HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 20 September 2018

MADEREVA BODA WANAOPORA SIMU KUKIONA -SSP MAGOMI


NA MWAMVUA MWINYI, PWANI
WILAYA ya kipolisi Chalinze, mkoani Pwani, haitakuwa na muhali na madereva pikipiki (boda boda) ambao wamekuwa na tabia za kupora simu za watu kisha kutokomea kusikojulikana .

Aidha madereva hao wameaswa kufuata sheria za usalama barabarani bila kuzikiuka ili kujiepusha na migongano inayojitokeza baina yao na askari wa usalama barabarani kutokana na kukaidi kuzifuata sheria hizo.

Mkuu wa polisi wilaya ya kipolisi Chalinze, SSP Janeth Magomi alitoa rai hiyo, wakati wa kikao cha polisi jamii kilichohusisha madiwani, wenyeviti wa serikali za mitaa, maafisa tarafa, viongozi wa dini, wananchi na madereva pikipiki.

Alifafanua , jeshi hilo limejipanga kuhakisha wenye tabia hizo wanadhibitiwa kwani wamejipanga kwa kushirikiana na vikundi vya ulinzi shirikishi kuweza kuwakamata bodaboda wote wenye tabia hizo.

SSP Janeth , alitakiwa madereva bodaboda  pia kujisajili katika ofisi za serikali za mitaa ili waweze kutambuliwa kisheria kutokana na huduma ya usafiri wanayoitoa kwa jamii.

"Iwapo madereva pikipiki watafanya kazi zao kwa kufuata sheria na kutambulika kila mmoja kijiwe anachopaki pikipiki yake, ni rahisi kuweza kuzuia uhalifu"

Alisema sheria wanazijua na wengine wanapewa elimu hivyo wazitii ili kuondokana na kukamatwa kwa makosa mbalimbali na usumbufu.

"Nyie mtakuwa ni wenye kuzuia watu wasiofahamika kupaki kwenye vijiwe vyenu na wale wenye nia ovu ya kutenda matukio ya uhalifu kuweza kudhibitiwa"alisema SSP Janeth.

Hata hivyo, SSP Janeth alisema, kwa kufanya hivyo itasaidia pale tukio la uhalifu linapotokea mhusika aweze kubainika kwa wepesi na kuweza kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mwenyekiti wa kamati ya amani alhaji Nasoro Hamisi ,aliomba jeshi la polisi kudumisha amani na usalama wa wananchi wa Chalinze .

Alitoa wito kwa viongozi wa serikali za mitaa pamoja na jeshi la polisi kuwa na kumbukumbu za madereva bodaboda wanaokesha katika vijiwe mbalimbali ikiwepo kuweka picha zao katika ofisi hizo ili waweze kutambulika.

Kwa upande wake ,ofisa wa polisi jamii mkoa wa Pwani (ASP) Grase Salia aliwataka wenyeviti wayatumie madaftari ya wakazi kujaza taarifa za wageni wanaoingia kwenye maeneo yao.

Alibainisha,  jambo hilo litaweza kusaidia kuwa na taarifa za wakazi wa eneo husika na iwapo patatokea uhalifu inakuwa rahisi kufanya ufuatiliaji.
 Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Chalinze SSP Janeth Magomi (wa tatu kulia) akifuatilia changamoto za wananchi wakati wa kikao cha polisi jamii huko Chalinze(picha na Mwamvua Mwinyi)
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Chalinze SSP Janeth Magomi akikagua paredi huko Chalinze. (picha na Mwamvua Mwinyi

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad