HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, September 13, 2018

WAGONJWA 20 KUFANYIWA UPASUAJI WA MOYO WA KUFUNGUA KIFUA NA KUWEKEWA VALVU ZAIDI YA MBILI KATIKA KAMBI MAALUM YA MATIBABU

Na Salome Majaliwa - JKCI
11/9/2018 Wagonjwa 20 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua na kuwekewa  valvu zaidi ya mbili (milango ya moyo) kwenye kambi maalum ya matibabu inayofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI). Upasuaji huo unafanywa na madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo kwa kushirikiana na wenzao wa Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya  Misaada (IIRO) ya nchini Saudi  Arabia.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete  Dkt. Bashir Nyangasa wakati akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Dkt. Nyangasa ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu alisema upasuaji huo unafanywa kwa wagonjwa ambao valvu zao tatu hazifanyi kazi vizuri hivyo basi zinabadilishwa na kuwekwa valvu  za bandia.

“Kambi hii ni ya siku saba tangu ilipoanza tumefanya  upasuaji na kubadilisha valvu kwa wagonjwa tisa ambao hali zao zinaendelea vizuri na hii leo  wataanza kutoka katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) na kurudi wodini kuendelea na matibabu”, alisema Dkt. Nyangasa.

Kwa upande wa uhitaji wa damu wakati wa upasuaji Dkt. Nyangasa alisema mgonjwa mmoja  anatumia kati ya chupa tano  hadi saba lakini kama mgonjwa atapata tatizo  anaweza kutumia chupa zaidi ya hizo na kuwaomba wananchi wajitokeze  kwa wingi kuchangia damu. Aidha Dkt. Nyangasa aliwasisitiza wananchi kujiunga na mifuko ya bima za afya wangali na afya njema wasisubiri kujiunga na mifuko hiyo wakati wagonjwa.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya  Misaada (IIRO) Tanzania, Hassan Katungunya alisema wanashukuru kwa wataalam hao kuja hapa nchini kufanya matibabuya moyo  kwa wagonjwa.

Katugunya alisema , “Ni faraja kuona  miongoni mwa watanzania wanyonge wanapata msaada wa matibabu kwani upasuaji wa moyo ni wa gharama na kuna wengine hawana uwezo wa kulipa”.
“Tunaomba uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Saudi Arabia uendelee.  Wageni wetu hawa wamepata faraja  kwa kuona nchi yetu inawajali na hawapati usumbufu wakati wa kuingia na kutoka nchini”,.

Jumla ya wataalam wa afya 15 wamekuja kwa ajili ya kufanya upasuaji wa moyo kati ya hao kuna madaktari bingwa, madaktari wa usingizi na wagonjwa mahututi, wataalam wa mashine za moyo na wauguzi.
Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya Misaada (IIRO) ya nchini Saudi Arabia wakiendelea na kazi ya kumfanyia mgonjwa upasuaji wa kubadilisha valvu ambazo hazifanyi kazi vizuri katika kambi maalum ya matibabu inayofanyika JKCI. Jumla ya wagonjwa tisa wameshafanyiwa upasuaji na hali zao zinaendelea vizuri.
Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya Misaada (IIRO) ya nchini Saudi Arabia wakimfanyia mgonjwa upasuaji wa kubadilisha valvu ambazo hazifanyi kazi vizuri katika kambi maalum ya matibabu inayofanyika JKCI. Jumla ya wagonjwa 20 wanatarajia kufanyiwa upasuaji wa kubadilishwa valvu zaidi ya mbili ambazo hazifanyi kazi vizuri.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad