HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, 2 September 2018

MWILI WA MWANAFUNZI ALIYEFARIKI KWA KUPIGWA VIBOKO NA MWALIMU WAKE WAZIKWA WILAYANI MULEBA

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa  na Serikali za Mitaa Mhe. Joseph Sinkamba Kandege akitoa heshima za mwisho kwa Mwlili wa Mwanafunzi Marehemu Sperius Eradius aliyefariki dunia Agosti 27, 2018 baada ya kupigwa viboko na Mwalimu wake wa nidhamu katika Shule ya Msingi Kibeta Manispaa ya Bukoba.

Na ALLAWI KABOYO, MULEBA

Mwlili wa Mwanafunzi Marehemu Sperius Eradius aliyefariki dunia Agosti 27, 2018 baada ya kupigwa viboko na Mwalimu Respicius Mtazangira ambaye alikuwa Mwalimu wa nidhamu katika Shule ya Msingi Kibeta Manispaa ya Bukoba umeagwa  na kusafirishwa Wilayani Muleba Kata Mubunda Kijiji Kitoko nyumbani kwa baba yake mzazi Eradius Petro na kuzikwa leo Agosti 31, 2018.

Katika mazishi hayo Serikali iliwakilishwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa  na Serikali za Mitaa Mhe. Joseph Sinkamba Kandege ambaye alitoa salaam za Serikali katika msiba huo kwa kuwahakikishia familia, ndugu, jamaa wa marehemu pamoja na wananchi waliojumuika kumuaga Sperius Eradius kuwa lazima Serikali isimamie haki mpaka ipatikane kwa waliohusika katika tukio la mauaji ya mwanafunzi huyo.
“Sisi tunawaacha watoto wetu waende shule kama sehemu salaama tukiamini kuwa ndiyo sehemu salama na ya kujifunzia na siyo chuo cha mafunzo ya viboko. Jambo hili haliwezi kuachwa likapita  hivi hivi tuseme inatosha na iwe fundisho kwa wengine.” Alisisitiza Mhe. Naibu Waziri Kandege.

Pia Mhe. Naibu Waziri Kandege  aliiomba familia ya marehemu kuwa na subira kwa wakati huu mgumu wa kupoteza mpedwa wao Sperius Eradius na kusema kuwa msiba si wao tu bali ni msiba wa taifa zima. Aidha, aliishukuru Serikali ya Mkoa ilivyoshughulikia tukio hilo tangu lilipotokea Agosti 27, 2018 hadi kuupumzisha mwili wa Mwanafuzi Marehemu Sperius Eradius nyumbani kwa baba yake mzazi Eradius Petro. 

Baba yake mlezi Mchungaji Justus Balilemwa akitoa historia ya Mwanafunzi Marehemu Sperius Eradius alisema kuwa mtoto huyo alizaliwa Mei 2005 na mara baada ya kuzaliwa mama yake aliaga dunia na Sperius Eradius kuchukuliwa na kupelekwa Ntoma katika Kituo cha kulelea watoto yatima na baada ya mwaka mmoja alimchukua mtoto huyo na kuanza kuishi na kumlea kama mtoto wake hadi mauti yalipomkuta Agosti 27, 2018 akiwa na umri wa miaka 13 Shuleni Kibeta Manispaa ya Bukoba.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa  na Serikali za Mitaa Mhe. Joseph Sinkamba Kandege akizungumza katika mazishi ya Mwanafunzi Marehemu Sperius Eradius aliyefariki dunia Agosti 27, 2018 baada ya kupigwa viboko na Mwalimu wake wa nidhamu katika Shule ya Msingi Kibeta Manispaa ya Bukoba.

“Kinachonisikitisha leo hii ni kuwa tulimchukua Sperius Eradius akiwa mzima lakini leo tumerudisha sanduku, haikuwa nia yetu tulitamani sana mtoto huyu atimize ndoto zake kwa kuwa alikuwa mchangamfu sana na alimjua Mungu kwa kuimba na kumtukuza Mungu katika Kwaya mbalimbali mfano kwaya ya Kagoma.” Alimalizia kwa uchungu mkubwa baba mlezi wa Sperius Eradius Mchungaji Justus Balilemwa.

Baba yake mzazi Marehemu Sperius Eradius, Eradius Petro akitoa neno kwa wananchi waliofika kumfariji katika mazishi hayo alisema yeye anamwachia Mungu kwa yaliyotokea bali anaishukuru Serikali kwa kulifuatilia tukio hilo kwa karibu sana. Pia na kutoa ushirikiano nyumbani kwa baba mlezi tangu tukio linatokea hadi kwenye mazishi ya Sperius Eradius.
Serikali ya Mkoa wa Kagera tangu kutokea kwa tukio hilo la mauaji ya Mwanfunzi Sperius Eradius (13) Agosti 27, 2018 imekuwa ikigharamia mahitaji yote katika familia ya baba mlezi na kugharamia jeneza la kumhifadhia marehemu pamoja na usafiri wa kusafirisha mwili wa marehemu, familia, ndugu na jamaa wa Sperius kutoka Kibeta kwenda Mubunda Kijiji Kitoko kwa ajili ya Mazishi. Aidha, Naibu Waziri  Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Kandege alitoa Shilingi Milioni mbili kwaniaba ya Serikali.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad