HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 10 October 2018

RC NDIKILO AKABIDHIWA MIFUKO YA SARUJI 960 KWA AJILI YA KUKARABATI UWANJA WA CCM PICHANDEGE

Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo amekabidhiwa mifuko ya saruji 960 kutoka kwa wadau wa maendeleo, kwa ajili ya ukarabati wa uwanja wa Chama Cha Mapinduzi (Sabasaba), Picha Ndege Kibaha ,ambao haujawahi kutumika tangu mwaka 1989.

Uwanja huo unatarajiwa kutumika kwenye maonyesho ya bidhaa mbalimbali  zinazozalishwa katika viwanda mkoani hapo kuanzia octoba 29-Novemba 4 mwaka huu.

Ndikilo alikabidhiwa saruji hiyo kutoka kampuni ya Mwanza Huduma Ltd ambao wametoa mifuko 660 na kampuni ya saruji Kisarawe Lucky Cement Company mifuko 300.

Aidha Ndikilo alielezea ,wameamua kuandaa maonyesho hayo ili kuvitangaza viwanda hivyo na bidhaa wanazozalisha ambapo mkoa unakadiriwa kuwa na viwanda 400.

"Misaada hii kwani itasaidia kufanikisha ukarabati wa uwanja wa maonyesho hayo yatakayoanza mwishoni mwa mwezi huu," alisema Ndikilo.

Alisema ,maonyesho hayo pia yatahamasisha uwekezaji wa viwanda kwenye mkoa na kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano.

"Tunaunga mkono jitihada za Rais Dk John Magufuli za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda vitakavyopelekea kuwa nchi yenye uchumi wa kati," alisema Ndikilo.

Mkurugenzi wa kampuni ya Kisarawe Lucky Cement Company Samir Jaffar alisema , wamejitolea Saruji hiyo yenye thamani ya sh.milioni nne kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za mkoa katika suala la uwekezaji wa viwanda.

Jaffar alisema , wao kama wenye viwanda wanampongeza Rais kwa kuweka nguvu kwenye suala la viwanda kwani ndiyo njia pekee ya kuinua uchumi na kufungua milango ya ajira.
Mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo akipokea mifuko ya saruji 960 kutoka kwa Mkurugenzi wa kampuni ya Kisarawe Lucky Cement Company Samir Jaffar  kwa ajili ya ukarabati wa uwanja wa Chama Cha Mapinduzi (Sabasaba), Picha Ndege Kibaha ,ambao haujawahi kutumika tangu mwaka 1989.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad