HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, August 26, 2018

Waziri Mwakyembe atoa Miezi 3 kwa Maafisa Utamaduni kukamilisha ukusanyaji wa maoni ya Sera

 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe(katikati) akitoa maagizo kwa Maafisa Utamaduni Mkoa na Wilaya nchini kukamilisha ukusanyaji wa maoni ya wadau wa Sekta ya Utamaduni kwa ajili ya kuboresha Sera ya Utamaduni ya Mwaka 1997 katika ufunguzi wa Mkutano wa Saba wa Umoja wa Machifu uliyofanyika leo katika Kijiji cha Marangu Mkoani Kilimanjaro,Kushoto ni Mlezi wa Umoja wa Machifu Tanzania Waziri Mkuu Mstaafu Mhe.John Samuel Malecela na kulia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Utamaduni Bi.Lilian Beleko kutoka Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo.
 Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu Tanzania Chifu Frank Marrialle (kushoto) akitoa ahadi ya umoja huo kuwasilisha maoni yao kwa ajili ya kuboresha Sera ya Utamaduni ya Mwaka 1997 kwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe(hayupo pichani) katika ufunguzi wa Mkutano wa Saba wa Umoja wa Machifu Tanzania uliyofanyika leo katika Kijiji cha Marangu Mkoani Kilimanjaro,kulia kwake ni Mlezi wa Umoja wa Machifu Tanzania Waziri Mkuu Mstaafu Mhe.John Samuel Malecela.
 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe (kulia) akikabidhi nakala 21 za Sera ya Utamaduni ya Mwaka 1997 kwa Mlezi wa Umoja wa Machifu Tanzania Waziri Mkuu Mstaafu Mhe.John Samuel Malecela (kushoto) katika Ufunguzi wa Mkutano wa Saba wa Umoja wa Machifu Tanzania,uliyofanyika leo katika Kijiji cha Marangu Mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kugawa kwa Machifu waliyoshiriki Mkutano huo ili waweze kutoa maoni yao kutokana na mapungufu ya sera hiyo inayofanyiwa marekebisho.
 Chifu Nshoma Hawa wa Ukamba Kahama akieleza  changamoto zinazomkumba katika ikulu yake ambapo ardhi ya himaya yake iliyozikiwa machifu wenzake kuporwa na kugawiwa kwa wananchi kwa ajili ya kilimo kinyume na utaratibu wa uhifadhi wa ardhi za makazi ya machifu kwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe (hayupo pichani) katika Mkutano wa Saba wa Umoja wa Machifu Tanzania uliyofanyika leo katika Kijiji cha Marangu Mkoani Kilimanjaro.
 Chifu Emmanuel Zulu Gama kutoka kwa Wangoni Songea akimwomba  Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe(hayupo pichani) ofisi yake kushiriki katika Tamasha la Mashujaa waliyopigana Vita ya Majimaji linalofanyika kila Mwaka Mwezi Februari mkoani Songea,katika ufunguzi Mkutano wa Saba wa Umoja wa Machifu Tanzania uliyofanyika leo katika Kijiji cha Marangu Mkoani Kilimanjaro.
 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe aliyeketi (watano kushoto) akiwa katika picha ya pamoja  na baadhi ya Machifu wa Tanzania mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Saba wa  Umoja wa Machifu Tanzania uliyofanyika leo katika Kijiji cha Marangu Mkoani Kilimanjaro,wanne kulia ni Mlezi wa Umoja wa Machifu Tanzania Waziri Mkuu Mstaafu Mhe.John Samuel Malecela,na wanne kulia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu Tanzania Chifu Frank Marrialle.

Na Anitha Jonas – WHUSM- Marangu
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe amewataka Maafisa Utamaduni Mkoa na Wilaya kuwahimiza wadau wa Sekta ya Utamaduni kuwasilisha maoni yao ndani ya miezi mitatu.
Mheshimiwa Mwakyembe ametoa kauli hiyo  leo katika Kijiji cha Marangu Mkoani Kilimanjaro alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Saba wa Umoja wa Machifu nchini wenye lengo la kujadili namna ya kuhakikisha umoja huo unasajiliwa kisheria pamoja na kuzungumzia nini kifanyike kutokana na kuwepo na mmomonyoko wa maadili katika jamii kwa kiasi kikubwa.
“Serikali iko katika mchakato wa kufanya maboresho ya Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997 ambayo imeonekana kuwa na mapungufu kulingana na hali ilivyosasa,hivyo basi nitoe rai kwenu Machifu kama wadau wakuu wa Sekta ya Utamaduni kutoa maoni yenu kwa haraka kwani yatasaidia kwa asilimia kubwa kuongeza ubora katika sera hii tunayoboresha na hivyo basi hakikisheni mnawasilisha maoni yenu kwa Maafisa Utamaduni ndani ya miezi hiyo,”alisema Mhe.Dkt.Mwakyembe.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu Tanzania Chifu Frank Marrialle alieleza kuwa umoja huo ulianza tangu mwaka 2014 na mpaka sasa unajumla ya wanachama 105 na kupitia umoja huo umekuwa ukisisitiza wajumbe wake kusimamia utunzaji mazingira pamoja usimamazi wa maadili katika jamii  kwani machifu ndiyo mhimili wa kulinda utamaduni wa taifa.
 “Mbali na Machifu hawa kujitahidi kupigania usimamizi wa maadili katika jamii zao wamekuwa wakikumbwa na changamoto nyingi kwani kwa baadhi ya maeneo wamekuwa wakitolewa maneno ya dharau na kejeli kwa kuwaelezwa kuwa utawala wao umepitwa na hauna maana kwa sasa ombi letu kwa serikali ni kuhakikisha kupitia maoni yetu tutakayowasilisha kwa ajili Sera hii ya Utamaduni inayofanyiwa marekebisho yatiliwe mkazo ili kuonyesha wa nguvu ya machifu kwa jamii,”alisema Marrialle.
Aidha,akiendelea kuzungumza Chifu Marialle alipongeza uongozi wa serikali ya awamu ya tano kwa kusimamia utunzaji wa rasilimali za nchi kwa kuhakikisha hakuna utoroshwaji unaofanyika kwa lengo la taifa kupata faida  itakayosaidia kuleta maendeleo nchini.
Pamoja na hayo nae  Chifu Nshoma Hawa wa Ukamba - Kahama alitoa ombi lake kwa serikali la kuomba kusaidiwa kutokana na ikulu yake kuvamiwa na wanasiasa na kugaiwa kwa wananchi kwa matumizi ya kilimo kinyume na utaratibu wa himaya hiyo kwani eneo hilo ndipo walipozikwa machifu wote wa ukoo huo.
Halikadhalika nae Mlezi Mteule wa Umoja wa Machifu Tanzania Mheshimiwa Waziri Mkuu Mstaafu Mhe.John Samuel Malecela alieleza kufurahishwa na uteuzi huo na kuahidi kushirikia na Machifu hao katika kuhakikisha Machifu hao wanafanikiwa kuleta maendeleo kwa taifa pamoja na kusimamia hali ya kupambana na mmomonyoko wa maadili uliyopo sasa kutokana na hali ya utandawazi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad