HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 19, 2018

SERIKALI KUONGEZA MAWASILIANO ENEO LA UWEKEZAJI MKURANGA

NAIBU Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amefanya ziara ya kukagua upatikanaji wa mawasiliano kwenye Wilaya ya Mkuranga iliyopo mkoa wa Pwani na kuahidi wananchi kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaongeza mawasiliano kwenye Wilaya hiyo ambayo ina viwanda vingi vyenye uwekezaji wa aina mbali mbali

Amesema kuwa katika ziara yake amebaini kuwa yapo baadhi ya maeneo ambayo yanahitaji kuongezewa nguvu ili mawasiliano yaweze kufika eneo kubwa zaidi na kupeleka mawasiliano kwenye baadhi ya maeneo ambayo yana ukosefu wa mawasiliano kwenye Wilaya hiyo kwa kuwa mawasiliano ni maendeleo, uchumi na ulinzi na usalama.

Amefafanua kuwa, “kimsingi mawasiliano yapo Mkuranga ila tunatakiwa kuongeza nguvu ili wananchi wapate mawasiliano. Tunahitaji wananchi wa Tanzania wawasiliane,” amesema Nditiye. Ameongeza kuwa minara iliyopo inaweza kuongezwa nguvu, kampuni nyingine zitafunga mawasiliano kwenye minara ya kampuni nyingine zilizopo na kujenga minara kwenye maeneo ambayo hayana mawasiliano kabisa. 

Nditiye amemshukuru Ulega na kuwapongeza wananchi wa Tanzania kwa kuonyesha uhitaji wa mawasiliano na wamegundua mawasiliano ni maendeleo yao, uchumi, ulinzi na usalama. Amesema kuwa karibu asilimia 60 ya eneo la Mkuranga halina mawasiliano na ameyataka makampuni ya simu yaliyojenga minara kwenye Wilaya ya Mkuranga kuongeza nguvu ya mawasiliano kutoka teknolojia ya 2G hadi teknolojia ya 4G. 

Naye Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, Mhe. Abdallah Ulega ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi amesema kuwa Mkuranga haina mawasiliano ya uhakika, kuna shida kubwa sana ya mawasiliano. “Tumefanya ziara ya kuja kuona hali halisi ya upatikanaji wa mawasiliano kwenye Wilaya ya Mkuranga ya upatikanaji wa mawasiliano ya uhakika, baadhi ya vijiji havina mawasiliano ya uhakika na wengine hawana mawasiliano kabisa na eneo hili lina wawekezaji wengi wa viwanda na mawasiliano yanawawezesha wananchi kutoa taarifa za masuala ya ulinzi na usalama”, amesema Ulega. Ameyataja maeneo hayo kuwa vijiji vilivyopo kwenye kata ya Mkuranga, Mpeko, Tengelea, Bupu, Kimanzichana, Kisegese, Mkamba, Lukanga, Magawa, Msonga, Dondo, Vikindu na kata ya Mbezi.

Akijibu kiu ya wananchi waliojitokeza wakati wa ziara hiyo, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Mhandisi Peter Ulanga akiwa kwenye ziara hiyo amesema kuwa UCSAF ilikuwa inaangalia Wilaya ya Mkuranga kwa muda na eneo lote la Mkuranga wataliangalia ili liweze kupata mawasiliano. “Serikali inaangalia mawasiliano kama dhana ya mkakati wa maendeleo ya wananchi kiuchumi, ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tutakuwa tumefikisha mawasiliano ya uhakika kwenye vijiji vyote” amesema Ulanga. Ameongeza kuwa Mkuranga ina kata 25 na tumeona bado kuna matatizo ya mawasiliano ambapo katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2018/2019, UCSAF itapeleka mawasiliano kwenye kata 100 zilizopo kwenye maeneo mbali mbali nchini ambapo watatoa kipaumbele kwenye kata za Mkuranga ambapo kuna uwekezaji mkubwa

Naye Meneja wa Kampuni ya Simu ya Vodacom wa Wilaya ya Mkuranga, Godfrey Kamage amesema kuwa, “tumepokea maoni ya wananchi na maelekezo ya Serikali, tutafikisha hili makao makuu ya Vodacom ili kuongeza nguvu ya mawasiliano kutoka 2G hadi 3G na yaweze kufika mbali zaidi,”.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kushoto) akifafanua jambo wakati wa ziara yake ya kukagua upatikanaji wa mawasiliano kwenye vijiji mbali mbali vya Wilaya ya Mkuranga. (wa kwanza kushoto) Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Mbunge wa jimbo hilo,Abdallah Ulega.
(Picha na Emmanuel Massaka wa Global ya jamii)
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kushoto pili ) akimsikiliza kwa makini Mbunge wa Mkuranga Abdallah Ulega kuhusu ukosefu wa mawasiliano ya uhakika kwenye eneo hilo. Wa kwanza kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Mhandisi Peter Ulanga.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (mstari wa mbele katikati) akikagua upatikanaji wa mawasiliano kwenye kata ya Mkamba Wilayani Mkuranga

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta,Nditiye akitoa maelekezo namna minala ya mawasiliano itakavyo jengwa katika ya  Wilayani Mkuranga mkoa wa Pwani.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad