jana katika ubalozi wa Sweden hapa Tanzania.

Ameongeza kuwa kwa miaka 16 sasa uwezeshaji wa FCS kwa azaki umefikia wilaya zote za Tanzania bara na Zanzibar, kupitia utoaji Ruzuku na huduma za kujenga uwezo kwa Asasi zaidi ya 5000, Na nyingi ni za ngazi ya chini na katika jamii zilizopo vijijini.

Kwa upande wake balozi wa Sweden nchini Bw. Anders Sjoberg alisema kuwa Sweden imeamua kushirikiana na Foundation for Civil Society kutokana na uwezo pamoja na kujituma kwake katika kuwezesha sekta ya asasi za kiraia ili kushiriki kikamilifu katika kujenga utawala bora nchini Tanzania.

“Kuwezesha asasi za kiraia kunatoa nafasi ya kujenga uwajibikaji na uwazi katika jamii” alisema Balozi Sjoberg


Balozi wa Sweden nchini Bw. Anders Sjoberg akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Bw. Krancis Kiwanga wakati wa kusaini Ruzuku kwa ajili ya kusaidia AZAKI za hapa nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad