HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, October 2, 2018

MKURUGENZI MKUU WA TAKUKURU AWEKA WAZI NAMNA ATAKAVYOIENDESHA TAASISI HIYO NYETI YA KUPAMBANA NA WALA RUSHWA NCHINI

Awaaga Rasmi Watumishi na Wananchi wa Mkoa wa Kagera Kama Katibu Tawala wa Mkoa

Na Sylvester Raphael
Mkurugenzi Mkuu mpya wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) nchini Kamishina wa Polisi Diwani Athumani aongea rasmi na Vyombo vya Habari nchini kwa mara ya kwanza akiwa Mkoani Kagera na kutaja vipaumbele vyake katika kuiongoza TAKUKURU ili iweze kufanya kazi kwa kasi na ufanisi katika mapambano dhidi ya rushwa.

Mkurugenzi Mkuu Diwani Athumani akitaja vipaumbele hivyo Oktoba Mosi, 2018 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba kwenye hafla fupi ya kuongea na kuwaaga rasmi Watumishi wa Serikali kama Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera alisema kuwa vipaumbele hivyo vimegawanyika katika sehemu kuu mbili ambapo kuna vipaumbele vya muda mfupi na vya muda mrefu ili kuifanya TAKUKURU kutekeleza majukumu yake kulingana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Vipaumbele vya Muda Mfupi; Kwanza ni kuwasimamia watumishi walio chini ya TAKUKURU kuchapa kazi kwa bidii na kuachana na utendaji wa mazoea. Pili, atahakikisha anachukua hatua stahiki na kwa wakati kwa watumishi wote watakaojihusisha na vitendo vya rushwa. Tatu, Kupeleka Kesi zote za masuala ya rushwa  Mahakamani na kufuatilia mienendo ya kesi hizo. Nne, kufuatilia miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa kama inatekelezwa kwa thamani stahiki kulingana na fedha iliyotolewa na Serikali.

Vipaumbele vya Muda Mrefu: Kwanza, Kufanya uchunguzi katika mfumo wa mapato ili kuziba mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali. Katika kipaumbele hiki Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Diwani Athumani alitolea mfano wa Wafanybiashara wanaotoa risiti za (EFD) zenye gharama pungufu ya kiwango cha fedha tofauti na thamani halisi ya bidhaa ilyonunuliwa kutoka katika maduka yao.

Kipaumbele cha Pili ni kufuatilia kesi zote za rushwa  zilizopo Mahakani na kuhakikisha kesi hizo zinafika mwisho kwa kutolewa hukumu. Tatu, Kutoa elimu kwa umma kuhusu athari za rushwa na kuelimisha wananchi kutojihusisha na vitendo vya rushwa kwani madhara yake ni makubwa. Nne, Kuweka mfumo mzuri wa kuhakikisha wananchi wanatoa taarifa za wala rushwa lakini pia kuhakikisha wananchi hao wanalindwa mara baada ya kutoa taarifa za kweli. Tano, ni kuongeza ushirikiano kati ya TAKUKURU na wadau wote katika mapambano dhidi ya wala rushwa nchini.

Mkurugenzi Mkuu mpya wa (TAKUKURU) nchini Kamishina wa Polisi Diwani Athumani alisema kuwa ameweka vipaumbele hivyo katika kutekeleza majukumu yake akiwa Mkurugenzi Mkuu lengo kuu likiwa ni kumsaidia Rais John Pombe Magufuli katika mapambano dhidi ya rushwa nchini. Lakini pia kuhakikisha anashirikiana na wadau wote wapinga rushwa kuhakikisha kaulimbiu ya “Tanzania Bila Rushwa Inawezekana”  inatimia.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mkuu Diwani Athumani alisema kuwa tayari maelekezo yote aliyopewa na Rais John Pombe Magufuli wakati akimuapisha Chamwino Jijini Dodoma  Septemba 12, 2018 tayari ameanza kuyafanyia kazi yote ili kuhakikisha TAKUKURU inatimiza wajibu wake kwa wakati na kupambana kisawasawa na wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa nchini.

Kamishina wa Polisi Diwani Athumani aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera tangu Novemba 2016 na kuteuliwa rasmi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Septemba 2018 alitoa wito kwa watumishi wote na wananchi kusoma alama za nyakati hasa wakati huu wa Serikali ya Awamu ya Tano kutojihusisha na vitendo vya rushwa kwani si salaam sana kwa wala rushwa nakusisistiza kuwa kesi ya rushwa haiozi hata kama ikipita miaka ishirini mhusika atafikishwa Mahakamani na kufirisiwa mali zake zote.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti akitoa neno katika hafla hiyo fupi alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Diwani Athumani kwa kuteuliwa na Rais John Pombe Magufuli kuiongoza Taasisi hiyo nyeti. Pili aliwapongeza watumishi na wananchi wa Mkoa wa Kagera kwa kutoa ushirikiano kwa Diwani Athumani katika majukumu yake akiwa Kagera mpaka Rais akamuona na kumteua kuiongoza Taasisi nyeti nchini.

Pili, Mkuu wa Mkoa Gaguti alimshukuru Diwani Athumani kwa kusimamia vizuri raslimali za Serikali na kusimamia utekelezaji wa miradi ya Serikali Mkoani Kagera hasa mara baada ya Tetemeko la Ardhi lililotokea Septemba 10, 2016. Na miradi hiyo imekamilika kikamilifu na thamani ya fedha inaonekana katika miradi hiyo ambapo alitoa mfano wa Shule za Sekondari za Ihungo na Nyakato kuwa kuwa za kisasa baada ya kujengwa upya.

Aidha, Mkuu wa Mkoa Gaguti alimuhaidi Mkurugenzi Mkuu mpya wa TAKUKURU kuwa Mkoa wa Kagera utampa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake kwenye Taasisi mpya kwake ili kuhakikish rushwa inakomeshwa nchini ukiwemo na Mkoa wa Kagera. Pia Mkuu wa Mkoa Gaguti alimshukuru Diwani Athumani kuona umuhimu wa kutoa msimamo wake wa kuiendesha TAKUKURU akiwa Mkoani Kagera kuwa ameupa Mkuo huo heshima kubwa.

Mwisho naye Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Bw. Nesphory Chacha Bwana aliyekabidhiwa Majukumu ya Katibu Tawala wa Mkoa Kagera na Kamishina wa Polisi Diwani Athumani alihaidi kuendeleza kusimamia majukumu aliyoachiwa kuyasimamia kikamilifu ikiwemo kuendelea na utatuzi wa migogoro ya wananchi, Kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali, Kushirikiana na watumishi katika kutekeleza majukumu ya Serikali na mwisho kufuatilia mifumo ya Seri.
 Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Nchini Kamishina wa Polisi Diwani Athumani akiongea na watumishi wa mkoa wa Kagera wakati wa ziara yake pamoja na kuwaaga.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Mstaafu Marco E Gaguti akitoa shukrani zake kwa  Diwani Athumani
 Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Bw. Nesphory  Bwana akitoa neno katika hafla fupi ya Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kuongea watumishi.
Watumishi wakimsikiliza kwa umakini Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Diwani Athumani
 Baadhi ya waandishi wa habari mkoani Kagera wakiwa katika picha ya pamoja na mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU Diwani Athumani.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad