HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 12 October 2018

KLABU YA SIMBA WAFANYA KISOMO KUMUOMBA MUNGU MO APATIKANE AKIWA SALAMA


*Hassan Dalali,wanachama watoa ya moyoni, wasema hivi..
Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
UONGOZI wa Klabu ya Simba umeamua kufanya dua na kisomo maalumu kwa lengo la kumuomba Mwenyezi Mungu ili Mfadhili wao na mwanachama wa klabu hiyo Mohamed Dewji 'MO' apatikane akiwa salama.

Kisomo hicho kimefanyika leo mchana katika Makao Makuu ya Klabu ya Simba yaliyopo mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam ambapo mashabiki wa Simba wameshiriki kisomo hicho. Kabla ya kisomo wameelezwa wazi lengo lao kuu ni kumuomba Mwenyezimungu aweze kuleta wepesi kwenye matatizo yaliyompata Mlezi na Mwekezaji wao Mohamed Dewji 'MO' 

Kaimu Katibu Mkuu wa Klabu ya Simba Hamis Kisiwa amesema kuwa wamekusanyika kufanya dua leo hii wakiamini Mwenyezi Mungu ndio muweza wa kila jambo na hivyo huko aliko Mohammed Dewji apatikane na arudi akiwa salama.

Amesema hayo baada ya kufanyika dua na kisomo maalumu kwa lengo la kumuomba Mungu afanye wepesi kwa kuwezesha Mo kupatikana."Wana Simba tumefanya kisomo ilo Mo aachiweakiwa salama.Kwa mwanachama wa Simba na sio wa Simba wamekusanyika kufanya dua hiyo ili Mohamed aachiwe akiwa salama na ndio msingi wa dua yetu," amesema Kisiwa

Amesisitiza kuwa wanaamini kwa dua hiyo Mo Dewji ataachiwa akiwa salama kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu Mungu.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa zamani wa Klabu ya Simba Hassan Dalali amesema lengo la dua hiyo ni kumuomba Mwenyezi Mungu ili mwanachama na mfadhili wao Mohamed Dewji aweze kupatikana akiwa salama. Amefafanua kwamba  wamefanya dua kwa ajili ya kuomba ili huko awe salama na wanaomba Mungu amfanyie wepesi.

"Mwenyezi Mungu amfanyi wepesi huko aliko arudi tuungane naye,pia aungane na familia yake.Ni tukio ambalo limetusikitisha sana.Hivi kama linatokea kwa ndugu yako utajisikiaje," amesema.

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Klabu ya Simba Said Tully amesema walichokifanya leo ni kumuomba Mwenyezi Mungu katika kufanikisha MO anapatikana akiwa salama. Pia amewaomba mashabiki wa Simba wote nchini kufanya dua na visomo kumuomba Mungu kuwezesha 'MO' Dewji anapatikana.

Amesema MO ni mfadhili wa  Simba na amekuwa na malengo makubwa kuhakikisha Simba inatimiza malengo yake. Hivyo amesema kikubwa ni kuendelea kufanya maombi ili huko aliko awe salama na arejee kuungana nao akiwa salama.

Ameomba mashabiki wa Simba kuwa watulivu na kuacha vyombo vya ulinzi na usalama viendele kufanya yake.Wakati huo huo Mwanachama wa Klabu ya Simba Saabun Abdulrahim Saadala amesema anamuomba Mungu huko aliko Mo awe salama.

"Tunamuombaa Mwenyezi Mungu mfadhili wetu apatikane akiwa salama .Ni kipenzi chetu, arudi akiwa salama na tunamuomba Mungu wana Simba waendelee kuwa wamoja," amesema.

Mwanachama Rehema Kabunju kutoka tawi la Mpira Pesa amesema tukio lililomtokea bosi wao limewaumiza mashabiki wa Simba na watanzania wote kwa ujumla. "Tumeumizwa sana na tukio ambalo limetokea kwa bosi wetu.Kwa mashabiki wa Simba hill ni tukio ambalo limetuacha na takari.Kikubwa tunaomba apatikane akiwa mzima," amesema.
Kaimu Katibu mkuu wa Klabu ya Simba Hamis Kisiwa wapili kushoto akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo mara baada ya kufanya kisomo kumuombea Mlezi wa klabu hiyo Mohamed Dewji ambaye ametekwa jana Oktoba 11 hoteli ya collesium jijini Dar es Salaam.
 Wanachama wa Klabu ya Simba wakimsikiliza kaimu katibu mkuu wa klabu ya Simba Hamisi Kisiwa  jijini Dar es Salaam leo mara baada ya kufanya kisomo kumuombea Mlezi wa klabu hiyo Mohamed Dewji ambaye ametekwa jana Oktoba 11 hoteli ya collesium jijini Dar es Salaam.
Wanachama wa Klabu ya Simba wanawake wakishiriki kwenye kisomo cha kumwombe Mlezi wa klabu hiyo jijini Dar es Salaam leo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad