HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, October 23, 2018

AZAM vs JKT TANZANIA KESHO UWANJA WA MEJA JENERALI ISAMUHYO MBWENI


BAADA ya kucheza mechi nne nyumbani, Azam  itakuwa ugenini kuvaana na JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaofanyika Kesho kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.

Azam  inaenda kucheza na JKT ikiwa na ari kubwa baada ya kushinda mechi tatu mfululizo huku ikivuna pointi 10 kati ya 12 katika mechi nne zilizopita, hadi sasa ikiwa kileleni kwa pointi zake 21 baada ya kucheza mara tisa, ikishinda sita, sare tatu na kutopoteza hata mmoja.

Wapinzani wao JKT Tanzania wanaofundishwa na Bakari Shime, nao hawajapoteza mchezo wowote hadi sasa ikiwa nafasi ya tisa kwenye msimamo na pointi zake 15, ikishinda mechi tatu na kutoka sare sita.

Kocha Msaidizi wa Azam , Juma Mwambusi, ameweka wazi kuwa wamekiandaa vema kikosi chao kwa ajili ya kupata matokeo mazuri kwenye mchezo huo huku akidai wanawafahamu vilivyo wapinzani wao.

Kuelekea mchezo huo, Azam  inatarajia kumkosa kiungo wake na Nahodha Msaidizi, Frank Domayo ‘Chumvi’, ambaye anasumbuliwa na majeraha ya goti akitarajia kukosekana kwa miezi minne huku pia Nahodha Agrey Moris, akiwa mgonjwa akitarajiwa kutokuwa sehemu ya mechi hiyo.

Kiungo wake mshambuliaji, Tafadzwa Kutinyu, aliyekuwa kwenye majukumu ya timu yake ya Taifa Zimbabwe tayari ameshajiunga na wenzake mazoezini tayari kwa maandalizi ya mchezo huo.

Huo utakuwa ni mchezo wa 19 timu hizo kukutana kwenye ligi hiyo, kwa mara ya kwanza zilikutana Septemba 6, 2008 ukiwa ni msimu wa kwanza tokea Azam FC ipande daraja, ilishuhudiwa JKT Ruvu ikishinda mabao 2-1 huku pia wakipata ushindi kama huo kwenye mechi ya mzunguko wa pili.

Katika mechi 18 zilizopita, Azam FC imeonekana kuwa na wastani mzuri wa kushinda mechi nyingi pamoja na mabao mengi dhidi ya JKT Tanzania, imeshinda mara 10, ikafungwa tatu huku nne zikiisha kwa sare.

Jumla ya mabao 47 yamefungwa katika mechi hizo 18, ukiwa ni wastani wa kufungwa mabao 2.6 kwenye kila mechi, Azam FC imefunga robo tatu kati ya hayo ikiweka nyavuni 33 huku JKT Tanzania yenyewe ikitupia 14 tu.

Hii ni mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana tokea JKT Tanzania ibadilishe jina kutoka JKT Ruvu Stars hadi jina hilo la sasa na Azam FC nayo kuwa rasmi kampuni msimu huu ikijulikana kama Azam FC Company Limited, pia matajiri hao watacheza kwa mara ya kwanza kwenye uwanja huo mpya wa maafande hao.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad