HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 17 September 2018

WAKANDARASI MIRADI YA UMEME WATAKIWA KUANZISHA YADI MAALUM

Na Veronica Simba – Chato
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewataka wakandarasi wote nchini wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini, kuwa na Yadi maalum za kuhifadhi vifaa katika maeneo wanakotekeleza miradi hiyo, ili kuondoa kisingizio cha kutowaunganishia wananchi umeme kutokana na kutokuwepo na vifaa.
Aliyasema hayo, jana Septemba 16, 2018 katika Kijiji cha Kahumo wilayani Chato, akiwa katika ziara ya kazi, ambapo pia aliwasha umeme rasmi kijijini hapo.
“Kuanzia sasa nawaelekeza muwe na Yadi zenu ambapo mtahifadhi vifaa vyote vya kazi na sisi Serikali tutazikagua. Maneneja wa TANESCO kagueni Yadi hizo.”
Waziri alitaja vifaa vya kazi vinavyotakiwa kuwepo katika Yadi hizo kuwa ni pamoja na nyaya za umeme, nguzo, transfoma pamoja na mita za Luku.
Aidha, akiwa katika Kijiji cha Magiri wilayani humo, ambako pia aliwasha umeme rasmi, Waziri Kalemani aliwaasa wananchi kuepukana na vishoka wakati wanapotaka kutandaziwa mfumo wa nyaya za umeme katika makazi yao.
Aliwataka wananchi kujiridhisha na uhalali wa mafundi watakaowatumia kuwatandazia mfumo wa nyaya, katika Ofisi za TANESCO zilizopo katika maeneo yao. Akifafanua, alisema majina ya mafundi wenye sifa yatatundikwa katika Ofisi hizo ili kuwarahisishia wananchi kuwatambua hivyo kuepukana na vishoka.
Waziri aliwahamasisha wananchi kuhakikisha wanalipia huduma ya kuunganishiwa umeme huo wa bei nafuu, ambao ni shilingi 27,000 tu ili wanufaike na Mradi husika wa Umeme Vijijini (REA), kwani Mradi huo utakapoisha, watalazimika kuunganishiwa umeme kwa bei ya kawaida, ambayo ni kubwa.
Akizungumza na wananchi wa Chato Mjini katika mkutano wa hadhara, Waziri alitoa maelekezo kwa wakandarasi wa REA, kuhakikisha wanawaunganishia umeme wananchi wasiopungua 10 kwa mkupuo kila siku, tofauti na ilivyo sasa ambapo wengi wao wamekuwa wakiwaunganishia umeme wananchi wachache tu katika maeneo wanakotekeleza miradi hiyo.
“Natoa rai kwa wataalam wangu wa TANESCO na REA nchi nzima kuhakikisha wakandarasi wanaotekeleza miradi hii nchi nzima, wanawaunganishia umeme wananchi wasiopungua 10 kwa mkupuo kwa siku moja, kila tunapokwenda kuwasha umeme.”
Hata hivyo, Waziri Kalemani aliwapongeza watendaji wa TANESCO na REA kwa kazi nzuri wanayofanya ambapo alisema kuwa hali ya umeme nchini imeimarika na kwamba umeme haukatiki-katiki.
Waziri Kalemani yuko katika ziara ya kazi Kanda ya Ziwa, ambapo mbali na Mkoa wa Geita, atatembelea pia Mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme pamoja na kuzungumza na wananchi.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Magiri wilayani Chato, Mkoa wa Geita akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme, Septemba 16, 2018.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, akiwasha umeme katika moja ya nyumba za wakazi wa Kijiji cha Kahumo wilayani Chato, Mkoa wa Geita, kuashiria kuwashwa rasmi kwa umeme kijijini humo. Tukio hilo lilifanyika Septemba 16, 2018, wakati Waziri akiwa katika ziara ya kazi.
Wananchi wa Kijiji cha Kahumo wilayani Chato, Mkoa wa Geita, wakimpokea kwa bashasha Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (mwenye shati la bluu-kulia), alipowasili kijijini hapo jana, Septemba 16, 2018, kuwasha rasmi umeme katika eneo hilo.
Kutoka kushoto ni Waziri wa Nishati na Mbunge wa Chato, Dkt. Medard Kalemani, Mbunge wa Nyang’hwale Hussein Kassu na Mbunge wa Igunga Seif Gulamali; wakifurahia jambo, wakati wa Mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Waziri Kalemani Chato Mjini, akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme na kuzungumza na wananchi, jana Septemba 16, 2018.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Chato, Elias Makory, akizungumza wakati wa mkutano wa Waziri wa Nishati, Dkt, Medard Kalemani (hayupo pichani) na wananchi wa Kijiji cha Kasenga, wilayani humo; jana Septemba 16, 2018 akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.
Kutoka kushoto ni Meneja Mwandamizi wa TANESCO Kanda ya Ziwa, Mhandisi Macleen Mbonile, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Geita, Mhandisi Joachim Ruweta na Mhandisi wa Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Salum Inegeja, wakijadiliana jambo wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) wilayani Chato, kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme, jana Septemba 16, 2018.
Waziri wa Nishati, Dkt, Medard Kalemani (kulia), akiwaonesha wananchi wa Kijiji cha Kasenga wilayani Chato, kifaa cha Umeme Tayari, kinachotumika kuunganisha umeme pasipo kutandaza mfumo wa nyaya (wiring). Waziri alikuwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme pamoja na kuzungumza na wananchi, jana Septemba 16, 2018. Pamoja naye pichani (kutoka kushoto) ni Meneja wa TANESCO Wilaya ya Chato, Nyabingiri Nyaonge na Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini katika eneo hilo, Ibrahim Saidi.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kulia), akiwatambulisha kwa wananchi wa Kijiji cha Kahumo wilayani Chato (hawapo pichani), Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini katika eneo hilo, Ibrahim Said (wa kwanza kushoto), Mameneja wa TANESCO (kutoka kushoto) wa Wilaya ya Chato, Nyabingiri Nyaonge, wa Mkoa wa Geita Mhandisi Joachim Ruweta na wa Kanda ya Ziwa, Mhandisi Macleen Mbonile. Waziri alikuwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme, jana Septemba 16, 2018.
Sehemu ya umati wa wananchi katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Chato wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani), alipowatembelea na kuzungumza nao akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, jana Septemba 16, 2018.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad