HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 28 September 2018

MAKAMU WA RAIS AZINDUA KIKOSI KAZI CHA KUTATUA CHANGAMOTO ZA VIUMBE WAGENI/VWAMIZI NCHINI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema ni vema kama nchi tukajipanga mapema kuhakikisha kwamba viumbe vamizi hawaendelei kushamiri ili kuepusha Taifa kuingia kwenye gharama kubwa za kukabiliana na janga hilo hapo baadaye.
Makamu wa Rais ameyasema haya wakati wa uzinduzi wa Kikosi Kazi cha Kutatua Changamoto za Viumbe Wageni/ Vamizi nchini uliofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Pamoja na kwamba viumbe hawa ni janga la kiuchumi, kimazingira na kiafya  lakini bado halijashughulikiwa kikamilifu hususani katika elimu ya kuzuia viumbe hawa na kuwa na mipango madhubuti ya kukabiliana nalo” alisema Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais amesisitiza kuwa Janga hili si la sekta moja. Kama tulifanya makosa huko nyuma kushughulikia jambo hili kila sekta kivyake tangu sasa TUACHE.  
Amezitaka Sekta zote na Taasisi zifanye kazi kwa pamoja kwa kupeana taarifa na mikakati ya kukabiliana na changamoto hii. Na kutaka ushirikishwaji wa wadau wote wakiwemo, Halmashauri za wilaya ,Wizara za kisekta, Serikali za Mitaa, Asasi za Serikali na zisizo za Serikali, Sekta binafsi pamoja na wananchi pamoja na vyombo vya habari.
Akitoa rai kwa waliochaguliwa kuunda Kikosi Kazi cha Kitaifa, Makamu wa Rais alisema “Tambueni kuwa mmepewa jukumu kubwa la kulisimamia suala hili kikamilifu. Kafanyeni kazi kulingana na Hadidu za Rejea tutakazo wakabidhi ili mwisho wa yote kuwe na matokeo chanya ya kazi mliyopewa na Taifa”.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano wa Mazingira Mhe. January Makamba amesema kuwa aligundua tatizo hili mara baada ya kufanya ziara yake ambapo amekuta athari za mimea na viumbe vamizi zimekuwa kubwa na tishio kwa wananchi hivyo kuona kuna kila sababu ya kuanza kulishughulikia.
Kikosi kazi hicho chenye wajumbe 18 kilichozinduliwa leo kitaongozwa nchi ya Mwenyekiti Dkt. Ezekiel Mwakalukwa.
Viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla, Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Juma Awesu, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega pamoja na wadau mbali mbali wa mazingira.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa uzinduzi wa Kikosi kazi cha kutatua changamoto za viumbe wageni/ vamizi nchini. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akihutubia wakati wa  Uzinduzi wa Kikosi cha kutatua changamoto za Viumbe Wageni/ Vamizi nchini uliofanyika kwenye kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
 Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi john Malongo akiwatambulisha Wajumbe 18 wa Kikosi Kazi cha kutatua changamoto za viumbe wageni/ vamizi nchini wakati wa uzinduzi wa kikosi kazi hicho kilichozinduliwa leo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. 
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa kikosi kazi cha kutatua changamoto za viumbe wageni/ vamizi nchini mara baada ya uzinduzi wa Kikosi kazi hicho uliofanyika kwenye kituo cha kimataifa cha mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, wengine Pichani ni Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangalla (kushoto), Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Juma Awesu, Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad