HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 18, 2018

PROFESA MBARAWA AZINDUA KAMPENI YA UTUNZAJI WA VYANZO VYA MAJI

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa  amezindua rasmi Kampeni ya Upandaji Miti kandokando ya vyanzo vya maji nchi nzima mkoani Mtwara kwa lengo la kuhakikisha vyanzo hivyo vinatunzwa na kuwa endelevu kwa miaka mingi ijayo.
Profesa Mbarawa amezindua kampeni hiyo kwa kupanda miti nane katika chanzo cha Mtawanya kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Mjini na kuzitaka Bodi zote za Mabonde tisa nchini kuweka mkazo na mipango madhubuti ya kusimamia na kutunza rasilimali za maji ziweze kuwa endelevu.
Ametoa agizo hilo kutokana na uvamizi na uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji katika maeneo mengi kwa sasa nchini, hali inayohatarisha kiasi kikubwa cha maji kupungua kutokana na vyanzo vingi kukauka, hali inayoweza  kusababisha ukosefu wa maji ya kutosha kwa ajili ya miradi inayoendelea kutekelezwa na Serikali.
Na kutaka vyanzo vyote vya maji vitunzwe na kulindwa kwa kupandwa miti maalumu inayohifadhi maji na kuagiza wale wote wanaofanya shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo waache tabia hiyo na watakao kaidi wachukuliwe hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine kwa kuwa sheria inaweka bayana kuhusu jambo hilo. 
Ametoa tamko hilo kwa kuzingatia Sheria ya Maji Na, 11 ya Mwaka 2009 inayokataza kufanya shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji, na ikieleza shughuli zote za kibinadamu zifanyike umbali wa mita 6o kutoka chanzo cha maji kilipo na kutaka maeneo yote yawekewe mipaka na vizuizi kuonyesha ukomo wa watu kuingia kwenye vyanzo hivyo.
‘‘Hatutaki kupata hasara kwenye miradi tunayowekeza fedha nyingi, halafu baadae iwe kama magofu kwa kukosa maji. Imefika hatua kuwa ni lazima tuchukue hatua za lazima kuinusuru taifa letu na uhaba wa maji. Niwatake wananchi watoe ushirikiano wa karibu na Serikali kuhakikisha vyanzo vyetu vyote vinakuwa endelevu kwa kuzalisha maji ya kutosha na kuwa na uwezo wa kutoa huduma ya uhakika kwa miaka ijayo’’, amezungumza Profesa Mbarawa. 
‘‘Kwa kuanza tumepanda miti nane katika chanzo hiki cha Mtawanya, nataka ifikapo Disemba mwaku huu, nikute zaidi ya miti 1,000 kwenye chanzo hiki na zoezi hili lifanyike nchi nzima kwa sababu kama waziri mwenye dhamana ya kusimamia rasilimali za maji nitalisimamia jambo hili ipasavyo’’, ameonya Profesa Mbarawa.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mjini, Evod Mmanda amesema ni muhimu zoezi la upandaji miti liwe endelevu lenye kuzingatia upandaji wa miti na kuachana na miti isiyo rafiki na maji kwa lengo la utunzaji wa maeneo yote yenye vyanzo na kutaka wananchi wazingatie sheria iliyopo kwa hiari, pasipo kutumika nguvu na kuonya kuwa hatavumilia uharibifu wa vyanzo vya maji katika wilaya yake.
Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Maji hivi karbuni imetoa Shilingi Bilioni 2.3 kwa ajili ya malipo ya madai kwa wakandarasi mbalimbali wanaotekeleza miradi ya maji katika Mkoa wa Mtwara, ambapo uzalishaji wa maji kwa siku kwa mji wa Mtwara umefikia lita milioni 10, huku mahitaji kwa siku ni lita milioni 13.7.
Fedha hizo zimetolewa kwa lengo la kuongeza kasi ya ujenzi wa miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma, ambapo hadi sasa miradi 45 ikiwa imeshakamilika na mingine 33 ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
 Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akiwa kwenye mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa.
 Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akipanda mti kwenye chanzo cha Mtawanya, Mtwara Mjini.
 Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mzingira Mtwara (MTUWASA), Mhandisi Mashaka Sita katika Mitambo ya Maji Mangamba, Mtwara MJini.
 Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akizungumza na wakazi wa Msanga Mkuu, Mtwara Vijijini.
Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akiinama kwa ajili ya kuonja na kujua ubora wa maji katika mradi wa Mpapura, Mtwara Vijijini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad