HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 28 September 2018

Mkutano mkuu wa kwanza wa MDIN wafanyika Sweden


Picha ya pamoja ya wana MDIN baada ya mkutano mkuu wa kwanza uliofanyika mjini Stockholm, Sweden katika ukumbi wa Ubalozi wa Tanzania. Kutoka kushoto Balozi Dkt. Wilbroad Slaa, Bi. Josephine Slaa, Bi. Joyce Kimwaga Lundin, Katibu Mkuu Ahmed Salum Ahmed na wanachama wengine wa MDIN.

Jumamosi ya tarehe 15 Septemba taasisi isiyo ya kiserikali ya Muheza Diaspora International Network (MDIN) ilifanya mkutano wake mkuu wa kwanza kwa wanachama wote. Taasisi ya MDIN iliyosajiliwa rasmi mwaka 2017 ina malengo ya kuchangia maendeleo ya Watanzania, hasa wale wenye kipato cha chini waweze kujiendeleza kupitia viwanda vidogo vya miradi ya kilimo na ufugaji.

Mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden, ulimualika Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mheshimiwa Balozi Dkt. Wilbroad Slaa kuwa mgeni rasmi. Mheshimiwa Balozi Dkt. Slaa aliambatana na mkewe, Bi. Josephine Slaa, ili kusikiliza mipango na changamoto za taasisi hii tangu kuanzishwa kwake rasmi. Pamoja nao, alialikwa pia Mwenyekiti wa Baraza la Diaspora la watanzania Duniani au TDC-Global, Norman Jasson.
Kutoka kushoto, Bi. Elizabeth Lugendo, Bwana Matiku Kimenya na mke wa Balozi Dkt. Slaa, Bi. Josephine Slaa  wakifuatilia kwa makini hoja katika mkutano mkuu cha MDIN. 

Kwa kipindi hiki, taasisi ya MDIN imejikita kwenye miradi ya majaribio katika Wilaya ya Muheza mkoani Tanga. Alipoulizwa kama taasisi hii inahusiana na Muheza peke yake, Mwenyekiti wa MDIN, Bi. Joyce Kimwaga Lundin, alisema "Jina la Muheza Diaspora International Network limetokana na sababu kuwa wengi kati ya waanzilishi, wametokea Muheza, lakini lengo ni kuleta maendeleo Tanzania nzima. Kutokana na sisi kuifahamu vizuri Muheza, tumeona tuanzie hapo ili tukishapata matokeo mazuri tuweze kusambaza hii miradi sehemu mbalimbali Tanzania. Lakini, sababu ya pili ni ubora wa ardhi ya Muheza ambayo ina uwezo wa kustawisha kila kitu bila tatizo. Hivyo, tunashirikiana na wataalamu wa viwanda, kilimo pamoja na mifugo katika kutafuta njia mbadala ili kuongeza faida kwa mkulima na kuinua kiwango chake cha maisha."

Mkutano huo ulijumuisha watanzania toka nchi mbali mbali duniani kama vile Norway, Ufaransa, na Sweden. Wana MDIN walitumia mkutano huu kutathmini safari yao tangu kuanzishwa kwake hadi walipofikia. Walitumia muda huo kuchambua mafanikio, changamoto na vikwazo walivyokutana navyo kabla ya kuanzisha MDIN hadi pale taasisi ilipotengemaa na kuanza kufanya miradi ya maendeleo katika wilaya ya Muheza mkoani Tanga.

Kwa upande wake, Balozi Slaa aliwashukuru na kuwapongeza wana MDIN kwa kuwa na malengo na mipango endelevu kusaidia watanzania nyumbani, hasa kwa kugusa watu wa chini zaidi "Nishukuru sana kwa jitihada mlizozichukua, nimeelezwa aina ya shughuli mnazofanya. Nimeelezwa kuwa mnatafuta fedha zenu kisha mnanunua vitu na kuvisafirisha Tanzania kwa ajili ya kuwasaidia watanzania wenzenu. Sina maneno ya kuwashukuru, lakini ninasema Asante. Hii inaonyesha ni jinsi gani Watanzania walivyo wazalendo hata kama wamechukua uraia wa nchi nyingine."

Pamoja na hayo, Balozi Slaa aliwasihi wana MDIN kumshirikisha kama kutakuwa na changamoto ya aina yeyote itakayojitokeza katika kutimiza majukumu yao ya kuwekeza nchini Tanzania ili aweze kuchangia mawazo na hata kuwapa mwongozo sahihi pale inapohitajika.
Kwa kuongezea, Bi. Josephine Slaa aliwapa moyo wana MDIN na kuwasihi wasikate tamaa hata kama vikwazo vitazidi kuwa vingi, kwani mara nyingi mwanzo huwa mgumu. Aliongeza pia, ni vizuri kama wakipanga mipango ya muda mfupi na ya muda mrefu ili kuweza kuona juhudi zao zinazaa matunda mapema na kuwapa moyo ili kutokata tamaa mapema. Hii inatokana na ukweli kuwa mipango ya muda mrefu huchukua muda kuzaa matunda, na binadamu hukata tamaa pale anapoona juhudi zake hazizai matunda.

Vilevile, Bi. Josephine Slaa aliwataka MDIN kujenga nia ya kubadilisha zaidi mtazamo na fikra za Watanzania kwa kutoa elimu sahihi juu ya dhana ya maendeleo ili misaada yao iwe endelevu. Aliongeza, "Mtazamo ndio kila kitu katika kuleta maendeleo. Kama mtaendelea kutaka kusaidia watanzania bila kuwasaidia kuboresha namna tofauti ya kufikiria, hamtoweza kuwapa maendeleo ya kweli na hawatoyathamini. Ni vizuri kama mtawawezesha ili waone wana mchango mkubwa katika kujiendeleza, ninyi mkishirikiana nao kwa karibu na siyo kuwapa msaada bila wao kuwa na kitu cha kuchangia."

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TDC-Global, Bw. Norman alitoa shukrani kwa taasisi ya MDIN kwa mwanzo wake mzuri na kuitakia kila lakheri katika kutimiza malengo yake. Pamoja na hayo, yeye kama Mwenyekiti wa TDC-Global ameahidi kutoa ushirikiano na kuwa karibu kabisa na taasisi hii ili kuweza kutimiza malengo ya pamoja ya kusaidia kuindeleza Tanzania, kwani ni lengo kuu la TDC-Global. TDC-Global ni jumuiya inayounganisha Watanzania wote waishio kwenye Diaspora, huku wanachama wake wakiwa ni watu binafsi pamoja na jumuiya mbalimbali za Watanzania waishio ughaibuni.

Kwa bahati ya kipekee, MDIN walipata kumkaribisha pia Katibu Mkuu Ofisi ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambaye pia ni kiongozi wa dawati la Diaspora kwa upande wa Zanzibar, Mheshimiwa Salum Maulid Salum. Katibu Mkuu alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano wa TDC Global uliofanyika mjini Stockholm, Sweden. Mh. Salum Maulid Salum alitoa pongezi kwa Watanzania waishio nje kwa kuwa na ari ya kuchangia maendeleo ya nchi yao na kuahidi kushughulikia masuala yote yahusuyo Diaspora kwa ukaribu na kwa ufanisi mkubwa ili kuweza kurahisisha juhudi zao katika kuwekeza nyumbani.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Salum Maulid Salum akitoa neno kwa wana MDIN alipohudhuria sherehe hizo kwa muda mfupi.

Maadhimisho ya mwaka mmoja ya MDIN yalifanyika kwa awamu mbili, ambapo baada ya kikao cha asubuhi kulikuwa sherehe ya kuitambulisha rasmi taasisi hii kwa Watanzania wa Sweden ikiwa pia na lengo la kuzalisha kiasi cha fedha cha kufanyia miradi ya maendeleo huko Muheza.Sherehe za jioni zilihudhuliwa na Watanzania mbalimbali toka mji wa Stockholm, kati yao akiwemo mke wa Balozi, Bi. Josephine Slaa pamoja na Katibu Mkuu Ahmed Salum Ahmed. Sherehe ilipambwa kwa uwepo wa mziki wa Dansi toka kwa Dekule Band, inayopita miziki yenye mahadhi ya Kiafrika. Sherehe za jioni zilijumuisha pia chakula cha kiafrika na vinywaji mbalimbali kwa waliohudhuria.

Hadi sasa MDIN ina wanachama hai takribani ishirini (20) waliotapakaa nchi tofauti duniani, ikiwemo Thailand, Afrika Kusini, Ufaransa, Norway, Sweden, Ujerumani na Tanzania. Wanachama hawa, hata kama siyo wote wanatokea Muheza, wana dhumuni moja kubwa - kutafuta njia ya kuwekeza Tanzania ili kuwapatia huduma bora wananchi wa kawaida. Katika mipango yao ya hapo baadae, wana MDIN walieleza nia yao ya kusaidia watu walioko kijijini kupata elimu bora juu ya kilimo bora na chenye faida, kuendeleza miradi mbalimbali katika jamii na pia kutumia makapi ya kilimo kama chanzo cha miradi mingine.


MDIN inapanga kufanya mikutano kama hii kila mwaka katika nchi tofauti. Mkutano wa mwakani unategemewa kufanyika Muheza, Tanzania ili kuwa karibu na sehemu miradi ya maendeleo  inapofanyika na kuitambulisha rasmi taasisi ya MDIN kwa Wanamuheza.


Taasisi ya MDIN inapatikana kwenye tovuti ya www.muhezadiaspora.org na pia ina ukurasa wa Facebook www.facebook.com/muhezadiaspora/.
Dekule Band ikitumbuiza waliokuja kuunga mkono sherehe za MDIN kutimiza mwaka mmoja. 
No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad