HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, August 14, 2018

WAZIRI JENISTA MHAGAMA AITAKA CMA KUONGEZA KASI YA UTATUZI WA MIGOGORO YA KIKAZI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, (kushoto), akiagana na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), Bw. Masha Mshomba (wapili kushoto), mara baada ya kufungua mafunzo ya siku tatu kwa watumishi wa Tume katika Utatuzi wa Migogoro ya Kikazi na Tathmini ya Utendaji Kazi(CMA), mjini Morogoro leo Agosti 14, 2018. Wengine ni Mkurugenzi Mkuu wa CMA, Bw. Shanes Nungu, (wakwanza kulia), Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mjini, Bi. Regina Chonjo, na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Bw.Noel Kazimoto. Mafunzo hayo yameandaliwa kwa pamoja na WCF na CMA. Ili kuwajengea uwezo watumishi hao katika kutekeleza majukumu yao.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kuwajengea uwezo watumishi wa Tume katika Utatuzi wa Migogoro ya Kikazi na Tathmini ya Utendaji Kazi. Mafunzo hayo yaliyowezeshwa kwa pamoja na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, na CMA, yamewaleta pamoja watumishi kutoka Tanzania Bara na yameanza leo Agosti 14, 2018 Mkoani Morogoro.

NA K-VIS BLOG/Khalfan Said, Morogoro

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, ameitaka Tume ya utatuzi wa migogoro ya kikazi na tathmini ya utendaji kazi, (CMA) kuongeza kasi ya kushughulikia migogoro ya kikazi.

Mhe. Mhagama ameyasema hayo leo Agosti 14, 2018 wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa watumishi wa Tume hiyo mjini Morogoro.

“Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imedhamiria kwa dhati kujenga uchumi wa Kati kupitia Viwanda. Hivyo basi, katika kuunga mkono dhamira hiyo ya Serikali, rai yangu kwa Tume ni kuhakikisha kuwa migogoro yote ya kikazi inayohusiana na masuala ya Viwanda inatatuliwa kwa wakati na bila ya upendeleo.” Alisema.

Akifafanua zaidi Mhe. Waziri alisema suala la kutatua migogoro kwa wakati, kwa haki na kwa kuzingatia sheria lina mchango mkubwa katika kudumisha amani na utulivu mahala pa kazi ikiwa ni pamoja na viwandani na kuleta tija, lakini pia kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza nchini. 

Aidha Mheshimiwa Waziri Jenista alisema, Ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wadau hasa wafanyakazi kwamba baadhi ya Wasuluhishi na Waamuzi wanachelewesha maamuzi na baadhi wanatoa uamuzi kwa upendeleo, hivyo kuleta hisia ya kujihusisha na vitendo vya rushwa. 

Alisema, anayotaarifa kwamba, mwaka 2017/2018 mtumishi mmoja (1) aliachishwa kazi kwa tuhuma za rushwa, mmoja (1) alifikishwa mahakamani, na mmoja (1) amepewa onyo kali sana kwa tuhuma ya kuondoka kazini bila ya ruhusa. 

“Nichukue nafasi hii kuuagiza uongozi wa Tume kuendelea kuchukua hatua kali kwa wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa naitaka TAKUKURU kuimulika Tume hii kwa macho yote ili wote wanaotaka kuichafua Tume waondolewe haraka na kukabidhiwa kwenye mkono wa Sheria.”

Ili kutilia mkazo suala la kuzingatia maadili ya kazi, Mhe. Waziri alisema atamuandindikia barua Waziri mwenye dhamana ya Utawala Bora, ili kumchunguza kila mmoja wenu, na hatimaye kuwabaini wote wanaojificha na kufanya vitendo viovu katika kutekeleza majukumu ya kazi. 

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mhe. Waziri, Mkurugrenzi Mkuu wa CMA, Bw.Shanes Nungu alisema, mafunzo hayo yameandaliwa na tume kwa kushriikiana na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), ili kuwajengea uwezo watumishi wa Tume kutoka Tanzania Bara.

Aliishukuru WCF, kwa kuwaunga mkono katika kuandaa mafunzo hayo ambayo yataboresha uwaji bikaji kutokana na kuongezewa ujuzi. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Bw. Masha Mshomba alisema, CMA ni wadau wakubwa wa Mfuko, na kwakuwa wameandaa mafunzo ili kuelimisha watumishi, Mfuko nao umechukua fursa hiyo kuendelea kutoa elimu kuhusu majukumu ya Mfuko, ikiwa ni pamoja na huduma mpya ya usajili wa waajiri kupitia mtandao.

"Wataalamu wetu wako hapa na watatoa elimu kuhusu shughuli mbalimbali za Mfuko, namna ya kufanya tathmini lakini kuhusu masuala ya sheria zinazotuongoza katika kutekeleza majukumu yetu." Alisema Bw. Masha Mshomba. 
Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Bw. Masha Mshomba, akitoa neon la utangulizi.
Waziri Jenista Mhagama, akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mjini, Bi Regina Chonjo.
Picha ya pamoja.
Picha ya pamoja.
Picha ya pamoja na watoa mada.
Baadhi ya washiriki
Kutoka kushoto, Mkurugenzi wa Uendeshaji, Bw. Anselim Peter, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini, Dkt. Abdulsalaam Omary, na Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kisheria wa WCF, Bw. Abraham Siyovelwa.
Mkurugenazi Mkuu wa CMA, Bw. Shanes Nungu, (kulia), akitoa hotuba yake. Kushoto ni Bw. Masha Mshomba.
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kisheria wa WCF, Bw. Abraham Siyovelwa, akitoa mada ambapo alizungumzia maswala ya kisheria yanayohusu Mfuko katika utendaji kazi wake.
Mkurugenzi wa Uendeshaji WCF, Bw. Anselim Peter, akizungumzia muundo wa Mfuko, wajibu mbalimbali kuhusu utekelzaji wa majukumu ya Mfuko, Mwajiri na mwajiriwa.
Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini wa WCF, Dkt. Abdulsalaam Omary, akitoa mada kuhusu hatua mbalimbali ambazo mwajiri na mfanyakazi wanapaswa kuzifuata sambamba na jinsi tathmini inavyofanyika kabla ya zoezi la kulipa fidia halijatekelezwa.
Bw. Ponziano Lukosi, kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kiwasilisha mada, ambapo alielezea shughuli za ofisi ya AG 
Bw.Frank Mwalonga, kutoka Chama Cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), akitoa mada kuhusu namna CMA inavyoweza kushughulikia masuala ya migogoro inapofika mahakamani.
Bw. Mshomba na Bw. Peter wakijadiliana jambo.
Picha ya pamoja meza kuu na watendaji wakuu wa CMA.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano WCF, Bi. Laura Kunenge, (kulia), na Afisa Matekelezo Mkuu wa Mfuko huo Bi. Amina Likungwala, wakijadiliana jambo muda mfupi kabla ya kuanza kwa mafunzo hayo.
Mkurugenzi Mkuu wa CMA, Bw. Shanes Nungu, akisalimiana na baadhi ya washiriki wa mafunzo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad