Na Mwandishi Wetu, Pugu
WAZIRI Mkuu mstaafu, Mizengo Peter Pinda, amesema asasi zisizo za
kiserikali zitachochea vikubwa maendeleo ya uchumi na ustawi wa
jamii nchini endapo zitahamasisha ushiriki wa vijana na wanawake
kwenye sekta za kilimo, uvuvi na biashara.
Akizungumza na ujumbe wa Agri-Thamani Foundation ya Mkoa wa Kagera
uliomtembelea nyumbani kwake Pugu, Dar es Salaam ili kumshukuru kwa
kuwa mlezi wa asasi hiyo, Waziri Mkuu mstaafu ameeleza thamani na
nguvu asasi zizizo za kiserikali duniani kote katika kusaidiana na
serikali kuneemesha maendeleo ya wananchi na akaahidi kutumia asasi
hiyo kuinua lishe katika Mkoa wa Kagera.
“Mimi pia ni mkulima na nina uzoefu wa muda mrefu katika kilimo. Kwa
sababu hii naamini nitaweza kuchangia vyema katika kuiongoza taasisi
hii kufikia malengo yake na kwa kuunga mkono azma ya serikali ya
awamu ya tano kujenga uchumi wa kati na viwanda…Ni matumaini yangu ni
kwamba tutashirikiana kuinua lishe Mkoa wa Kagera. La muhimu ni
ushirikiano na uaminifu wa hali ya juu, ameasa Bw Pinda.
Ametumia fursa hiyo kuwaeleza Watanzania kwamba ili asasi zisizo za
kiserikali zifikie malengo yake, ni lazima zihamasishe ushiriki wa
vijana na wanawake katika sekta za kilimo, uvuvi na biashara na
kufafanua kwamba, ni muhimu kuthaminisha mazao ya wakulima ili
waweze kunufaika. Uzalishaji wa mazao ukiongezeka, ameeleza, uhitaji
wa viwanda kuchakata mazao hayo yataongezeka pia.
Kiongozi huyo ameeleza kuwa tatizo la unyafuzi limesababishwa na
kukosekana lishe bora, kwani lishe bora ni muhimu kwa afya njema na
kumwezesha mtu kujikinga na magonjwa mbalimbali na kuahidi kwamba yeye
binafsi atahakikisha asasisi hiyo inashirikiana na wizara ya afya na
taasisi nyingine za afya ndani na nje ya nchi ili elimu ya lishe
iwafikike walengwa kwa usahihi vijana na wanawake wa Mkoa wa Kagera
kutambua umuhimu wa lishe na afya bora katika juhudi za kuleta
maendeleo.
Naye Mwenyekiti na mwanzilishi Bi. Neema Lugangira ambaye ni
mwanzilishi na mwenyekiti wa taasisi hiyo amesema sehemu pekee ambayo
lishe bora inaweza kupatikana Ni kupitia Kilimo, ufugaji na uvuvi.
Hivyo kuwaomba wananchi wa Kagera hasa vijana na wanawake wa Kagera
ambao ndio wanufaika wakubwa wa taasisi hii kutoa ushirikiano wa
kutosha na kujituma ili kujiendeleza kiuchumi na kutumia mazao hayo
katika kujenga afya zao.
“Ili taifa liwe endelevu linahitaji kuwa na wananchi wenye afya nzuri,
kimwili na kiakili pamoja na nguvu ya kufanya kazi. Nitoe wito kwa
vijana na wanawake wa Kagera kutumia fursa hii kwa kushirikiana na
taasisi yetu katika kutokomeza tatizo la utapia mlo na magonjwa
mengine ya lishe mkoani Kagera,” aliongeza Bi.Neema Lugangira
Alisema Tanzania inategemea wananchi wake kutumia fursa zilizopo
kuendelea. Na katika kutimiza hili, vijana wanategemewa kwa kiasi
kikubwa. Na kwasababu kilimo ni uti wa mgongo wa taifa hawana budi
kuwekeza juhudi zao katika kilimo.
“Ni matumaini yangu wananchi wa Kagera wataweza kuondokana na
umaskini, kuimarisha hali ya lishe na ushiriki wenu katika mnyororo
wa thamani wa kilimo, mifugo na uvuvi kuimarika.” Bi Lugangira
alisisitiza.
WAZIRI Mkuu mstaafu Mizengo Peter Pinda(kushot) akizungumza na Mwenyekiti wa Asasi isiyo ya kiserikali
Agri Thamani Foundation kutoka Kagera, Bi. Neema Lugangira (kulia). Mzee
panda ni mlezi wa asasi hiyo alielezea umuhimu wa kutoa elimu
sambamba na uboreshaji wa upatikaji wa lishe bora pamoja na
kuwaunganisha vijana na wanawake katika sekta zingine za kimkakati
hapa nchini ili kutokomeza unyafuzi na umaskini.
No comments:
Post a Comment