HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 24 September 2018

RC MAKONDA ASAINI MKATABA WA LISHE ILI KUTOKOMEZA ASILIMIA 14.6 ZA UDUMAVU SUGU KWA WATOTO

Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii
MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda amesaini mkataba na wakuu wa Wilaya zote tano za jiji la Dar es salaam katika kuhakikisha suala la afya na ukuaji wa watoto.

Akizungumza katika hafla hiyo Makonda amesema kuwa mkataba huo uliosainiwa ufanyiwe kazi ili kupunguza asilimia 14.6 za watoto wenye udumavu sugu jijini humo.

Aidha amewataka makatibu tawala katika Wilaya zote kuhusisha suala la lishe katika vikao vyote vya Manispaa hasa kwa Wilaya za Temeke, Kinondoni na Ilala ambazo zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto ukilinganisha na Ubungo na Kigamboni.

Pia amewataka wananchi kuzingatia mlo kamili na usafi katika kuandaa mlo wa watoto kabla ya siku 1000 za mabadiliko kutoka kutokwa kutungwa kwa mimba hadi mtoto afikapo miaka miwili.

Kwa upande wake mratibu lishe kutoka TAMISEMI Mwita Waibe ameeleza kuwa hayo yote ni matekelezo ya makamu wa Rais na wakuu wa Mikoa kote nchini katika kuhakikisha suala la lishe linapewa kipaumbele ili watoto waweze kukua kiafya na akili.

Na amesema kuwa " Kuanzia mimba inapotungwa hadi mtoto kufikia miaka 2 takribani siku 1000 ni siku pekee za kumtengeneza mtoto hasa katika ubongo kwa kuzingatia lishe, na baada ya hapo  mtoto hataweza kuepuka udumavu alioupata" ameeleza. 

Aidha ameeleza kuwa Mikoa ambayo inaongoza kwa uzalishaji wa chakula ndio inayoongoza kwa udumavu ikiongozwa na Rukwa yenye asilimia 50, Katavi, Ruvuma na Mbeya.

Afisa lishe wa Mkoa wa Dar es salaam Janeth Mzamva amesema kuwa hali ya lishe jiji humo si nzuri sana kwani asilimia 34 katika tafiti uliofanyika 2014 unaonesha watoto wana udumavu kwa kukosa lishe.

Aidha amesema kuwa asilimia 3.7 ya watoto wana ukondefu, 20.2 wana uzito uliokithiri (obesity,) asilimia 59  ya watoto chini ya miaka 5 wana upungufu wa damu na amewataka wakuu wa Wilaya kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia mkataba huo.

Mikataba hiyo iliyosainiwa na wakuu wa Wilaya ni agizo la kitaifa la kutenga shilingi 1000 kwa kila mtoto chini ya miaka 5, kupata matone ya vitamini A  sambamba na matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoto chini ya miaka 5.
 Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam,Paul Makonda akizungumza leo na wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi  wa wilaya tano za jijini Dar es salaam katika kuhakikisha suala la afya na ukuaji wa watoto(Picha na Emmanuel Massaka wa Global ya jamii)
 Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam,Paul Makonda(kulia) pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Iala Sophia Mjema(kushoto)  wakisani hati ya makubaliano ya lishe.
 Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam,Paul Makonda (kulia) akimkabidhi hati ya mkataba wa lishe Mkuu wa wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva  leo jijini Dar es Salaam.
 Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (kulia) akimkabidhi  hati ya mkataba wa lishe Mkuu wa Wilaya Ilala, Sophia Mjema(kushoto)  leo jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad