HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, October 20, 2018

TRA yawaonya wafanyabishara kariakoo

Na mwandishi wetu, Dar es salaam
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewaonya wafanyabiashara wa eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam, wanaotumia risiti moja iliyotolewa kwenye mashine ya EFD kwa ajili ya kusafirishia mzigo zaidi ya mmoja kutoka eneo la Kariakoo kwenda eneo la Jangwani wanapoenda kupakia mizigo kwa ajili ya kusafirisha mikoani, kwani atakayekamatwa adhabu yake ni faini ya asilimia 200 ya kodi iliyopaswa kulipwa katika mzigo huo.
Onyo hilo limetolewa na Kamishna wa Kodi za Ndani kutoka TRA Bw. Elijah Mwandumbya, alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara wa eneo la Kariakoo katika utaratibu wake wa kuwafuata wafanyabiashara katika maeneo yao na kuzumgumza nao masuala mbalimbali ya kodi. 
Kamishna Mwandumbya amesema kuwa TRA imethibitisha kwamba, baadhi ya wafanyabiashara wanaotumia mikokoteni au magari madogo ya kubebea mizigo maarufu kama ‘Kirikuu’, wanatumia risiti moja iliyotolewa kwenye mashine ya EFD muda wa asubuhi ili kupeleka mzigo eneo la Jangwani, na risiti hiyo hiyo inaendelea kutumika kusafirishia mizigo mingine hadi jioni kwa safari zaidi ya mara moja.
“Tumethibitisha hata wengine, risiti ile ile moja imetolewa asubuhi, inapeleka mizigo jangwani kwa kutumia kirikuu kwenda na kurudi mpaka jioni, hii siyo sawa, ni vyema kila mmoja atimize wajibu wake, jambo hili tutalijadili,” amesema Bw. Mwandumbya.
Bw.Mwandumbya, amesema hata kwenye vitabu vitakatifu vinaonesha kwamba mtoza ushuru hapendwi, ila TRA inapenda kujenga mazingira mazuri ya mahusiano kati ya mtoza ushuru na mlipakodi.
Aidha, Kamishna Mwandumbya, amesisitiza wafanyabiashara wa eneo la Kariakoo nan chi nzima, kutoa risiti sahihi za mauzo yao lakini pia kuchukua risiti pale wanapofanya mazunuzi ya bidhaa za jumla na rejareja ili kuepuka usumbufu wowote kutoka kwa maofisa wa TRA wanapokuwa kwenye operesheni.
“Niwaombe wafanyabishara na watanzania wenzangu tudai na tuchukue risiti za EFD kwa kila manunuzi tunayofanya, hii itaisaidia kuongeza mapato ya serikali na kuiwezesha nchi kufikia malengo yake pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuunga mkono juhudi za rais wetu”, amesema Mwandumbya.
Naye mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Mch. Silva Kiondo, amesema imekuwa Faraja kwa Kamishna kukutana na wafanyabiashara wa eneo la kariakoo kwa kuwa wanayo mambo mengi ya kujadiliana ili kuifufua Kariakoo kibiashara.
“Nadhani, sababu kubwa iliyomfanya Kamishna wa Kodi za Ndani kufika hapa ni kutaka kuona Kariakoo inafufuka kibiashara”, amesema.
 Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA Bw. Elijah Mwandumbya akijibu hoja za wafanyabiashara wa eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam alipokutana nao kwa mazungumzo katika mkutano uliofanyika mtaa wa Mchikichi eneo la Kariakoo
 Mfanyabiashara wa Kariakoo Bw. Emmanuel Mwakatungila, akiuliza swali wakati wa mkutano kati Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA na wafanyabishara wa eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam. 
Wafanyabiashara wa eneo la Kariakoo jijini Dar es salaam wakimsikiliza Kamisha wa  Kodi za Ndani Bw. Elijah Mwandumbya alipofanya nao mkutano katika mtaa wa Mchikichi, Kariakoo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad