HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 24, 2018

MATAIFA ZAIDI YA 75 YASHIRIKI KONGAMANO LA MAFUTA NA GESI, SERIKALI YATOA NENO

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
SERIKALI imesema imejipanga vema kuhakikisha sekta ya nishati na hasa ya mafuta na gesi inawanufaisha Watanzania wote na kwamba nchi imefanya maandalizi makubwa kwa ajili ya kunufaika na sekta hiyo.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira na Muungano January Makamba wakati anafungua kongamano la pili la wadau wa sekta ya mafuta na gesi wakati anamwakilisha mgeni rasmi Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Kongamano hilo limehudhuriwa na zaidi ya wadau 200 kutoka mataifa zaidi ya 75 duniani na moja ya ajenda ni kuangalia fursa ambazo zinaweza kupatikana katika sekta ya mafuta na gesi huku pia kongamano hilo likijita kuangalia fursa ambazo watanzania watanufaika nazo kutokana na uwepo wa miradi mikubwa inayoendelea nchini.

Hivyo Waziri Januari Makamba amesema ujumbe wa Waziri Mkuu katika kongamano hilo ni kwamba nchi imefanya maandalizi makubwa kwa ajili ya kunufaika na sekta ya gesi na mafuta.

"Pia Serikali imeweka maandalizi ya kutosha ikiwa ni pamoja na kuandaa rasilimali watu, miundombinu, watalaamu na mambo mengine muhimu kwa lengo la kuhakikisha sekta hiyo inawanufaisha Watanzania wote,"amesema Januari Makamba.

Amefafanua Serikali inatambua namna ambavyo gesi asili itatumika kwenye viwanda vya kemikali na kubwa zaidi gesi hiyo itatumika kwenye viwanda vya mbolea na kubwa zaidi huu ni wakati sahihi wa nchi kunufaika na sekta ya nishati.

Akitoa maoni yake binafsi Waziri Januari Makamba amesema ili nchi iweze kunufaika na sekta ya nishati kuna mambo kadhaa ya kutazama na miongoni mwao ni soko la gesi na mafuta ambalo ni la kiulimwengu.

"Soko la mafuta na gesi lipo kwenye nchi chache sana duniani na hivyo kufanya nchi zote duniani kuangalia eneo hilo. Hivyo mwenendo wa siasa na uchumi duniani una uhusiano wa moja kwa moja wa gesi na mafuta,"amesema.

Pia amesema Bara la Afrika ndilo bara ambalo kuna chachu ya kukua kwa maendeleo na kwa kipindi cha miaka 10 limekuwa likiongoza kwa ukuaji wa uchumi wake ikiwamo Tanzania.

Ameongeza ukuaji huo wa maendeleo unakwenda sambamba na ujenzi wa viwanda na hivyo nishati hiyo itasaidia kuchochea ukuaji wa viwanda Barani Afrika na Tanzania kwa ujumla.

Pamoja na hayo amesema ipo haja ya kuangalia gharama za miradi kwani ili Taifa liweze kunufaika lazima lijue gharama za miradi namna ambavyo faida yake inaweza kupatikana.

"Manufaa makubwa kwa nchi ambayo inaweza kupata ni baada ya kutambua gharama za miradi,"amesema na kufafanua ni muhimu kujua faida inapatikana baada ya kuangalia gharama za mradi au laa.

Kwa upande wake Muandaaji wa kongamano hilo ambaye pia ni Mwanzilishi na Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Watoa Huduma za Mafuta na Gesi nchini Tanzania Abdulsamad Abdulrahim amewataka Watanzania wote kuchangia fursa ambazo zinapatikana kutokana na uwepo wa nishati hiyo pamoja na miradi mikubwa inayoendelea nchini ambayo kuna mabilioni ya fedha yatatumika.

Amefafanua sekta binafsi imeamua kushirikiana na Serikali kuandaa kongamano hilo ambalo dhamira yake ni kuhakikisha wadau wanapata fursa ya kujadili na kuchambua kwa kina namna ambavyo watanzania watanufaika na sekta ya gesi na mafuta.

"Kongamano hili limeshirikisha wadau wote wenye miradi mikubwa ya maendeleo na lengo la kuwepo kwao ni kuonesha fursa ambazo zinaweza kupatikana kutokana na uwepo wa miradi hiyo. Sekta binafsi wamejitolea kuandaa kongamano hilo na hiyo inathibitisha namna ambavyo Serikali inashirikiana na sekta binafsi.

"Mataifa zaidi ya 75 yameshiriki ambapo baadhi ya wadau wamekuja na ndege zao. Ni vema Watanzania kokote waliko wakachangamkia fursa hizo ambazo zitapatikana kwenye miradi iliyopo. Nito rai kwa wafanyabishara kuja kwenye kongamano hili kwa ajili ya kuchangamkia fursa na kwa vyombo vya habari tunaomba mueleze umma kuhusu fursa ambazo zipo nchini kwetu kupitia miradi,"amesema.

Abdulrahim amesema kuwa baadhi ya wawekezaji wamekuja nchini na wanaonesha kuhitaji kuwekeza, hivyo ni wakati muafaka wa kuchangamkia fursa zilizopo na hakuna sababu ya watanzania kuendelea kuwa wasindikizaji kila siku na badala yake wahakikishe wanashiriki kwenye fursa zilizopo.

Wakati huo huo Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu ametoa pongezi kwa Abdulrahim kwa kuandaa kongamano hilo huku akielezea namna ambavyo Serikali imejipanga katika kuhakikisha sekta ya nishati ya gesi na mafuta inawanufaisha Watanzania wote.

Ametumia nafasi hiyo kuwaleza wadau hao muhimu namna ambavyo Serikali ya Tanzania imetoka, ilipo na inakokwenda katika sekta ya gesi na mafuta na kuwahakikisha imejianda vema na ndio maana imetoa muelekeo wake kuhusu sekta hiyo.
Baadhi ya washiriki wa kongamano wa mafuta na gesi wakisikiliza maada kuhusu sekta hiyo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira na Muungano January Makamba akizungumza wakati akifungua kongamano la pili la wadau wa sekta ya mafuta na gesi jijini Dar es Salaam leo kuhusu kongomano la wadau wa mafuta na gesi.
Waziri wa wizara ya Ardhi, nyumba, maji, nishati na mazingira Zanzibar, Salama Aboud Talib akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu kongomano la wadau wa mafuta na gesi.
Naibu waziri wa wizara ya nishati, Subira Mgalu akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu kongomano la wadau wa mafuta na gesi.
Muandaaji wa kongamano la mafuta na gesi ambaye pia ni Mwanzilishi na Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Watoa Huduma za Mafuta na Gesi nchini Tanzania Abdulsamad Abdulrahim akifafanua jambo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad